OFISI YA MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI YAFUNGUA OFISI 23 KATIKA MIKOA MBALIMBALI
Wakili wa serikali Mkuu, Ofisi ya
Mwanasheria Mkuu wa Serikali Bw. Frederick Manyanda (kulia) akieleza kwa
waandishi wa (hawapo pichani) mkakati wa kuhakikisha kuwa huduma ya
usimamizi na utoaji wa haki inawafikia wananchi wote kwa karibu kwa
kufungua ofisi zaidi Mikoani, Katika mkutano uliofanyika ukumbi wa Idara
ya Habari(MAELEZO) leo Jijini Dar es Salaam,katikati ni Afisa Habari
toka ofisi hiyo Bi. Asiatu Msuya na Kulia kushoto ni Afisa Habari wa
Idara ya Habari Bi. Georgina Misama.(P.T)
Afisa Habari, Ofisi ya Mwanasheria
Mkuu wa Serikali Bi. Asiatu Msuya (kushoto) akieleza kwa waandishi wa
Habari (hawapo pichani) kuhusu ufunguaji wa ofisi 23 katika mikoa
mbalimbali nchini ili kutekeleza Mpango wa kutenganisha Upelelezi na
uendeshaji wa Mashtaka, wakati wa mkutano uliofanyika ukumbi wa Idara ya
Habari (MAELEZO) leo Jijini Dar es Salaam. Kulia ni Wakili wa serikali
Mkuu wa Ofisi hiyo Bw. Frederick Manyanda.
PICHA NA HASSAN SILAYO> MAELEZO
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
OFISI YA MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
OFISI
YA MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI YAFUNGUA OFISI 23 KATIKA MIKOA
MBALIMBALI KUFANIKISHA MPANGO WA UTENGANISHWAJI WA SHUGHULI ZA UPELELEZI
NA UENDESHAJI WA MASHTAKA NCHINI
______________________________
Utangulizi
Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali
imefanikiwa kufungua Ofisi 23 katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani,
Tanga, Kilimanjaro (Moshi), Arusha, Mwanza, Kagera (Bukoba) Mara
(Musoma), Shinyanga, Tabora, Singida, Iringa, Mbeya, Mtwara, Lindi,
Dodoma, Rukwa (Sumbawanga),Ruvuma (Songea), Njombe,
Manyara,Morogoro,Kigoma,Geita na Pwani. Aidha jumla ya Ofisi mbili (2)
za zimefunguliwa katika Wilaya za Temeke na Monduli. Kwa mwaka wa fedha
2012/2013 pekee jumla ya Ofisi tano (5) zimefunguliwa katika mikoa ya
Pwani, Kigoma, Morogoro, Manyara, Njombe na Geita ikiwemo pia Ofisi
mbili za Wilaya.
Lengo
Lengo kuanzishwa na kuimarishwa kwa
Ofisi hizi za Mikoa na Wilaya ni kuhakikisha kuwa huduma ya usimamizi na
utoaji wa haki inawafikia wananchi wote kwa karibu zaidi. Baadhi ya
huduma zinazotolewa ni pamoja na kuendesha Mashtaka mahakamani,
kushughulikia malalamiko na kero za wananchi kuhusiana na kesi za jinai
na madai zinazowakabili, kutembelea mahabusu na kuratibu upelelezi wa
kazi za upelelezi wa makosa ya jinai zinazofanywa na vyombo
pelelezi/chunguzi ikiwemo Polisi, Magereza, Uhamiaji,TAKUKURU.
Utekelezaji wa Mpango wa kutenganisha Upelelezi na Mashtaka nchini
Serikali kupitia Ofisi ya Mwanasheria
Mkuu wa Serikali imeendelea kutekeleza mpango huu wa Utenganishwaji wa
Upelelezi na Mashtaka kwa mujibu wa Sheria ambapo mfumo wa Sheria ambao
uliwezesha kutungwa kwa Sheria ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu, 2005 na
Sheria ya Usimamizi wa Uendeshaji Mashtaka nchini, 2008 umeboreshwa;
pamoja na kuanzishwa kwa Jukwaa la Ki-taifa la Haki-Jinai (National
Criminal Justice Forum) Desemba 2009 linaloviunganisha pamoja vyombo
vyote vinavyosimamia utolewaji wa Haki-Jinai nchini;
Serikali pia imeboresha Muundo wa
Divisheni ya Mashtaka kwa kuweka Sehemu (Section) mahsusi inayosimamia
utekelezaji wa mchakato wa utenganishaji wa kazi za upelelezi na
Mashtaka na uratibu wa kazi za ki-pelelezi; pamoja na kuanzishwa kwa
huduma ya Mashtaka ya moja kwa moja ambako Mawakili wa Serikali
wanaendesha kesi; Hii imepelekea idadi ya kesi zinazofunguliwa
Mahakamani ambako Mawakili wa Serikali wanaendesha Mashtaka kupungua
ikilinganishwa na kipindi cha nyuma; Kuongezeka kwa ubora wa huduma
zitolewazo na kupungua kwa kesi za kubambikizwa.
Utekelezaji wa Programu ya
Utenganishwaji wa Mashtaka na Upelelezi (Civilianization) imetoa msukumo
mkubwa kwa Ofisi kuingia uanachama na makubaliano ya mashirikiano na
vyama vinavyohusiana na kazi za Uendeshaji Mashtaka duniani, kama
vile-IAP, HOPAC, APA, EAAP, na ARINSA; Serikali itaendelea kupanua wigo
wa uendeshaji wa Mashtaka kwa kuanzisha na kuimarisha Ofisi katika
Wilaya zote nchini pamoja na Mikoa miwili iliyobaki ya Katavi na Simiyu.
Tunapenda kuwakumbusha Wadau wetu wote
na Wananchi kwa ujumla kuwa mstari wa mbele katika kutoa taarifa za
uhalifu au jinai yoyote katika jamii kwa vyombo husika kupitia utaratibu
unaofaa; na kutoa ushahidi Mahakamani pale unapohitajika kwa kuwa hizi
ni nguzo muhimu katika uendeshaji wa kesi mbalimbali. Aidha tunatoa wito
kwa umma, wadau wetu na wananchi wote kwa ujumla pamoja na vyombo vya
habari nchini kufuatilia mtiririko, hoja zinazowalishwa Mahakamani na
uamuzi uliotolewa na Mahakama katika kesi mbalimbali zinazoendelea kuwa
na taarifa sahihi ya kuhusu kesi hizo.
Imetolewa Na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali
Ijumaa, Septemba 27, 2013
Kwa mawasiliano zaidi
OFISI YA MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI
SLP 9050
KIVUKONI FRONT
DAR ES SALAAM
SIMU: +255 22 21181778
NUKUSHI: +255 22 2113236
BARUA PEPE:
info@agctz.go.tz
TOVUTI: www.agctz.go.tz
No comments:
Post a Comment