Jaji Mutungi aiumbua CCM
HATIMAYE
Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi ameanza kuonyesha
makali, baada ya kukipa onyo kali Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kukitaka
kuacha mara moja kutumia viongozi wa kidiplomasia kwenye shughuli za
kisiasa.
Hatua ya
Jaji Mutungi, imekuja siku chache baada ya CCM kumtumia Balozi wa China,
Dk. Lu Youping katika shughuli za kisiasa mkoani Shinyanga wiki
iliyopita.(hd)
Taarifa
iliyotolewa kwa vyombo vya habari mjini Dar es Salaam jana, ilisema
suala la ushiriki wa raia wa kigeni ikijumuisha wanadiplomasia katika
shughuli za kisiasa nchini, halikubaliki.
Alisema
ofisi yake, inaunga mkono kwa dhati hatua iliyochukuliwa na Serikali
kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, kukemea
jambo hilo.
"Tamko la
Serikali limezingatia sheria na wajibu wa wanadiplomasia, wakati wa
uwepo wao hapa nchini, mimi nikiwa mlezi wa vyama vya siasa, ninakemea
kitendo cha CCM kumshirikisha Balozi wa China katika shughuli za
kisiasa," alisema Jaji Mutungi.
Alisema
katika tukio hilo, CCM kuruhusu raia wa kigeni kutumia jukwaa lake ni
dhahiri limezua hali ya taharuki kwa wananchi, japo sheria ya vyama vya
siasa kwa upande wake iko kimya katika suala hilo.
"Naviasa
vyama vya siasa kwa ujumla wake, kuzingatia na kufuata sheria na
taratibu stahiki katika utekelezaji wa shughuli zao za kisiasa.
"Napenda
kuujulisha umma kwamba, ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kwa wakati
huu ipo kwenye mchakato wa marekebisho ya sheria husika ya vyama vya
siasa, ambayo imebainika kuwa na upungufu....lengo ni kukabiliana na
changamoto zilizopo likiwemo suala hili," alisema Msajili, Jaji Mutungi
katika taarifa yake aliongeza sasa hivi ofisi yake inaendelea kukusanya maoni ya wadau katika jitihada za kufanikisha marekebisho ya sheria hiyo.
Suala la
CCM kumshirikisha Balozi wa China katika masuala ya kisiasa, lilizua
mjadala mkubwa hali iliyosababisha CHADEMA kutoa tamko na kuandika barua
ya malalamiko UN wakitaka aondolewe kwa kupoteza sifa za kuwa balozi,
baada ya kuvunja mkataba wa Umoja wa Mataifa wa 1961 unaosimamia nchi na
nchi.
CHADEMA
waliandika barua nyingine kwenda Serikali ya China na Tanzania, wakitaka
msimamo na hatua zitakazochukuliwa dhidi ya balozi huyo kuvunja mkataba
huo ibara ya 41(1-3), kinachokataza balozi kujihusisha na siasa katika
Taifa ambalo yuko.
Chadema
imesema inalaani kitendo hicho na itachukua hatua kwenda Umoja wa
Mataifa na pia kupata maelezo toka Serikali ya China kama imemtuma
balozi huyo kujihusisha na mambo ya siasa za ndani za vyama au
kuiwakilisha nchi.
Akijibu
tuhuma hizo, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema
alichofanya balozi huyo ni kitendo cha kuungwa mkono, maana alikuwepo
kwa nia ya kuangalia maeneo ya uwekezaji wa zao la Pamba katika Mkoa wa
Shinyanga.
Alisema
uwekezaji kutoka China, utasaidia kuondoa tatizo sugu la ajira, kupanda
kwa bei ya zao la pamba ambacho kimekuwa kilio kikubwa cha wakulima
pamoja na ujengwaji wa viwanda vya nguo na kuchuja mafuta.
Hivyo ni
vema kumpongeza balozi huyo na kuunga juhudi za CCM za kuwatafuta
wawekezaji wa nje, badala ya kusingizia uvunjaji wa Mkataba wa Vienna
ili kupata umaarufu wa kisiasa:chanzo mtanzania
No comments:
Post a Comment