Rais Kikwete aongeza viongozi wanaotakiwa kutangaza mali zao
Washirikiwa wa Semina wakiwa katika
picha ya pamoja na Mgeni Rasmi wa ufunguzi wa Semina hiyo, Waziri wa
Nchi Ofisi ya Rais Utawala Bora George Mkuchika (aliyekaa katika mstari
wa mbele).Wa kwanza kushoto waliokaa ni mwakilishi wa Shirika la Misaada
la Marekani USAID.
Hussein Makame
RAIS Jakaya Kikwete ameongeza vyeo vya
wa viongozi wa umma wanaowajibika na Sheria ya Maadili ya Viongozi wa
Umma ambao watapaswa mara moja kujaza fomu za kutangaza mali walizonazo
kila mwaka.
Hayo yamesemwa na Kamishna wa
Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Jaji Mstaafu Salome Kaganda
katika Semina ya Wahariri wa Vyombo vya Habari iliyofanyika katika
hoteli ya Peacock jijini Dar es Salaam Septemba 12 mwaka huu.
Jaji Mstaafu Kaganda alisema kuwa
nyongeza hiyo iliyotiwa sahihi na Rais Kikwete Agosti 14 mwaka huu na
tayari na imeshatoka kwenye gazeti la Serikali, inaongeza wigo wa
viongozi wa umma wanaotakiwa kutangaza mali zao.
Alitaja vyeo vya viongozi hao
walioongezwa kuwa ni Msajili wa Hati, Wasajili Wasaidizi wa Hati wa
Kanda, Makamishna Wasaidizi katika Taasisi za Umma, Wakuu wa Hazina
ndogo, Wakuu wa Idara na Vitengo na sehemu za ugavi na manunuzi katika
Wizara, Idara za Serikali, Wakala wa Serikali na Mamlaka za Serikali za
Mitaa.
Wengine ni Mtendaji Mkuu Shirika la
Magazeti ya Serikali (TSN),Makanali wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania,
Waratibu wa Miradi katika Wizara, Idara, Wakala na Taasisi za Umma,
Waganga Wakuu wa mikoa, Watendaji Wakuu wa Taasisi, Makatibu,
Wakurugenzi na Mameneja katika Taasisi za Umma.
Viongozi wengine walioongezwa ni
Msajili wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba, Wasajili Wasaidizi wa Baraza la
Ardhi na Nyumba wa Kanda, Wenyeviti wa Barza la Ardhi na Nyumba la
Wilaya, Wakuu wa Idara na Vitengo vya Serikali za Mitaa, Wakuu wa Polisi
wa Wilaya(OCDs), Wakuu wa Upelelezi wa Wilaya(OCCIDs), Wakuu wa
Upelelezi wa Mikoa(RCOs),Maafisa Usalama wa Wilaya na Mikoa.
Akizungumza katika ufunguzi wa semina
hiyo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utawala Bora George Mkuchika aliwaasa
wahariri wa vyombo vya habari na waandishi kwa ujumla kutumia kalamu
zenu na midomo yao katika kuheshimu maadili ya kazi zao ili kutoa
mchango katika kuijenga Tanzania.
Alisema vyombo vya habari vinayo fursa
ya kuishawishi jamii kuendeleza yale mema yaliyo katika jamii, hivyo
aliwaomba wanahabari kuhakikisha kwamba wanatumia kalamu zao kuendeleza
umoja na amani nchini.
Naye Mkurugenzi wa Idara ya Habari
MAELEZO, Assah Mwambene aliviasa vyombo vya habari kuacha kuwa sehemu ya
kuendeleza ajenda za watu badala ya kutekeleza moja ya majukumu yao ya
kuweka ajenda zenye muelekeo wa kuijenga jamii ya Watanzania.
Akifafanua juu ya semina hiyo, Waziri
Mkuchika alisema semina hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa
kujenga uelewa kwa umma kuhusu Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma,
unaofadhiliwa na Shirika la Misaada la Marekani USAID.
"Lengo ni kuhakikisha kuwa kila mdau
wakiwemo waandishi wa habarai wanashiriki kikamilifu kuunga mkono
jitihada za Serikali kujenga misingi imara ya maadili na utawala bora
ili kuongeza kasi ya maendeleo endelevu katika nchi yetu" alisema Waziri
Mkuchika
Alisema kuwa Sekretarieti ya Maadili
ya Viongozi wa Umma ni chombo kilichoundwa kikatiba kwa mujibu wa Ibara
ya 132 ya Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na kupewa dhamana
ya kusimamia maadili ya viongozi wa Umma iliyoainishwa katika Sheria ya
Maadili ya Viongozi wa Umma namba 13 ya mwaka 1995.
Alibainisha kuwa lengo la Sheria hiyo
ni kuhakikisha kwamba viongozi wa umma wanatekeleza majukumu yao kwa
namna ambayo wanadumisha na kukuza imani na heshima ya wananchi kwa
Serikali yao.
Akizungumzia vyeo vya viongozi
walioongezwa na Rais Kikwete kutangaza mali zao, Waziri Mkuchika alisema
kuwa Sheria imeweka kifungu kinachomruhusu Rais kuongeza idadi ya
viongozi wanaotakiwa kutangaza mali zao kila mwaka kwa kadri atakavyoona
inafaa kwani hawakuwepo wakati wa kutungwa sheria hiyo.
Mada zilizowasilishwa kwenye semina
hiyo ni Umuhimu wa Maadili katika Maendeleo ya Nchi, Sheria ya Maadili
ya Viongozi wa Umma na Majukumu ya Sekretarieti ya Maadili na Nafasi ya
Vyombo vya Habari Katika Kusimamia Maadili na Utawala Bora katika Jamii,
ambayo ilikuwa maudhui kuu ya semina hiyo.
No comments:
Post a Comment