TIFFAN ENT

TIFFAN ENT

TUKO WANGAPI

TUKO WANGAPI

GLORY FREIGHT

GLORY FREIGHT

Wednesday, August 14, 2013

HAYA NDO MASHITAKA ALIYOSOMEWA SHEIKH PONDA AKIWA HOSPITALINI


KATIBU wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda (54), amesomewa shtaka akiwa kitandani katika Kitengo cha Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Upasuaji wa Mishipa ya Fahamu (MOI).

Katika shtaka hilo, Ponda anadaiwa kuwahamasisha wafuasi wake kufanya kosa.
 
Mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Kisutu, Hellen Riwa, Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Tumaini Kweka, alidai kuwa uhamasishaji huo ulifanyika sehemu mbalimbali nchini kuanzia Juni 2 hadi Agosti 11 mwaka huu.
 
Kweka alidai kuwa kosa hilo ni kinyume cha sheria ya makosa ya jinai kifungu 390 na 35 ya kanuni za adhabu.
 
Kutokana na shtaka hilo, Hakimu Riwa aliahirisha kesi hadi Agosti 28 na kutoa agizo Sheikh Ponda aendelee kuwa chini ya uangalizi wa vyombo vya dola wakati akiendelea na matibabu.
 
Baada ya Hakimu Riwa kuahirisha kesi, wakili wa mshtakiwa Nasoro Jumaa, alilaumu utaratibu uliotumika na kusema kuwa mahakama imefanya kazi nje ya muda wa kawaida wa saa za kazi za kiserikali.
 
Alisema mawasiliano ya awali ilikuwa askari na Tume ya Haki Jinai ya Jeshi la Polisi kufika hospitalini hapo kwa ajili ya kufanya mahojiano na Sheikh Ponda.
 
Aliongeza kuwa baada ya maofisa hao kufika hali ya Sheikh Ponda haikuruhusu mahojiano kufanyika na ilipofika saa kumi jioni kila mmoja alitawanyika.

Jumaa alisema kuwa wakiwa wanakaribia geti la kutokea Muhimbili, walipigiwa simu kuwa Sheikh Ponda anasomewa mashtaka, hatua aliyodai kuwa iliwashangaza.
 
“Kama walikuwa na dhamira ya kumsomea mashtaka wangetuambia, kwa kuwa ni haki ya msingi kwa mtuhumiwa kuwa na mwanasheria wake kwa ajili ya kujua taratibu zilizotumika,” alisema.
 
Alisisitiza kuwa baada ya kupata hati ya mashtaka wanajiandaa kupinga kosa hilo kwa kile alichoeleza kuwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu haina uwezo wa kusikiliza kosa la aina hiyo.
 
Aliongeza kuwa kabla ya kufikiwa kwa hatua ya kumsomea shtaka Sheikh Ponda, walishaandika barua ya kutokuwa na imani na Tume ya Haki Jinai ya Jeshi la Polisi katika uchunguzi wao kwa kile alichoeleza kuwa ni watuhumiwa wa kwanza katika tukio la kujeruhiwa kwa mteja wake.

Awali kabla ya kesi hiyo kusomwa maeneo mbalimbali ya Hospitali ya Muhimbili hususan jirani na jengo alilolazwa Sheikh Ponda, yalikuwa yamezingirwa na makachero wa polisi wakiwa na magari matano ya Kikosi cha Kutuliza Ghasia.

Magari mawili yenye namba PT 2072 na PT 2061 yalikuwa jirani na mlango wa kuingilia katika kitengo cha mifupa huku askari wakiwazuia wananchi wasiende kumuona Ponda kwa kile walichoeleza kuwa kuna shughuli za kiserikali zinaendelea.
 
Miongoni mwa watu waliozuiwa ni wakili maarufu nchini, Profesa Abdallah Safari.

-Tanzania daima

No comments:

Post a Comment