Taharuki kubwa yaibuka katika mpaka wa Rwanda na Tanzania.
Taharuki imeibuka katika mpaka wa Tanzania na Rwanda wakati madereva wa malori kutoka nchini wakihaha kuvuka kuingia Rwanda kabla ya kuanza kutumika kwa ushuru mpya wa barabara ambao unaanza kutumika tena leo kwa upande wa Rwanda ukilenga magari kutoka Tanzania tu.
Rwanda iliongeza ushuru kwa zaidi asilimia 229 dhidi ya magari ya mizigo ya Tanzania tu kutoka viwango vya zamani vya Dola za Marekani 152 hadi Dola 500 kwa madai ya kutaka usawa na Tanzania.
Ushuru huo ambao ulianza kutumika rasmi Septemba mosi mwaka huu kisha kusitishwa kwa muda, unatarajiwa kurejeshwa tena leo kulingana na tangazo la Rwanda mpakani Rusumo.
Kadhia hiyo imesababisha msururu mrefu wa malori yanayoingia Rwanda kutoka Tanzania kuanzia jana ambayo ilikuwa siku ya mwisho kabla ushuri huo wa kutoka Dola za Marekani 152 hadi 500 kuanza kutozwa tena kuanzia leo.
Kaimu Ofisa Mwandamizi wa Forodha wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) katika kituo cha Rusumo, Sure Mohamed, jana alilithibitisha NIPASHE kwamba wiki moja iliyopita serikali ya Rwanda iliweka ongezeko la ghafla la ushuru wa barabara kutoka Dola 152 hadi Dola 500 za Marekani.
Alisema hali hiyo ilisababisha msururu mrefu wa magari umbali wa zaidi ya kilometa 20 kwa kuwa madereva wengi hawakuwa na taarifa za ongezeko hilo, hali iliyowalazimu kuwasiliana na waajiri wao ili wawatumie fedha za ziada.
Hata hivyo, alisema ongezeko hilo la ushuru lililodumu kwa takribani wiki moja inakadiriwa magari zaidi ya 200 yalitozwa ushuru mpya wa Dola 500 kabla serikali ya Tanzania kufanya mazungumzo na serikali ya Rwanda na kufikia mwafaka wa kurejesha ushuru wa zamani wa Dola 152.
Alisema ingawa serikali ya Rwanda ilikubali kurejesha ushuru wa zamani, lakini baadaye iliweka bango mpakani upande wake lililosema tozo hiyo ya zamani ingedumu hadi jana na baada ya hapo malori yatatakiwa kulipa Dola 500.
“Ni kweli kulitokea ongezeko la ghafla la road toll (ushuru wa barabara) kwa upande wa wenzetu kutoka Dola 152 hadi Dola 500.
Tulipouliza kwa nini wamefanya hivyo tena ghafla, walidai wanataka kuwa na kiwango sawa na cha kwetu,” alisema.
Aliongeza kwamba kimsingi, madai hayo ya Rwanda kwamba wanataka kuwa na kiwango cha tozo sawa na cha Tanzania hayana ukweli wowote kwa sababu hapa nchini ushuru wa barabara unatozwa kulingana na umbali ambao gari linasafiri.
“Sisi hapa nchini tunatoza ushuru wa barabara kwa kuangalia kilometa, hiyo Dola 500 wanayodai tunatoza ni umbali wa kutoka hapa Rusumo hadi Dar es Salaam ambao ni zaidi ya kilometa 1,800,” alisema Mohamed.
Aliongeza kwamba kwa magari yanayoishia Isaka wilayani Kahama yanayotozwa Dola 110 tu, tofauti na Rwanda ambao wao kiwango chao ni kimoja hata kama gari litasafiri umbali wa nusu kilometa.
DC NGARA ANENA
Mkuu wa Wilaya ya Ngara, Constantine Kanyasu, alithibitisha serikali ya Rwanda kuongeza ushuru wa barabara kutoka Dola 152 hadi Dola 500 na kwamba baada ya mazungumzo na serikali ya Tanzania walikubali kurejesha kiwango cha zamani, lakini kwa muda tu.
“Baada ya kufanya nao mazungumzo kuhusu uamuzi wao wa kupandisha ushuru wa barabara, walikubali kurejesha kiwango cha zamani, lakini wakasema wanafanya hivyo kwa muda tu ili kuruhusu magari yaliyokuwa tayari yamepakia mizigo Dar es Salaam hadi Septemba 9, hivyo tunasubiri kuona hiyo kesho (leo) kama watarejesha tozo mpya au wataendelea na tozo ya zamani,” alisema.
Hata hivyo, Kanyasu alisema Tanzania ina mtandao mrefu wa barabara wa karibu kilometa 2,000 na ndiyo sababu tozo inafikia hadi Dola 500, lakini Rwanda ina mtandao wa barabara usiozidi kilometa 300, hivyo madai yao ya kupandisha ushuru wa barabara hauna maelezo ya kuridhisha.
KAULI ZA MADEREVA
Baadhi ya madereva wa malori ya mizigo waliozungumza na NIPASHE wakati wakisubiri kuvuka kuingia Rwanda walisema ingawa hawana uwezo wa kuzuia ongezeko la ushuru, lakini pia hawaoni kama lina tija hususani kwa wananchi wa Rwanda.
Kassim Salum anayeendesha lori la mizigo la kampuni ya Bhanji Logistics ya jijini Dar es Salaam, alisema ameshangazwa na ongezeko hilo kwa upande wa Rwanda kwa sababu kwa upande wa Burundi kiwango ni kile kile cha Dola 152.
“Kimsingi, hakuna tofauti kubwa ya kijiografia kati ya Rwanda na Burundi, lakini tumeshangaa kusikia kwamba Rwanda wanakusudia kupandisha ushuru kutoka Dola 152 hadi Dola 500 wakati wenzao wa Burundi kiwango ni kile kile na hakuna usumbufu wowote,” alisema.
Aliongeza kwamba kama Rwanda wataendelea na msimamo wao ni wazi watakaoathirika ni wananchi wake kwa sababu wenye magari wataongeza gharama za usafirishaji na wafanyabiashara wataongeza bei ya bidhaa, hivyo atakayeathirika ni mlaji wa mwisho ambaye ni mwananchi wa Rwanda.
John Nzigila, anayeendesha lori la Kampuni ya Mafuta ya Eafco, alisema alifika katika mpaka wa Rusumo juzi na kukuta foleni kubwa.
Alisema pengine foleni hiyo ilitokana na malori mengi kutaka kuwahi kuvuka kuingia Rwanda kabla ya jana ambayo ilikuwa siku ya mwisho ya kutozwa kiwango cha zamani cha ushuru.
“Mimi nimeingia hapa jana (juzi) na nililazimika kulipia hiyo hiyo jana (juzi) ili kuepuka kulipa tozo mpya ambayo tuliambiwa inaanza kesho,” alisema Nzigila.
Naye Zuberi Denya anayeendesha lori la mizigo la Kampuni ya Kleb ya jijini Dar es Salaam, alisema serikali ya Rwanda ina uhuru wa kuongeza ushuru kadri itakavyoona inafaa, lakini haoni kama kulikuwa na sababu yoyote ya msingi ya kufanya hivyo hivi sasa.
“Unajua katika siku za karibuni kumekuwapo na mgongano wa kisiasa kati ya Tanzania na Rwanda, hivyo hatuwezi kuhusisha moja kwa moja ongezeko la ushuru na mgongano huo, lakini tunajiuliza kwa nini wafanye hivyo sasa hivi baada ya Tanzania kuwataka wahamiaji haramu kurejea kwao?”
NIPASHE ambalo limefika eneo la Rusumo kwenye mpaka wa Tanzania na Rwanda jana lilishuhudia msururu mrefu wa malori yakisubiri kuvuka mpaka huku baadhi ya madereva wakijaribu kuvunja utaratibu na kuchepuka foleni kwa lengo la kutaka kuwahi.
KAULI YA WAZIRI MGIMWA
Waziri wa Fedha, Dk. William Mgimwa, jana aliliambia NIPASHE kuwa amesikia habari hizo, lakini alisema mazungumzo kuhusiana na suala hilo kati ya Tanzania na Rwanda yanaendelea.
Dk. Mgimwa alisema kesho atakutana na waziri mwenzake wa Fedha wa Rwanda jijini Kampala, Uganda kuzungumzia suala hilo.
Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, hakupatikana jana kuzungumzia suala hilo kwani simu zake zilikuwa zimefungwa.
Hata hivyo, Naibu wake, Dk. Charles Tizeba, alipoulizwa jana, alisema asingeweza kulizungumzia suala hilo kwa kuwa alikuwa katika ziara ya Rais Jakaya Kikwete mkoani Mwanza na kushauri aulizwe Waziri Mwakyembe.
TATOA YATANGAZA MSIMAMO
Naye Msemaji wa Chama cha Wamiliki wa Malori Tanzania (Tatoa), Elias Lukumay, alisema msimamo wao uko pale pale kwamba hawatakuwa tayari kulipa nyongeza ya ushuru.
Lukumay alisema wataendelea kusimamisha magari mpakani mpaka pale mawaziri wawili wa fedha watakapokutana na kufikia mwafaka.
Septemba 3, mwaka huu, Serikali ya Tanzania ilisema mgogoro wa ushuru mpakani kati ya wafanyabiashara wa Tanzania na Rwanda kwa sasa umemalizika.
Hayo yalisemwa na Naibu Waziri wa Uchukuzi, Dk. Charles Tzeba, na kusema kuwa wafanyabiashara wa Kitanzania walisumbuliwa baada ya kulazimika kulipa Dola 500 za Marekani ili kuingiza mizigo yao Rwanda.
Alisema baada ya kutokea tatizo hilo, alimpigia simu Waziri wa Uchukuzi wa Rwanda, Profesa Silas Lwakabamba, ambaye alisema hana taarifa juu ya taarifa hizo na kuwasiliana na Waziri wa Fedha wa Rwanda ambaye alimpa taarifa kuhusiana na suala hilo.
Hata hivyo, Tzeba alikanusha madai ya kupandishwa ushuru huo kutokana na mgogoro wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Rwanda.
Alisema walipata taarifa zisizo rasmi kuwa Rwanda ingepandisha gharama za ushuru kuanzia mwanzoni mwa mwezi huu na kwamba walikuwa wakisubiri taarifa rasmi.
Hata hivyo, alisema taarifa hizo zilikuwa na ukweli kwani Septemba Mosi, mwaka huu alipigiwa simu kutoka mpakani kuwa magari ya Tanzania yamezuiwa eneo la Rusumo na wanatakiwa walipe Dola 500.
Tzeba alisema baada ya kuwasiliana na Profesa Lwakatamba walikubaliana kuwa suala hilo litafanyiwa kazi na mawaziri wa fedha wa nchi hizo mbili.
- Nipashe.
No comments:
Post a Comment