TCAA YATOA UFADHILI KWA MARUBANI WANAFUNZI;
Wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na
Chuo cha 43 Air School nchini Afrika Kusini wakiwa katika picha ya
pamoja wakati wa hafla ya kuwaaga iliyofanyika Jijini Dar es Salaam
katika ukumbi wa Mamlaka ya Usafir wa Anga Tanzania.
Picha zote na ELIPHACE MARWA - MAELEZO (P.T)
Mamlaka ya Usafiri wa Anga kupitia
Mfuko wa Mafunzo watoa ufadhili kwa wanafunzi watano kusomea Urubani na
Uhandisi wa usafiri wa ndege Afrika Kusini.
Akizungumza katika hafla ya kuwaaga
wanafunzi hao Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga, Fadhil
Manongi amesema kuwa kutokana na uhaba wa Marubani na Wahandisi katika
tasnia ya usafiri wa anga Mamlaka ilianzisha mfuko kwa ajili ya
kugharamia mafunzo hayo.
Aliongeza kuwa wanafunzi hao
wamepatikana kupitia michakato mbalimbali ambapo jumla ya wanafunzi 272
waliomba nafasi hizo ambapo waliochaguliwa ni watano na watasoma chuo
cha 43 Air School kilichopo Port Elizabeth nchini Afrika Kusini.
Aidha, Manongi alisema kuwa mafunzo
hayo yatachukua muda wa miaka miwili na yanagharimu jumla ya Dola za
Kimarekani 310,000 ambapo kila moja atatumia dola 62,000 ambazo ni zaidi
ya shilingi milioni mia moja za Tanzania.
Mpaka sasa mfuko una jumla ya Dola za
Kimarekani 250,000 ambazo zimetokana na michango na misaada ya wadau
mbalimbali katika sekta ya usafiri wa anga.
Kwa upande wake Kaimu Mwenyekiti wa
Kamati ya Mfuko wa mafunzo Gaudence Temu amesema kuwa upungufu wa
Marubani na Wahandisi ndiyo changamoto iliwasukuma wadau wa usafiri wa
anga kuanzisha mfuko huo ambao lengo lake ni kuwawezesha wazawa wengi
zaidi kumudu gharama za kusoma kozi za urubani.
Pamoja na hayo wanafunzi hao wameombwa
kuwa wazalendo kwa kurejea nchini na kutumikia taifa lao mara
watakapohitimu mafunzo yao badala ya kutokomea na kunufaisha mataifa
mengine.
Wanafunzi waliopata ufadhili huo ni pamoja na Herman Mushi, Doris Bariki, James John Castico, Linus Mtimba na Calvin Massao
Mwisho.
No comments:
Post a Comment