KLABU YA THAILAND YASAKA WACHEZAJI TANZANIA
Klabu ya
Thai Port Football ya Thailand inatafuta wachezaji nchini Tanzania kwa
ajili ya kucheza mpira wa miguu nchini humo na katika nchi nyingine
barani Ulaya.
Kupitia kwa wakala wake, klabu hiyo
imetuma taarifa kupitia Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
ikitaka wachezaji wenye umri kuanzia miaka 15 hadi 28 kwa ajili ya
kuwafanyia majaribio ambapo watakaofuzu watacheza nchini humo na katika
klabu nyingine za Ulaya ambazo wana ushirikiano nazo.
Wachezaji wenye nia ya kufanya
majaribio wanatakiwa kutuma taarifa za wasifu wao (CV) kwa klabu hiyo
kwa njia ya emaili, wawe na pasi ya kusafiria pamoja na pasi ya mchezaji
(player passport).
Wakala atapitia vitu hivyo, na kwa wachezaji atakaowahitaji atawatumia tiketi za ndege na viza kwa ajili ya kwenda kufanya majaribio nchini humo, na watakaofanikiwa kabla ya kusaini nao mikataba watawasiliana na klabu zao nchini (kwa wale wenye klabu).
MTANZANIA APEWA ITC ACHEZE YEMEN
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limetoa Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) kwa mchezaji Mtanzania Gossage Mtumwa ili aweze kucheza mpira nchini Yemen.
Mtumwa ambaye anatoka katika kituo cha kukuza na kuendeleza vipaji cha Rollingstone cha Arusha aliombewa hati hiyo na Chama cha Mpira wa Miguu cha Yemen (YFA) kwa ajili ya kucheza nchini humo.
TFF inamtakia kila la kheri Mtumwa katika safari yake ya Yemen, na ni matarajio yetu kuwa atakuwa balozi mzuri wa Tanzania nchini humo ili wachezaji wengine wa Tanzania nao wapate fursa ya kucheza mpira wa miguu nchini Yemen. Boniface Wambura
No comments:
Post a Comment