TIFFAN ENT

TIFFAN ENT

TUKO WANGAPI

TUKO WANGAPI

GLORY FREIGHT

GLORY FREIGHT

Monday, September 23, 2013

BARABARA YA MLIMA KITONGA MKOANI IRINGA KUPANULIWA

Picha-21 d563b
Waziri wa Ujenzi Mheshimiwa Dkt. John Magufuli (katikati) akipewa maelezo na Meneja wa Tanroads mkoa wa Iringa Eng. Poul Lyakurwa wakati alipokuwa akipita kukagua eneo la Kitonga katika barabara ya TANZAM mkoani Iringa. Wengine katika picha ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi Eng. Joseph Nyamhanga (kulia) na Eng. Chrispianus Ako kutoka Tanroads Makao Makuu (wa kwanza Kushoto) pamoja na watendaji wengine kutoka Wizara ya Ujenzi.(hd)
Kujifunga kwa barabara katika eneo la Kitonga katika barabara kuu ya TANZAM kumekuwa kukisababisha adha kubwa kwa wasafiri. Eneo hilo liko mkoani Iringa katika barabara kuu inayoanzia jijini Dar es Salaam ikiunganisha na mikoa ya kusini magharibi mwa nchi yetu pamoja na nchi jirani za Zambia, Congo DR na Malawi.
Barabara katika sehemu ya Kitonga inapita katika muinuko mkali ambapo inapotokea ajali au gari kuharibika, huwa ni vigumu kwa magari mengine kupita hadi gari lilizoba njia liondolewe.
Hivi karibuni Waziri wa Ujenzi Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli alikutana na Mkuu wa Mkoa wa Iringa Mheshimiwa Dkt. Christine Ishengoma ambapo pamoja ya mambo mengine yaliyozungumziwa katika kikao hicho, lilijitokeza suala la kujifunga mara kwa mara kwa barabara ya TANZAM katika eneo la Kitonga.
Meneja wa Tanroads mkoani Iringa Injinia Poul Lwakurwa alimfahamisha Waziri wa Ujenzi kuwa, pale inapotokea ajali au gari kuharibika na kufunga njia, husababisha msongamano mkubwa wa magari na hata upelekaji wa msaada huwa mgumu na huchukua muda mrefu kutokana na wembamba wa barabara katika eneo hilo pamoja na kutokuwepo kwa barabara mbadala jirani.
Mheshimiwa Magufuli wakati akihitimisha ziara yake mkoani Iringa alitembelea eneo la Kitona na kujionea hali halisi na kuiagiza Tanroads kumpatia taarifa mapema iwezekanavyo juu ya hatua za muda mfupi na muda mrefu ambazo watachukua ili kuondoa adha hiyo ya kujifunga barabara mara kwa mara.
Mwakilishi wa Mtendaji Mkuu wa Tanroads aliyekuwepo katika ziara hiyo Injinia Chrispianus Ako alimtaarifu Waziri wa ujenzi kuwa tayari Tanroads imaenza mchakato wa kupanua barabara katika eneo hilo ikiwa ni pamoja na kutafuta barabara mbadala jirani na eneo hilo.
Serikali tayari imekwishatumia fedha nyingi kuijenga kwa zege sehemu hiyo ya Kitonga kilometa zote 7 badala ya kutumia lami ya kawaida ili kudhibiti uharibifu uliokuwa ukisababishwa na magari yanayozidisha uzito au kumwaga mafuta barabarani. Mafuta hasa petrol na diseli yakimwagika katika barabara za lami huidhoofisha na kusababisha kubomoka. Hata hivyo kwa upande wa barabara za zege mafuta husababisha utelezi ambao wakati wa mvua huweza kusababisha ajali hasa katika maeneo yenye miinuko mikali kama ilivyo kwa sehemu ya hiyo ya Kitonga.

No comments:

Post a Comment