MFUMO MPYA WA USAJILI WA VIZAZI WA WATOTO
Meneja
Masoko na Mawasiliano kutoka Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini
(RITA) Josephat Kimaro KUSHOTO akieleza kwa waandishi wa habari juu ya
mafanikio ya utekelezaji wa mfumo mpya wa usajili wa vizazi kupitia
mkakati wa usajili wa watoto walio na umri chini ya miaka mitano, katika
mkutano na waandishi wa habari uliofanyika leo Jijini Dar es salaam
kulia ni Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Habari Zamaradi Kawawa.
Mfumo
mpya wa Usajili ulizinduliwa Tarehe 23 Julai 2013 mkoani Mbeya na Naibu
Waziri wa Katiba na Sheria Mh. Angellah Kairuki. Lengo kuu la mabadiliko
ya mfumo wa Usajili ni kuondoa changamoto zilizokuwa zinasababisha
wananchi wengi kotosajiliwa na kupata vyeti vya Kuzaliwa Nchini. Kwa
mujibu wa Takwimu ni asilimia 23 tu ya Watanzania wamesajiliwa na kupata
vyeti vya kuzaliwa. Changamoto ambazo zimekuwa zikisababisha wananchi
wengi kutosajiliwa ni....M.M
pamoja
na umbali mrefu kutoka maeneo wanayoishi mpaka katika Ofisi za Wasajili
wa Wilaya, ada ya cheti, taratibu za usajili zisizo rafiki, elimu ndogo
ya wananchi kuhusu umuhimu wa cheti cha kuzaliwa, na nyinginezo.
Kwa
Kuanzia, utekelezaji wa mfumo mpya wa Usajili wa Vizazi umeanza kwa
Kundi la Watoto walio na Umri chini ya Miaka Mitano( Underfive Birth
Registration Initiative – U5BRI) katika Mkoa wa Mbeya.
Katika
Mfumo mpya maboresho yaliyofanyika ni pamoja na kushusha huduma za
Usajili na kutoa vyeti katika ngazi ya kata ambapo utafanyika katika
Ofisi za Watendaji kata na katika vituo vya Tiba vinavyotoa huduma ya
Afya ya Mama na Mtoto. Pia katika mfumo mpya Serekali imeondoa ada ya
Cheti kwa Watoto wa chini ya Miaka Mitano. Vilevile taratibu za usajili
zimeboreshwa kwani mzazi wa mtoto akifika katika vituo vya usajili
ataweza kumsajili na kupata cheti cha kuzaliwa hapohapo tofauti na awali
ambapo usajili ulifanyika hospitali mtoto anapozaliwa na baadae mzazi
kutakiwa kwenda katika ofisi za RITA ili kupata cheti cha Mtoto. Pia
watendaji kata wanatumika katika kutoa elimu ya umuhimu wa usajili na
kuwa na Vyeti vya kuzaliwa
Pia
kumekuwa na changamoto ya kupatikana taarifa za waliosajiliwa kwani
katika mfumo wa awali wasajili wa wilaya wamekuwa hawaziwakilishi kwa
wakati hivyo Serikali kukosa taarifa za Vizazi kwa ajili ya matumizi ya
Mipango ya Maendeleo. Katika utekelezaji unaoendelea Mkoani Mbeya
utumaji taarifa kutumia teknolojia unaenda kufanyika kwa kutumia simu za
Kiganjani.
Katika
utekelezaji unaoendelea mkoani Mbeya, mwamko wa Wananchi umekuwa mkubwa
sana kwa zaidi ya watoto 61,000 walio na umri wa chini ya Miaka Mitano
wameweza kusajiliwa na kupatiwa vyeti kwa muda wa siku 14 za awali za
utekelezaji na kati ya hao asilimia 49 wakiwa wanawake na wanaume
asilimia 51. Wilaya zinazoongoza kwa usajili ni Mbozi, Rungwe na Mbarali
na Wilaya ya Momba ni ya Mwisho mpaka sasa kwa Mujibu wa Takwimu. Pia
watoto wengi zaidi wamesajiliwa katika Ofisi za Watendaji Kata kuliko
katika Vituo vya Tiba. Lengo la RITA ni kusajili watoto 230,000 Mkoani
Mbeya kufikia mwezi Juni 2014.
Zoezi la Usajili na kutoa vyeti katika Ofisi za Kata na Vituo vya Tiba kwa watoto wa Umri chini ya Miaka Mitano ni la Kudumu.
Awamu ya
kwanza ya utekelezaji wa Mkakati huu inajumuisha Mikoa ya Mbeya, Mwanza,
Shinyanga, Simiyu na Geita ambayo inategemea kukamiliaka Julai 2015.
Josephat Kimaro
Meneja Masoko na Mawasiliano – RITA
12 AGOSTI 2013
No comments:
Post a Comment