"KESI DHIDI YA WAZIRI MKUU HAINA MANTIKI....SIJAONA SEHEMU ALIYOVUNJA SHERIA"...DPP
MKURUGENZI wa Mashitaka (DPP), Eliezer Feleshi, amesema haoni mantiki yoyote au uhalali wa Kituo cha Haki za Binadamu (LHRC), kumshitaki Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
Alisema hayo janai wakati akijibu
maswali ya waandishi wa habari, baada ya kufungwa kwa mkutano wa siku
tatu wa mawakili wa Serikali wafawidhi, wakuu wa upelelezi wa mikoa na
vikosi vingine vya Polisi Alisema kauli aliyotoa Pinda bungeni,
alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Kilwa Kaskazini, Murtaza Mangungu
kuhusu Polisi kutumia nguvu kwa wananchi, ililenga wanaokaidi kukamatwa
na kufikishwa mbele ya sheria na si kupiga na kuua kama ilivyotafsiriwa
na wengi.
“Sijapata taarifa kwa maandishi juu ya
azma ya kumshitaki Waziri Mkuu, lakini Pinda hajavunja sheria kwa kauli
yake aliyotoa,” alisema.
Alisema kwa jinsi alivyosikia maelezo ya
Waziri Mkuu bungeni, kama LHRC wanamshitaki kwa jinai Waziri Mkuu,
haoni uhalali wa mashitaka hayo.
Usahihi wa Pinda Alisema Waziri Mkuu
alieleza hatua zinazochukuliwa dhidi ya mvunja sheria, na kufafanua kuwa
Mtanzania yeyote ana haki kwa mujibu wa sheria, lakini pia ana wajibu,
ndiyo maana vipo vyombo na kila chombo kimepewa mamlaka na wajibu wa
kutekeleza.
Alifafanua, kwamba kilichoongelewa ni
dhana ya mkusanyiko ambayo ni haki kwa mujibu wa Katiba, ikiwemo uhuru
wa kukutana, kutoa mawazo na kufanya mawasiliano.
Hata hivyo, alikumbusha kuwa Sheria ya
Jeshi la Polisi, inasema ili mkusanyiko ufanyike, lazima taarifa itolewe
kwa kiongozi wa Polisi wa eneo husika.
Sheria hiyo inasema, kama mkusanyiko una
nia ya kutenda kosa na ikafanyika hivyo, kuna chombo kilichopewa
dhamana ya kuhakikisha mkusanyiko haramu unatawanyika na sheria hiyo
inaruhusu Polisi kutawanya mkusanyiko haramu.
“Unatarajia nini kama kuna watu
wanafanya fujo na polisi wana mamlaka ya kuwakamata waliofanya fujo?”
Alihoji Feleshi na kuongeza kuwa dhana ya matumizi ya nguvu ni ya
kisheria pia.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji
Frederick Werema, akizungumza kwa simu na gazeti hili, alisema utaratibu
wa Polisi kulazimika kutumia nguvu upo. Aliutaja utaratibu huo kwamba
unatumika hasa katika mikusanyiko isiyotakiwa, ambapo Polisi hulazimika
kutoa tangazo la angalizo mara kadhaa kutaka watu watawanyike.
“Tangazo linapotolewa, Polisi kwa
kutumia kipaza sauti husema, tawanyikeni, tawanyikeni na kusisitiza
hivyo mara kadhaa, hapo wanaopaswa kutawanyika wakikaidi, nguvu hutumika
ingawa inaweza isiwe ya kupiga risasi, pengine virungu, yote hiyo si
kupiga?
“Risasi ni kitu cha mwisho, labda uwe
unashambuliwa wewe (polisi), hata ikiwa hivyo, ukipiga risasi kuna
maeneo ya kupiga, si kichwani, polisi wana mafunzo ya kupiga maeneo ya
miguuni, hivyo kutumia nguvu kwa polisi kupo,” alisema Jaji Werema.
No comments:
Post a Comment