Zaidi ya 6,000 wagoma UDSM
Makamu Mkuu wa UDSM, Profesa Rwekaza Mukandala (katikati) akizungumzia moja ya migomo ya wanafunzi wa chuo hicho.
ZAIDI ya
wanafunzi 6,000 wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) sehemu ya
Mlimani, wanaodai fedha za kujikimu kutoka Bodi ya Mikopo ya Elimu ya
Juu Nchini (HESLB), jana waligoma kuingia darasani wakishinikiza kulipwa
fedha zao.
Kwa
ujumla, wanafunzi hao wanaosomea fani mbalimbali, wanadai zaidi ya Sh
bilioni 2.8. Makamu Mkuu wa chuo hicho kikongwe zaidi nchini na maarufu
barani Afrika, Profesa Rwekaza Mukandala alikiri kuwepo kwa mgomo huo.
Alithibitisha kuwa wanafunzi wawili walijeruhiwa na kulazwa katika zahanati ya chuo hicho, kutokana na vurugu za hapa na pale.
Alisema
kutokana na vurugu hizo, kumetokea uharibifu katika hosteli za chuo
hicho, ikiwemo ya Mabibo kutokana na wanafunzi hao kugoma kuhudhuria
masomo, badala yake wakaanza kufanya uharibifu.
Aliongeza
kuwa wanafunzi wanaokaa katika hosteli ya Mabibo, walifanya uharibifu
asubuhi na uongozi umefanya ufuatiliaji na kubaini kuwa baadhi yao
hawakuingia darasani, na badala yake kujikusanya katika vikundi na
wengine wakijikusanya katika bwalo la chakula chuoni hapo.
"Wanafunzi
walikuwa wanategemea malipo kuanzia wiki iliyopita. Ilipoanza jana
(juzi) wakaleta malalamiko yao tukafanya jitihada nyingi, tukaamua chuo
kitawasaidia fedha kidogo mpaka watakapopata," alisema.
Aliongeza
kuwa kufikia jana Hazina (Wizara ya Fedha) waliuhakikishia uongozi wa
chuo hicho fedha hizo zingelipwa kufikia jana jioni.
Katika
maeneo ya chuo, askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) kutoka Jeshi
la Polisi walifurika kwa lengo la kuchukua tahadhari za kiusalama chuoni
hapo.
Waziri wa
Mikopo katika Serikali ya Wanafunzi chuoni hapo, Shitindi Venance
alisema fedha za kujikimu wamekuwa wakipatiwa kila baada ya wiki nane,
sawa na miezi miwili, lakini hadi sasa wamevumilia na kuchoka.
Kila
mwanafunzi anastahili kulipwa Sh 450,000. Mbali na fedha za kujikimu,
pia alisema zipo dalili za kucheleweshewa ama kutopatiwa fedha za
mafunzo kwa vitendo kwa kuwa muda wa kupewa fedha hiyo umekaribia huku
dalili zikiwa hazionekani.
Wanafunzi
hao waligoma jana kuingia madarasani huku wengi wao wakibaki wakiwa
wamejikusanya vikundi katika eneo la karibu na bwalo la kulia chakula
huku wakiimba njaa inawasumbua.
Mkurugenzi
Msaidizi wa Habari, Elimu na Mawasiliano wa HESLB, Cosmas Mwaisoba
alikiri kuwapo kwa tatizo hilo. Aliwataka walioathirika na ucheleweshaji
huo, kuwa na subira kwa kuwa taratibu za kuwalipa, zilikuwa zinafanywa.CHANZO:HABARI LEO (Muro)
No comments:
Post a Comment