MEMBE:MSIJE DAR WAKATI WA ZIARA YA OBAMA
Rais wa Marekani, Barack Obama
Waziri wa
Mambo ya Nje, Bernard Membe amewashauri watu walioko mikoani kusitisha
safari za kuja Dar es Salaam wakati wa ziara ya Rais wa Marekani,
Barrack Obama kutokana na wingi wa wageni katika jiji hilo. Ugeni huo
pamoja na ule wa viongozi kumi na moja kutoka nchi mbalimbali duniani
watakaohudhuria mkutano wa kimataifa wa Smart Partnership
utakaofunguliwa kesho na Rais Jakaya Kikwete kwenye Ukumbi wa Mikutano
wa Kimataifa wa Julius Nyerere, umesababisha kuimarishwa kwa ulinzi
katika maeneo mbalimbali hasa katika hoteli za kitalii ambazo
zimeanza....
utaratibu wa upekuzi kwa wageni wake.
Akizungumza na katika mahojiano na Redio ya Clouds jana, Membe alisema jiji limefurika kwa wingi wa wageni.
“Hoteli na nyumba za wageni zimefurika
wageni na magari mengi yamekodiwa. Kwa ujumla, huduma za kijamii
zitakuwa shida,” alisema.
Rais Obama na mkewe Michelle
watawasili nchini Jumatatu na tayari wapambe na maofisa usalama kutokana
Marekani wameanza kuwasili. Mbali ya ujio huo, wake wa marais kutoka
nchi 14 za Afrika watakaokutana na Laura Bush, mke wa Rais wa zamani wa
Marekani, George Bush. Pia Michelle atahudhuria mkutano huo
utakaofanyika Jumanne na Jumatano ijayo.
“Jiji la Dar es Salaam litakuwa na
mambo mengi kwa hiyo wale wenye kuja kutaka kustarehe wafute safari
zao,” alisema na kuongeza: “Kama kuna watu ambao hawapo Dar es Salaam na
hawana sababu za kuja mjini waache tu mpaka wageni watakapoondoka kwa
sababu jiji la litakuwa limejaa na baadhi ya barabara zitachukuliwa
zitumike na wageni hao.”
Alisema katika kipindi cha siku tano
zijazo, baadhi ya barabara za Jiji la Dar es Salaam zitakuwa na shughuli
nyingi na nyingine zitalazimika kufungwa. Barabara itakayofungwa ni
pamoja na ile ya Mwai Kibaki na ile ya Bagamoyo itakuwa na shughuli
nyingi pia wakati Michelle atakapokwenda Jumba la Makumbusho, Jumanne
ijayo.
Wasafiri wa mikoani
Wasafiri wa mikoani wataathirika zaidi
Jumanne ijayo wakati Rais Obama atakapokwenda kutembelea mitambo ya
kufua umeme ya Kampuni ya Symbion Ubungo.
Kituo hicho kipo Barabara ya Morogoro, ambayo ndiyo inayotumiwa na magari yanayoingia na kutoka mikoani.
Rais Obama atakwenda katika kituo
hicho yapata saa 4.00 asubuhi na kwa kiasi kikubwa itaathiri magari ya
usafirishaji wa mizigo na abiria yatakayokuwa yanatoka na kuingia Dar es
Salaam kabla na wakati huo.
Wengine watakaoathirika ni wakazi wa
Kimara, Mbezi, Kibamba hadi Kiluvya. Athari nyingine ya usafiri itakuwa
katikati ya jiji ambako Obama na msafara watakuwa na shughuli nyingi na
hasa ile ya ufunguzi wa barabara karibu na Ikulu na kukutana na
wafanyabiashara kwenye Hoteli ya Hyatt Regency, Jumatatu ijayo.
Watumiaji wengine wa barabara
watakaopata shida ni wale wa Barabara ya Bagamoyo hasa pale Rais Obama
na mkewe watakapokwenda kuweka mashada ya maua kwenye ubalozi wa zamani
wa Marekani uliopuliwa na mabomu mwaka 1998.
Ulinzi hoteli za kitalii
Mashushushu wa ndani na nje ya nchi
wamezingira kwenye hoteli kubwa za Dar es Salaam na walionekana katika
baadhi ya hoteli hizo, wakiwatumia mbwa maalumu kufanya ukaguzi wa
chumba hadi chumba.
Tofauti na utaratibu uliozoeleka,
baadhi ya hoteli zenye hadhi ya nyota tano zimeanza kutumia mitambo
maalumu ya kompyuta kuwafanyia ukaguzi wageni wote wanaoingia.
Wamchongea JK
Mtandao wa Kutetea Waandishi wa Habari
Duniani (CPJ), umemwandikia barua Rais Obama ukimtaka kujadiliana kwa
kina na mwenyeji wake Rais Kikwete wakati wa ziara yake nchini kuhusiana
na vitendo vya kuuawa na kuteswa kwa waandishi wa habari wa Tanzania.
Katika barua hiyo iliyosainiwa na
Mtendaji Mkuu wa CPJ, Joel Simon na nakala yake kusambazwa kwa viongozi
mbalimbali akiwemo Rais Kikwete mwenyewe, mtandao huo ulitolea mfano wa
kuuawa kwa Mwandishi wa Channel 10, Daudi Mwangozi na Issa Ngumba wa
Redio Kwizera. Pia kupigwa na kuteswa kwa Mhariri Mtendaji wa Habari
Corporation, Absalom Kibanda.
Marais waja Smart Partnership
Akizungumzia mkutano wa Smart
Partnership utakaoanza kesho, Membe alisema utajadili jinsi ya kutumia
sayansi na teknolojia kukuza uchumi.
Viongozi watakaohudhuria mkutano huo
ni Waziri Mkuu wa Malayasia, Najib Razak, Rais wa Uganda, Yoweri
Museveni, Uhuru Kenyetta (Kenya), Boni Yayi (Benin), Ali Omar Bongo
(Gabon), Ikililou Dhoinine (Comoro), Faure Gnassingbe (Togo), Ernest
Koroma (Sierra Leone), Blaise Compaore (Burkina Fasso), Mahinda
Rajapaska (Sri Lanka) na Mfalme wa Swaziland, Mswati II, ambaye
aliwasili jana. Chanzo: mwananchi
No comments:
Post a Comment