Mzee Mwinyi awaonya wanaotumia Elimu na ujuzi wao kuangamiza Ustawi wa Jamii
Baadhi ya wageni waalikwa waliohudhuria sherehe hizo.
.awaasa vijana kutotumiwa na wanasiasa kwa maslahi yao
.ashangaa wajuzi walivyompachika jina la Ruksa enzi za miaka 1990s
Na.Mo Blog Team
Rais Mstaafu wa awamu ya pili, Alhaji
Ali Hassan Mwinyi amesema kuna baadhi ya watu katika jamii hutumia
elimu, ujuzi na maarifa yao kuangamiza, kubomoa na kudumaza Ustawi wa
Jamii kwa maslahi binafsi na si ya Umma. Mo blog inaripoti.
Mzee mwinyi amesema hayo wakati wa
kuadhimisha siku ya Kimataifa ya Amani Duniani inayoadhimishwa 21th
Septemba kila mwaka ambayo imefanyika katika ukumbi wa Don Bosco jijini
Dar es Salaam, amesema kuna baadhi ya watu wanatumia elimu yao vibaya
kwa kupanga kuua watu wengine kwa maslahi yao aidha ya kisiasa au ya
kiuchumi.
"Elimu kwa kawaida kuleta matokeo
mazuri kwa jamii husika endapo itatumika sawia kwa malengo
yaliyokusudiwa na kwa maendeleo endelevu ya taifa kwa ujumla, ila kuna
baadhi ya wanajamii kutumia ujuzi huu vibaya na kuangamiza ustawi wa
jamii husika," amesema.
Mzee Mwinyi aliendelea kusema kwamba
katika kuadhimisha siku ya kimataifa ya amani duniani yenye kauli mbiu
"Education for Peace" ni lazima elimu kwa ajili ya amani iwe endelevu
hapa duniani ili iweze kuleta suluhu na utengamano katika jamii na
mataifa yote duniani.
Amesema kwamba vijana nchini lazima
waepuke kutumiwa na wanasiasa kwa maslahi yao ya kisiasa na wajifunze
kutatua matatizo yao kwa njia ya amani bila ya kuwa na mihemko, jazba,
misongo na hasira ili kuendelea kudumisha amani na upendo katika nchi
yetu ambayo ni kisiwa cha amani.
"nawaasa vijana wakitanzania wa leo
hata kama mmenyimwa haki zenu ni bora kutumia njia ya kistaarabu na
kutumia elimu mnayopata mashuleni bila kusahau macho, masikio na vipawa
vyenu mlivyopewa na mwenyezi mungu katika kutafuta haki yenu kwa njia ya
amani bila misukosuko," aliongeza.
Mzee Mwinyi alitumia nafasi hiyo
kuwashangaa baadhi ya watu kwa kutumia ujuzi na elimu yao kwa kumpachika
jina la Ruksa bila yeye kujua wametumia muktha gani kumpa jina hilo,
lakini Mzee Mwinyi alitumia jukwaa hilo pia kuwapa ruksa vijana kutumia
elimu yao kuleta hali ya amani na utulivu ndani ya nchi.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Shirika
la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto (UNICEF) Jama Gulaid amesema
kwamba Umoja wa Mataifa uliweka maazimio siku ya kimataifa ya amani
duniani ili watu wanaogombana na kupigana kwa shida mbalimbali kupata
nafasi ya kuweka silaha zao chini katika siku hii adhimu.
Amesema kupitia azimio hilo ambalo
lilizinduliwa mwaka 1982 kwa mara kwanza linatambua uwepo wa watu
wanaoathirika na vita katika sehemu mbalimbali duniani na
waliokwishapoteza maisha kutokana na matatizo vita vya wenyewe kwa
wenyewe.
Naye Mratibu na Mtathimini wa Mtandao
wa watoto na vijana kutoka Imani Mbalimbali (GNRC) Bi, Joyce Mdachi
amesema swala la amani na utulivu linaanzia kwenye kaya hadi ngazi ya
taifa kwahiyo ni muhimu kwa jamii na vijana kuelewa amani inaanzia
nyumbani.
"jamii iliyolelewa katika mazingira
mazuri ina nafasi kubwa ya kuleta matokeo chanya kwenye mustakabali wa
taifa kwa ujumla lakini jamii iliyolelewa vibaya haiwezi kubadilisha
taifa kwa sababu ni zao la tunda baya," alisema.
Mdachi alisisitiza kwamba kuporomoka
kwa maadili ndani ya jamii ya leo swala hilo pia lilianzia kwenye kaya
ya mtu mmoja mmoja hadi ngazi ya taifa ambapo leo hii taifa linashuhudia
mambo ya kifisadi, rushwa na ubadhilifu wa mali za umma kunakofanywa na
viongozi waandamizi.
No comments:
Post a Comment