FILAMU YA "HE HURTS ME" YAZINDULIWA KWA KISHINDO
Mtengenezaji wa filamu ya "He hurts
Me" Bi. Hilda Ngaja (kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na mme wake
Mr. Mwambene (kulia) wakati wa uzinduzi wa filamu yake uliofanyika
katika ukumbi wa Mbezi Garden jijini Dar es Salaam.
PICHA ZOTE NA BENEDICT LIWENGA-MAELEZO, DAR ES SALAAM.
Katibu mtendaji Bodi ya Filamu
Tanzania Bi. Joyce Fissoo amezindua filamu mpya ya "He hurts me"
(ameniumiza au amenitenda), filamu ambayo imetengenezwa na Bi. Hilda
Ngaja hivi karibuni jijini Dar es Salaam.
Bi. Fissoo ametoa pongezi kwa msanii
huyo na Kampuni ya Hilderly Straight Film kwa kuthubutu kwao na
ameongeza kuwa ana imani kuwa wadau haowataendelea kuzalisha filamu
bora, zenye weledi, maadili na zinazoweza kuingia katika soko la
ushindani. Pia amewashukuru washiriki wote kwa kushiriki kwao kikamilifu
katika kufanikisha filamu hiyo.
Bi. Fissoo amesema kuwa filamu ya "He
Hurts Me" (ameniumiza au amenitenda) ni kati ya filamu zinazolenga kutoa
elimu katika jamii na ni filamu inayoweza kuonwa na wanajamii kwani
imejikita katika kuelimisha, kuburudisha, kuadabisha na ni filamu
inayofaa kuingia sokoni.
"Maudhui mahususi ya filamu hii kwetu
sote na jamii kwa ujumla ni katika kutukumbusha umuhimu wa kuwapa malezi
mema watoto wetu, jamii zinazotuzunguka zina watu wa aina na tabia
mbalimbali ambazo kwa kiasi kikubwa zinaathiri nguvu kazi ya taifa".
Alisema Bi. Fissoo.
Aidha, Bi. Fissoo amezungumzia suala
kubwa juu ya malezi kwa watoto na vijana pia akaongeza kuwa ujio wa
filamu hii utakuwa ni chachu na mchango mkubwa katika malezi na umekuja
wakati ambapo taifa linahitaji wazazi na walezi kushiriki ipasavyo
katika kuwezesha watoto na vijana kukua katika misingi ya malezi bora.
Kwa upande mwingine Katibu Mtendaji
huyo amegusia masuala ya ukuaji wa tasnia ya filamu nchini na amesema
kuwa tasnia hii imeendelea kukua kwa kasi sana na hii inadhihirishwa na
idadi kubwa ya filamu zinazozalishwa.
"Vijana na watu wa makundi mbalimbali
wamejikita katika tasnia hii. Ni ukweli usiopingika kuwa tasnia ya
filamu inatoa ajira nyingi". Alisema Bi. Fissoo.
Bi. Fissoo amegusia pia masuala ya
utamaduni na jinsi gani utamaduni unavyoweza kumuathiri ama kumnufaisha
mtu hivyo amesisitiza kuzienzi tamaduni zetu.
"Napenda kuwakumbusha waandaaji wa
filamu na watengenezaji filamu wote nchini kutengeneza filamu
zisizodhalilisha , zisizolenga kuuza tu bali ziwe zinazolinda maadili,
zenye kutumia rasilimali , mandhari na lugha yetu ya kiswahili katika
kutangaza utaifa na utamaduni wetu ; hata majina ya filamu zetu ni vema
yawe kwa lugha ya kiswahili.Tupende na kuenzi utamaduni, maadili na
lugha yetu". Alisisitiza Bi. Fissoo.
Bi. Fissoo alimalizia hotuba yake kwa
kuwaasa wadau wote wa filamu wakiwemo watengenezaji na wasambazaji wa
filamu kuheshimu Sheria na Kanuni zinazosimamia tasnia ya filamu nchini
ambapo kwa sasa mwitikio wake umeanza kuwa mkubwa pia amewasihi kupeleka
sokoni filamu zilizokamilisha taratibu zote na zilizowekwa stamp za TRA
kwani Stamp hizo zina lengo la kuondokana na wizi wa kazi za wasanii
pia amewasihi wadau wote kuunga mkono juhudi za serikali za kurasimisha
tasnia za filamu na muziki kwani nia ya urasimishaji huu ni kurejesha
nidhamu na hadhi katika tasni hizi na kuondokana na kilio cha muda mrefu
ambacho kwa kiasi kikubwa kimefanya wasanii wa filamu na muziki
kutonufaika na jasho lao.
Filamu ya "He hurts Me" (ameniumiza au
amenitenda) imekaguliwa na Bodi na kupewa daraja 16 yaani inaruhusiwa
kuonwa na watu kuanzia miaka 16 nakuendelea.
-MWISHO-
No comments:
Post a Comment