ICC INAHARIBU MAHUSIANO YAKE NA AFRIKA - RAIS KIKWETE 
            
Rais wa 
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete 
amesema kuwa mwenendo wa Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC) 
kuhusu Bara la Afrika na viongozi wake, unainyima Mahakama hiyo nafasi 
kubwa ya kuungwa mkono na Bara la Afrika.
Rais Kikwete pia amelaani vikali 
mashambulizi yanayoongezeka dhidi ya vikosi vya kimataifa vya kulinda 
amani katika nchi mbali mbali duniani wakiwamo walinda amani wa 
Tanzania.(P.T)
 
                        
        
        
        
            
Rais Kikwete alitoa msimamo huo wa Tanzania mwishoni mwa wiki wakati alipohutubia Kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa
Mataifa (UNGA) mwaka huu, kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, Marekani.
Katika hotuba yake fupi na 
iliyowavutia wasikilizaji, Rais Kikwete alisema kuwa ni dhahiri 
kuanzishwa kwa ICC kutokana na Mkataba wa Rome kulikuwa ni hatua muhimu 
sana katika mfumo wa kimataifa wa kupambana na makosa ya jinai.
"Kwa hakika kuundwa kwa Mahakama hiyo 
kuliweka mfumo mzuri wa kuondokana na watu kutenda vitendo vya jinai na 
kuweza kuepukana na kuwajibika kwa vitendo hivyo na Mahakama hiyo 
ilianzishwa kwa kuungwa mkono kwa kiasi kikubwa na Afrika.
"Hata hivyo, muongo mmoja tu baada ya 
kuanzishwa kwa Mahakama hiyo, ni dhahiri kuwa mvutano umezuka kati ya 
ICC na Bara la Afrika. Sasa Mahakama hiyo inaonekana kama taasisi 
isiyojali maoni na msimamo wa Afrika, kwa mambo ambayo kwa maoni yangu, 
ni hofu halali ya Waafrika," amesema Rais Kikwete na kuongeza:
"Bado Mahakama hiyo inaendelea kupuuza
 maombi ya mara kwa mara ya Umoja wa Afrika. Ni jambo la kutia huzuni 
kuwa maombi ya kubadilisha muda wa kuanza kusikilizwa kwa kesi dhidi ya 
Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya na Naibu Rais William Ruto yalipuuzwa na 
hata hayakujibiwa kabisa."
Ameongeza Rais: "Tabia hii imekuwa ni 
hitilafu kubwa ambayo inaleta kikwazo kwa ICC kushindwa kutimiza wajibu 
wake wa kupambana na tabia ya watu wanaofanya makosa ya jinai 
kutokuchukuliwa hatua. Kwa hakika, kugangamara kwa ICC hata katika 
masuala yaliyo wazi, kumethibitika kuwa kunainyima Mahakama hiyo nafasi 
ya kuendelea kuungwa mkono Barani Afrika."
Rais Kikwete alisema pia kuwa Tanzania
 sasa imekuwa moja ya nchi ambazo zinashiriki zaidi katika shughuli za 
kimataifa za kulinda amani chini ya Umoja wa Mataifa. Tanzania ina zaidi
 ya walinda amani 2,500 katika Darfur, Sudan; Lebanon na Jamhuri ya 
Kidemokrasi ya Congo (DRC) na kuwa ni nchi ya sita katika Afrika na ya 
12 duniani kwa kutoa walinzi wa amani duniani.
"Kwa hakika tunaridhishwa na mchango 
wetu mdogo katika shughuli hii. Na tunajua kuwa wakati mwingine tunalipa
 gharama kubwa na maisha ya vijana wetu kwenye shughuli hizi kama 
ilivyotokea majuzi katika Darfur na DRC. Waliopoteza maisha yao ni 
mashujaa wa taifa letu ambao maisha yao hayakupotea bure."
Aliongeza Rais Kikwete: "Vifo vya 
walinda amani wetu ni ukumbusho wa kutosha wa hatari zinazowakabili 
walinda amani wote duniani. Ni jambo la kuudhi, kwamba vikundi vyenye 
silaha na waharibifu wa amani duniani wanaongeza mashambulizi hayo dhidi
 ya watumishi wa amani. Ni lazima tulaani mashambulizi haya kwa nguvu 
zetu zote kwa sababu hakuna sababu yoyote ya kuhalalisha mashambulizi 
haya ya kinyama ambayo ni kosa la kimataifa la jinai chini ya Sheria za 
Kimataifa."
Alisisitiza: "Baraza la Usalama la 
Umoja wa Mataifa ambalo wajibu wake mkuu ni kulinda amani na usalama wa 
kimataifa lazima liwe mstari wa mbele katika kulaani vitendo hivyo vya 
kinyama na haraka tu vinapotokea."
Rais Kikwete ambaye alikuwa katika 
ziara ya kikazi katika Marekani na Canada ameondoka New York usiku wa 
leo, Jumamosi, Septemba 28, 2013, kurejea nyumbani ambako atawasili 
Jumatatu mchana.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.