KHAMENEI: IRAN KUIUNGA MKONO SYRIA HADI MWISHO
Kiongozi mkuu wa kidini wa Iran,
Ayatollah Ali Khamenei, amesema Marekani inayatumia mashambulizi ya
kemikali nchini Syria kama kisingizio cha kuivamia nchi hiyo
inayokabiliwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Aidha, ameionya Marekani kutokana na
hasara itakazopata iwapo itafanya uvamizi wowote ule. Ama kwa upande
mwingine, Umoja wa Ulaya umelipinga suala la kuivamia Syria kijeshi.(P.T)
Akizungumza kwenye mkutano wa baraza
la wataalamu, Khamenei amesema kuwa Marekani inajifanya kujiingiza
katika mzozo wa Syria kwa kuzingatia zaidi suala la hali ya kibinaadamu
na kwamba mashambulizi ya kutumika kwa silaha za kemikali, ni kama
kisingizio kwao na kwamba nchi hiyo itajiingiza katika hasara kubwa
iwapo itaivamia Syria kijeshi.
Iran kuendelea kumuunga mkono Rais Assad
Matamshi ya Khamenei yanaonyesha
dalili za kutoacha kumuunga mkono mshirika wake wa karibu, Rais Bashar
al-Assad, ambaye anashutumiwa na mataifa ya Magharibi kwa kutumia gesi
ya sumu katika mashambulizi ya Agosti 21 mwaka huu dhidi ya raia. Kwa
mujibu wa maafisa wa Marekani, kiasi watu 1,400 waliuawa katika
mashambulio hayo.
Jana Jumatano (04.09.2013), mkuu wa
kundi la Quds lenye mafungamano na Iran, Qassem Soleimani, aliliambia
baraza la watalamu kwamba Iran itaiunga mkono Syria hadi mwisho.
Ama kwa upande mwingine, Urusi
imeionya Marekani kwamba mashambulizi yoyote ya kijeshi dhidi ya Syria
bila ya idhini ya Umoja wa Mataifa, yanaweza kuwa na madhara makubwa
kama kombora litaangukia kwenye kiwanda kidogo cha madini ya uranium
kilichoko karibu na Damascus.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Urusi,
imelitaka shirika la Umoja wa Mataifa linalosimamia masuala ya nyuklia,
kutathmini haraka hatari itakayoweza kutokea, wakati Marekani inafikiria
kuiadhibu serikali ya Syria kutokana na kuituhumu kutumia gesi yenye
sumu.
Umoja wa Ulaya waizungumzia Syria
Wakati huo huo, Rais wa Umoja wa Ulaya
Herman Van Rompuy na Rais wa Halmashauri Kuu ya Ulaya, Jose Manuel
Barroso, wamezungumza suala la kuivamia Syria kijeshi, huku wakiipinga
hatua hiyo.
Akizungumza leo na waandishi wa habari
kabla ya kuanza kwa mkutano wa viongozi wa kundi la nchi zinazoongoza
kiuchumi duniani-G20 unaofanyika mjini St. Petersburg, Van Rompuy
amesema kuwa wanaheshimu wito wa Syria kuvamiwa kijeshi, lakini
wanahitaji kuusogeza mbele mchakato wa Umoja wa Mataifa.
Kwa upande wake Barroso amesema
jumuiya ya kimataifa haiwezi kukaa kimya baada ya kutokea kwa
mashambulizi hayo ya Agosti 21 ambapo silaha za kemikali zinadaiwa
kutumika na kutoa wito kwa Umoja wa Mataifa kuitangaza mapema
iwezekanavyo ripoti ya awali ya wakaguzi wa umoja huo.
Katika hatua nyingine kiongozi wa
Kanisa Katoliki duniani, Baba Mtakatifu Francis, amemuandikia Rais wa
Urusi, Vladmir Putin barua, akitoa wito kwa viongozi katika mkutano huo
kutafuta njia ya kuepusha mashambulizi ya kijeshi dhidi ya Syria, ambayo
amesema hayana faida yoyote.
No comments:
Post a Comment