TIFFAN ENT

TIFFAN ENT

TUKO WANGAPI

TUKO WANGAPI

GLORY FREIGHT

GLORY FREIGHT

Thursday, August 29, 2013

KAGAME ATUA RASMI KENYA 

marais1 27613
MKAKATI wa kiuchumi na kimiundombinu unaozihusisha nchi za Kenya, Uganda na Rwanda ambao pamoja na mambo mengine unaitenga Tanzania, ulizinduliwa rasmi mjini Mombasa juzi na marais watatu wa mataifa hayo ya Afrika Mashariki. (HM)
Katikati ya mkakati huo wa mataifa hayo matatu yuko Rais wa Rwanda, Paul Kagame ambaye jana aliwasili Mombasa na kushiriki katika mkakati wa kuzinduliwa kwa gati namba 19 katika bandari ya Mombasa ambayo inakusudiwa kutumiwa na nchi hizo kupakulia na kusafirishia mizigo yake.
Mbali ya Rais Kagame, uzinduzi wa gati hilo uliwakutanisha pia Rais wa Uganda,Yoweri Museveni , Salva Kiir wa Sudani Kusini na mwenyeji wao Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta.
Tukio la Kagame kuwapo katika tukio hilo la kihistoria kiuchumi katika ukanda huu linakuja siku chache, baada ya kuwapo kwa taarifa kwamba wafanyabiashara wa Rwanda walikuwa wameamua kuacha kuitumia bandari ya Dar es Salaam katika kupakua na kusafirishia mizigo yao.
Akizungumza katika hafla hiyo, Rais Kenyatta alisema uamuzi wa Kenya kuipanua bandari hiyo ni jambo lisiloweza kuepukwa iwapo mataifa hayo ya mashariki mwa Afrika yana kusudi la kweli la kujiendeleza kiuchumi.
"Tunalenga ufanisi na kupunguza vikwazo vya biashara na kuboresha fursa za nchi zetu. Bandari hii, ni muhimu kwa maendeleo ya eneo letu na uzinduzi wa gati namba 19, unawakilisha dhamira ya serikali ninayoiongoza.
"Dhamira ya serikali yangu ni kuona bandari ya Mombasa inakuwa kubwa zaidi, yenye shughuli nyingi na mazingira rafiki zaidi ya kibiashara katika pwani ya Afrika Mashariki," alisema Kenyatta.
Akizungumza baada ya tukio hilo, Rais Kagame alisema ni hatua muhimu ya maendeleo na katika kuimarisha uwekezaji.
"Kuzinduliwa kwa bandari hii, kutaongeza biashara na kuvutia wawekezaji katika ukanda wa Afrika Mashariki," alisema Rais Kagame.
Eneo hilo jipya la maegesho lenye urefu wa mita 240 linatarajia kuboresha shughuli za upakiaji na upakuaji makontena na uwezo wa bandari hiyo.
Rais Museveni ambaye ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, alisema bandari hiyo itakuwa kichocheo cha kutoa bidhaa na huduma ndani ya nchi hizo na katika masoko ya kimataifa.
Alisema nchi wanachama wa jumuiya hiyo, zinapaswa kuwa na umoja na kuanzisha masoko yenye bidhaa bora na huduma kwa watumiaji.
"Tunategemea bandari hii itakuwa mkombozi katika masoko yetu na kukabiliana na ushindi mkubwa wa biashara duniani," alisema Rais Museveni.
Kutokana na hali hiyo, Museveni alimwagia sifa Rais Kenyatta kwa uamuzi wa kuondoa vikwazo ambavyo vimekuwa chanzo kikubwa cha kuenea kwa rushwa.
"Hatua hii, ni nzuri beria nyingi zimegeuka kuwa za wala rushwa, naamini sasa bidhaa, huduma na wananchi wa Kenya na Uganda wataufurahia," alisema Museveni.
Ujenzi wa gati namba 19 lililozinduliwa jana na marais hao unakadiriwa kugharimu dola za Marekani milioni 66.7 na utaongeza uwezo wa huduma zake kwa asilimia 33 zaidi ya sasa.
MZOZO BUNGE LA AFRIKA MASHARIKI
Wakati viongozi hao wakizindua gati hilo, jijini Arusha, kwa siku ya pili mfululizo kuliibuka mzozo miongoni mwa wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki.
Mzozo huo ambao unaonekana kuchochewa zaidi na uhasama wa kidiplomasia baina ya Tanzania na Rwanda, jana uliendelea baada ya wabunge wa Tanzania katika bunge hilo kutoka nje ya ukumbi wa bunge.
Wabunge wa Tanzania, walifikia uamuzi huo kwa kile walichodai kupinga kitendo cha wabunge wenzao wa Rwanda wanaoungwa mkono na wale wa kutoka Kenya na Uganda kutaka hoja yao ya vikao vya bunge vifanyike kwa mzunguko katika nchi zote wanachama, ijadiliwe bila kufuata kanuni za bunge.
Katika kikao cha juzi, Mbunge wa Rwanda, James Ndahiro, aliomba mwongozo kwa Spika akitaka hoja ya vikao vya Bunge hilo kufanyika kwa mzunguko ijadiliwe katika kikao hicho.
Mbunge Ndahiro, aliomba mwongozo huo baada ya Mbunge wa Kenya, Peter Mathuki kutoa hoja ya kutaka suala la vikao hivyo kufanyika kila nchi wanachama, lijadiliwe lakini Spika wa Bunge, Margaret Zziwa,
alitoa utaratibu kuwa limekuwa jambo la haraka na muda uliobaki ni mchache hivyo anaweza kulileta jambo hilo kama motion kwa muda mwingine.
Kauli hiyo ya Spika iliwaudhi wabunge wa Rwanda ambao walisimama na kutoka nje ya ukumbi wa Bunge huku wakieleza kuwa hawataki kuburuzwa na walifuatiwa na wa Kenya.
Katika kikao cha jana, wabunge wa Tanzania wakiongozwa na Abdula Mwinyi nao walisusia kikao kwa kutoka nje ya ukumbi wa Bunge.
Kabla ya kufikiwa kwa hatua hiyo, Mwinyi alisimama na kulieleza Bunge hilo kuwa kitendo kilichofanywa na wabunge wa Rwanda juzi hakikuwa cha kistaarabu na si utamaduni mzuri, bali ni dharau kubwa kwa kiti cha spika na Bunge zima la Afrika Mashariki kwa sababu hoja iliyowasilishwa haikufuata utaratibu wa kibunge.
"Mheshimiwa Spika, nimesikitishwa na kilichotokea jana (juzi) hapa, haikuwa utamaduni mzuri tuliouzoea ni udhalilishaji wa kiti na kimechafua hata sifa ya Bunge lako, tunatakiwa kuweka utaratibu sawa ili kiti kiheshimiwe," alisema Mwinyi.
Baada ya kumaliza kuzungumza, wabunge wa Tanzania walitoka nje ya ukumbi wa Bunge, ambapo kwa mujibu wa utaratibu vikao haviwezi kuendelea kama wabunge kutoka nchi mwanachama wakitoka nje kama ishara ya kutokukubaliana na hoja inayojadiliwa.
Wakizungumza nje ya ukumbi, baadhi ya wabunge hao walisema utaratibu wa kidemokrasia kote duniani ni kwamba anayeshambuliwa kidemokrasia anapaswa kujibu mapigo.
"Katika demokrasia mtu 'akikuhit', wewe unapaswa 'kumhit' zaidi ya kile alichokufanyia, sasa sisi tumeamua kujibu zaidi yao kama ishara ya kupinga kitendo chao cha jana," alisema Shy rose Bhanji.
Kwa upande wake, Mwinyi alikiita kitendo kilichofanywa na wenzao kuwa ni uhuni na ukosefu wa ustaarabu, kwani kabla ya kuwasilisha hoja hiyo hakukuwa na kusudio la kuwasilishwa kwa hoja hiyo mezani kwa spika.
"Tunataka kuweka rekodi sawa, huu sio utaratibu ni uhuni na hatutaki urudiwe popote katika jumuiya...kwanza hawakutoa 'notice' mezani kwa spika kama utaratibu unavyotaka wanaamua tu na kushinikiza mambo wanavyotaka haikubaliki.
"Kutoka kwetu nje ni kupinga uhuni huu, wao hawakuwa na sababu yoyote ya kutoka na kama walitaka kuwepo na mzunguko katika vikao vya bunge wangefuata utaratibu," alisema Mwinyi.
Wabunge wengine wa Tanzania waliokuwepo katika kikao hicho cha jana ni pamoja na Twaha Taslima, Makongoro Nyerere na Nderikio Kessy. Chanzo: mtanzania

No comments:

Post a Comment