Watumishi Bodi ya Mikopo watakiwa kuongeza ufanisi
Mkurugenzi
Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) Bw.
George Nyatega (mwenye tai) akipokea tuzo kutoka kwa Mwenyekiti wa Chama
cha Wafanyakazi wa Taasisi za Elimu ya Juu, Sayansi, Teknolojia, Habari
na Utafiti (RAAWU) – Tawi la HESLB Bw. Deodatus Mwiliko kutambua
uongozi wake bora katika HESLB tangu ilipoanzishwa mwaka 2005. Wengine
ni viongozi wa RAAWU-HESLB Bw. Luhano Lupogo na Bi. Octavia
Selemani. (Picha na HESLB).
Na Mwandishi wetu
Watumishi
wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) wametakiwa
kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao ili kuondokana na
malalamiko kutoka kwa wanafunzi.(P.T)
Mkurugenzi
Mtendaji wa HESLB Bw. George Nyatega ametoa wito huo mara baada ya
kukabidhiwa tuzo naChama cha Wafanyakazi wa Taasisi za Elimu ya Juu,
Sayansi, Teknolojia, Habari na Utafiti (RAAWU), tawi la Bodi ya Mikopo
ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB).
Akiongea
katika hafla fupi ya kukabidhi ngao hiyo, Mwenyekiti wa RAAWU Tawi la
HESLB Bw. Deodatus Mwiliko alisema RAAWU, Tawi la HESLB imeamua
kumkabidhi Mkurugenzi mtendaji huyo ngao hiyo kutokana na kujali na
kuboresha mazingira ya kufanya kazi kwa watumishi wote wa HESLB.
Akizungumza
mara baada ya kukabidhiwa tuzo hiyo, Mkurugenzi Mtendaji huyo alisema
amepokea tuzo hiyo kwa niaba ya menejimenti anayoingoza na wafanyakazi
wote na kuwataka watumishi wa HESLB kutoridhika na ufanisi uliopo na
badala yake waongeze juhudi.
“Ninapokea
hii ngao kwa niaba ya menejimenti na wafanyakazi wote kwa sababu
sifanyi kazi peke yangu,” alisema Bw. Nyatega jana (Alhamisi, Mei 28,
2015) katika makao makuu ya HESLB jijini Dar es Salaam.
“Ninawapongeza
kwa kufanya kazi kwa ufanisi, lakini pia muongeze juhudi katika utoaji
wa huduma kwa wanafunzi ili pasiwe na malalamiko,” amesema Bw. Nyatega.
HESLB
ilianzishwa kwa sheria ya Bunge na 9 ya mwaka 2004 na kuanza kazi rasmi
mwezi Julai, 2005 ili, pamoja na majukumu mengine kutoa mikopo kwa
wanafunzi wahitaji waliodahiliwa katika taasisi za elimu ya juu. Tangu
kuanzishwa kwake, Bw. Nyatega amekuwa Mkurugenzi Mtendaji wake.
No comments:
Post a Comment