TIFFAN ENT

TIFFAN ENT

TUKO WANGAPI

TUKO WANGAPI

GLORY FREIGHT

GLORY FREIGHT

Saturday, September 14, 2013

SAMAKI HATARI WAINGIZWA NCHINI

samaki_df55c.jpg
Afya za Watanzania ziko shakani kutokana na kuwapo kwa biashara ya kuingiza samaki kutoka nje ya nchi, wanaodaiwa kuharibika na kuuzwa katika la Soko la Feri jijini Dar es Salaam.
Samaki hao kutoka Yemen, Dubai, China na Japan, wanaoingizwa nchini wakiwa wameganda kwenye barafu, wengi huharibika muda mfupi baada ya barafu kuyeyuka au baada ya kununuliwa.(P.T)
Uchunguzi wa gazeti hili umegundua kuwa samaki hao huletwa nchini kutafutiwa soko baada ya kukaa kwenye majokofu kwa muda mrefu huko wanakotoka, kiasi cha kuelekea kuharibika.
Ili wasiharibike, samaki hao aina ya Marckerel hukaangwa hadi wakauke. Uchunguzi zaidi umebaini kuwa wanunuzi wake wakuu ni wafanyabiashara wa chakula wakiwamo wamiliki wa migahawa na Mama Lishe wanaofanya shughuli zao katika miji ya Dar es Salaam, Pwani, Morogoro na Dodoma.
Samaki hao wanauzwa kwa bei ya chini ambayo ni Sh38,000 kwa boksi lenye uzito wa kilo 15, ikilinganishwa na wanaovuliwa hapa nchini ambao bei yake ni Sh60,000, kwa uzito huohuo.
Inaelezwa kuwa samaki hao baadhi yake ni waleambao wamekwisha muda wake wa kutumika katika nchi hizo, hivyo kuingizwa nchini kutafutiwa soko.
Gazeti hili lilifika katika soko hilo kwa siku mbili na kushuhudia samaki hao wakiuzwa kwa wingi, huku wauzaji wakihimizwa wateja wao kuwahi kuwakaanga au kuwaweka kwenye jokofu.
Gazeti hili pia lilinunua boksi moja la samaki hao lenye uzito wa kilo 15 kwa Sh38,000, lakini lilipodai kupewa stakabadhi wauzaji walisema: "Hatuna stakabadhi ya kukupa ndugu yangu," alisema muuzaji.
Baada ya kuwasafirisha kutoka Soko la Feri hadi ofisi za gazeti hili zilizopo Tabata Reli, Barabara ya Mandela kwa muda wa saa moja, tayari walikuwa wameharibika.
Baadhi ya samaki hao walianza kuoza huku wengine wakiwa wamelegea tofauti na samaki wa kawaida. Baada ya saa nne kupita, samaki hao waliharibika na kuanza kutoa harufu mbaya.
Dk Raymond Mwenekano wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, anayataja madhara ya ulaji wa samaki wa aina hiyo kuwa ni kupata magonjwa kama vile kansa ya utumbo, mwili kuwasha, kubabuka na vidonda mwilini.
"Madhara yake ni makubwa, ndiyo maana siku zote tunasisitiza kula vyakula visivyokaa sana kwani vingine vimehifadhiwa kwa dawa na wanaofanya hivi ni wafanyabiashara kwa faida yao," alisema Dk Mwenekano.
Daktari huyo alisema pia yapo madhara ya muda mfupi ambayo ni mtu aliyekula samaki wa aina hiyo kuharisha na kutapika muda mfupi baada ya kula.
Mamlaka husika
Ofisa Afya katika Soko la Feri, Barnabas Hanje alithibitisha kuwepo katika soko hilo, samaki wabovu wanaotoka nje ya nchi na kwamba ofisi yake imekuwa ikipokea malalamiko mengi kuhusu suala hilo.
Hanje ambaye pia alitajwa kuwa ni Mwakilishi wa Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA) katika soko hilo, alisema kesi zinawahusu wanunuzi wanaodai warejeshewe fedha au kubadilishiwa samaki, baada ya wale waliowanunua kuharibika haraka hata kabla hawajatoka sokoni hapo.
Alifafanua kuwa baadhi ya kesi hupata ufumbuzi baada ya waliouza samaki wabovu kukubali kurejesha fedha kwa wahusika na kwamba kwa pale mwagizaji wa jumla anapokataa kurejesha fedha kesi hizo hupelekwa mahakamani.
"Sina idadi kamili ya kesi, lakini kesi kama hizo ni nyingi na baadhi yake tuliposhindwa kuwapatanisha watu wawili mnunuzi na muuzaji tuliwaambia waende mahakamani, lakini nakiri ni kweli jambo kama hilo lipo," alisema Hanje.
Ofisa Uvuvi wa Manispaa ya Ilala, Msongo Songoro alisema wamekuwa wakipata changamoto nyingi kuhusiana na suala hilo ndiyo maana wameanza mchakato wa kutambua kampuni zote zinazoingiza katika Soko la Feri samaki kutoka nje ya nchi.
Alisema hadi sasa wamebaini kuwapo kwa kampuni 20 na kati ya hizo ni sita pekee ambazo zimewasilisha uthibitisho wa kufuata sheria pale wanapoingiza shehena ya samaki nchini. Songoro aliongeza kuwa kaributani moja na nusu ya samaki hao kutoka nje wanauzwa kila siku katika Soko la Feri.
"Niliwahi kupata kesi kama hizo ambapo nilichukulia kama changamoto na kuanza kufanya hiki ninachokifanya sasa na hadi sasa ni kampuni sita pekee ambazo wameniletea vibali vyao vinavyoonyesha uhalali wa kuagiza shehena ya samaki kutoka nje kati ya kampuni 20 ambazo zinaagiza,"alisema Songoro.
Songoro alivitaja vitu ambavyo kila kampuni inatakiwa kuviwasilisha kwao kuwa ni pamoja na Cheti cha Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Cheti cha Usajili wa kampuni, Cheti cha TFDA, leseni ya biashara na vibali vyote vinavyoruhusu kuingiza samaki nchini.
Ofisa Maliasili wa Manispaa ya Ilala, Charles Seche, alisema hatua walizochukua ni mwanzo lakini lengo ni kuondosha bidhaa zote zisizo na ubora katika soko hilo.
Ofisa Uhusiano wa TFDA, Gaudencia Simwanza alipoulizwa alisema hafahamu kuhusu uwepo wa samaki wabovu na kuahidi kwamba angekwenda kulijadili na wahusika.
Alimtaka mwandishi wa habari amwambie samaki hao wameanza kuingia lini nchini, wanatoka nchini gani na wanaitwaje, ili aweze kuwasiliana na wahusika wa idara ya chakula.
"Wewe ndiyo unaniambia nitaiwasilisha kwenye idara ya wahusika wa chakula moja kwa moja waifanyie kazi na baada ya kukamilisha uchunguzi nitakupa taarifa," alisema Simwanza.
Alipohojiwa baada siku moja, Simwanza alisema jukumu la TFDA ni kuangalia mzigo ambao unaingizwa kwa wingi na hii ni baada ya kupokea sampuli na kuridhishwa nao, kisha hutoa kibali kwa ajili ya kuruhusu uingizwe.
"Kazi yetu sisi ni hiyo kwa mzigo uliopo sokoni hasa wa vyakula muhusika mkuu ambaye tunafanya naye kazi kwa karibu ni ofisa afya wa soko ambaye ndiye ana wajibu wa kukagua mzigo na kuangalia una tatizo gani,"alisema Simwanza.
Simwanza alifafanua kuwa hata wanapotoa kibali cha kuingiza mzigo siyo mwisho, kwani unapowasili huwa unafanyiwa ukaguzi mwingine uwapo bandarini na ukigundulika una matatizo unazuiliwa.

No comments:

Post a Comment