YANGA NA AZAM ZAINGIZA MILIONI 208;
MECHI
ya Ngao ya Jamii kuashiria ufunguzi wa msimu mpya wa 2013/2014
iliyochezwa jana (Agosti 17 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam
imeingiza sh. 208,107,000. Washabiki 26,084 walikata tiketi kushuhudia
mechi hiyo ambayo ilimalizika kwa Yanga kushinda Azam bao 1-0.
P.T
Mgawanyo wa mapato ya mechi hiyo uliokuwa kama ifuatavyo; asilimia 18 ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) sh. 31,745,135.59, asilimia 10 ya mchango wa kusaidia jamii sh. 20,810,700, gharama ya tiketi sh. 7,309,866. Uwanja sh. 22,236,194.76, gharama za mchezo sh.13,341,716.86, Chama cha pira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 5,188,445.44, TFF sh. 13,341,716.86 na Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 6,670,858.43. Kila klabu imepata mgawo wa sh. 43,731,183.03.
Katika mchezo huo, bao pekee la kiungo Salum Abdul Telela ndilo lililoipa Yanga SC ushindi huo.
Mechi hiyo iliyochezeshwa na refa Oden Mbaga, aliyesaidiwa na Hamisi Chang'walu na Omar Kambangwa wote wa Dar es Salaam, hadi mapumziko Yanga SC walikuwa mbele kwa bao 1-0.
Yanga ilipata bao hilo mapema tu dakika ya pili, mfungaji kiungo Salum Abdula Telela aliyeunganisha pasi ya Didier Kavumbangu.
Baada ya bao hilo, Yanga iliongeza kasi ya mashambulizi langoni mwa Azam na kipa Aishi Manula alifanya kazi ya ziada kuokoa.
Dakika ya 11, Yanga ilipata pigo baada ya beki wake Kevin Yondan kuumia kufuatia kugongana na mshambuliaji wa Azam FC, John Bocco 'Aedebayor'. Yondan alitibiwa kwa dakika nne, lakini akashindwa kurejea uwanjani na nafasi yake ikachukuliwa na Mbuyu Twite dakika ya 15.
Dakika tano baadaye Yanga ikapata pigo lingine baada ya kipa wake, Ally Mustafa 'Barthez' kuumia kufuatia kugongana na Kipre Tchetche.
Barthez 'alijitoa muhanga' kuutokea mpira miguuni mwa mshambuliaji huyo wa Ivory Coast baada ya kuwatoka mabeki wake, Juma Abdul na Nadir Haroub 'Cannavaro'- hivyo kugongwa kifuani na mguu wa Kipre.
Barthez alitibiwa kwa dakika nne kabla ya kumpisha Deo Munishi 'Dida'. Azam waliongeza kasi ya mashambulizi langoni mwa Yanga na dakika ya 30 Kipre Tchetche alifumua shuti kali likagonga mwamba na kutoka nje akiwa ndani ya 18 baada ya kupokea pasi ya Bocco.
Aishi Manula alikuwa majaribuni tena dakika ya 30 baada ya krosi maridadi ya Simon Msuva kumponyoka kabla ya kuondoshwa hatarini na Erasto Nyoni.
Dakika ya 38 Dida alidaka shuti kali la mfungaji bora wa Ligi Kuu msimu uliopita Kipre Tchetche kutoka umbali wa mita 17 na kupigiwa makofi na mashabiki.
Kipindi cha pili, Yanga SC waliendelea kucheza vizuri na kukosa mabao zaidi, huku sifa zaidi akistahili kipa chipukizi Aishi Manula.
Dakika ya 67 Telela alikarbia kufunga tena baada ya kuunganishia nje krosi nzuri ya Haruna Niyonzima.
Dakika ya 81 Niyonzima alikaribia kufunga mwenyewe kwa mpira wa adhabu, lakini shuti lake liligonga mwamba wa juu na kudondokea chini kabla ya beki Aggrey Morris kuondosha katika hatari.
No comments:
Post a Comment