VIONGOZI WOTE KUKAGULIWA VIWANJA VYA NDEGE...!
KUANZIA sasa viongozi wote serikalini
watakaopita kwenye viwanja vya ndege nchini, watakuwa wakikaguliwa kama
abiria wengine, isipokuwa Rais, Makamu wake, Waziri Mkuu, Jaji Mkuu na
Spika wa Bunge.
Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison
Mwakyembe amesema ipo tabia ya viongozi wenye madaraka, kukiuka
utaratibu na kupita katika viwanja vya ndege bila kukaguliwa.
Alisema kutokana na hali hiyo,
amewaambia watumishi wanaofanya kazi katika viwanja hivyo, hususan
Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Julius Nyerere (JNIA) viongozi
wasiokaguliwa ni Rais, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Jaji Mkuu na Spika
wa Bunge.
Alitoa msimamo huo wiki iliyopita
kupitia kipindi cha Jenerali on Monday, kinachorushwa na Televisheni ya
Channel Ten. Alisema viongozi wengine wote, wakiwamo mabalozi na
mawaziri lazima wakaguliwe.
Dk Mwakyembe alisema aliwaambia viongozi wasiopenda kukaguliwa, wasipande ndege. Alisema pamoja na
baadhi kuona ni usumbufu, inawezekana
wakajikuta wamesahau vitu hatari, kama vile risasi na wakaenda
kugundulika nje ya nchi ikawa tatizo.
Alitoa mfano kwamba aliwahi kupigiwa simu na mmoja wa mabalozi, akilalamika kwamba vijana wake wamemkagua uwanja wa ndege.
Alisema alimjibu kwamba wanatimiza
wajibu wao. Katika mahojiano yaliyojikita juu ya tatizo la dawa za
kulevya nchini, Dk Mwakyembe alisisitiza kwamba hatua alizoanza kuchukua
kudhibiti upitishaji dawa hizo kwenye viwanja vya ndege, siyo moto wa
kifuu wala nguvu ya soda.
"Ninachokifanya hapa ni kile ambacho
kinapaswa kufanywa... na hili la dawa za kulevya katika viwanja vya
ndege, nitalikomesha," alisema. Alisisitiza kwamba udhibiti huo ni kwa
viwanja vyote vya ndege nchini. Dk Mwakyembe alisema, "kwa sasa mizigo
yote inayoingia katika eneo hilo, lazima ikaguliwe, kwani huo sio mzaha,
sio moto wa kifuu wala nguvu ya soda."
Kwa mujibu wa Waziri, mizigo
inayoingia imekuwa haikaguliwi. Alisema katika kutekeleza ukaguzi huo wa
mizigo inayoingia, imenunuliwa mitambo kwa ajili hiyo.
Kuhusu wanaomeza dawa za kulevya,
alisema wamekuwa wakigundulika kutokana na ufuatiliaji kuanzia kwenye
ndege. Alitoa mfano kwamba kwa sasa endapo abiria atapanda ndege katika
uwanja wa ndege wa Dar es Salaam, mathalani kwenda Dubai, akipewa chai
au pombe, akakataa kunywa, kwa vyovyote huyo lazima akaguliwe zaidi.
Katika hilo, aliwaasa vijana wa
Tanzania kujiepusha na hali hiyo, kwani pindi akishuka kwenye uwanja
wowote, namba yake ya kiti itashikiliwa na atakaguliwa ipasavyo, kubaini
kama amemeza dawa.
Hatua ya Mwakyembe kuamua kuvalia
njuga dawa za kulevya, inatokana na kile ambacho kinaelezwa kuwa ni
kuchafuka kwa Tanzania, kutokana na baadhi ya watanzania kukamatwa nje
ya nchi, wakisafirisha dawa hizo, wakiwa wamezipitisha uwanja wa ndege.
Dk Mwakyembe alieleza kuwa hatua yake
ya kuvalia njuga suala hilo, inaungwa mkono na serikali kwa ujumla. Hivi
karibuni waziri huyo alifanya ziara ya ghafla katika uwanja wa ndege wa
Mwalimu Nyerere na kubaini kuwa tatizo si vifaa vya ukaguzi, bali ni
baadhi ya wafanyakazi wasio waadilifu.
Msemaji Mkuu wa Serikali ambaye ni
Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO), Assah Mwambene alisema hivi
karibuni serikali imeanzisha mkakati wa kutokomeza wimbi la dawa za
kulevya kwa kudhibiti viwanja vya ndege na sehemu mbalimbali za
mipakani, zinazotumiwa kupitisha.
Chanzo:HabariLeo
No comments:
Post a Comment