Ripoti ya CAG yaanika madudu
Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad
RIPOTI ya
Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa
Assad, imetolewa na kuwasilishwa bungeni jana huku ikiendelea kuibua
madudu katika matumizi ya fedha.
Moja ya
madudu hayo yamebainika katika usimamizi wa rasilimali watu katika
balozi za Tanzania, ambapo watumishi waliokoma kutumikia Taifa,
wameendelea kugharimiwa katika maisha yao katika nchi hizo.
Moja ya
gharama iliyotajwa na Profesa Assad wakati alipozungumza na waandishi wa
habari katika ofisi za Bunge ni Sh milioni 543 zilizotumika kulipa
posho ya pango kwa watumishi hao baada ya kustaafu.
Katika
Ripoti ya Ukaguzi ya Serikali Kuu, Profesa Assad alikwenda ndani zaidi
na kutaja orodha ya balozi hizo ambazo watumishi wake wameendelea
kulipwa ingawa wamestaafu, kwa madai kuwa hakukuwa na fedha za
kugharimia urudishwaji wao nyumbani.
"Maofisa
hawa wastaafu, walibakia wakifanya kazi bila kuwa na mikataba kwa kuwa
Serikali ilikuwa na uhaba wa fedha, kwa ajili ya kulipia gharama ya
kuwarudisha nyumbani baada ya kufikia umri wa kustaafu," ameeleza
Profesa Assad katika ripoti yake.
*Balozi zenyewe
Ubalozi
wa kwanza kuwa na maofisa wa aina hiyo ni wa Kinshasa katika Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Congo (DRC), ambapo mtumishi alistaafu tangu Machi 28,
2014 na akalipwa posho ya Sh milioni 130.8, kutokana na kufanya kazi kwa
miezi 10 zaidi.
Katika
ubalozi huo huo, Profesa Assad alisema mtumishi huyo huyo alipewa Sh
milioni 41.2 ya kodi ya pango kwa miezi kumi aliyofanya kazi akiwa
amestaafu na hana mkataba na Serikali.
Ubalozi
mwingine ni wa Maputo nchini Msumbiji, ambapo mtu alilipwa posho ya
kufanya kazi akiwa amestaafu ya Sh milioni 204 kwa miezi 19 zaidi baada
ya kustaafu.
"Kiwango
hiki cha posho ni sawa na mara tatu ya gharama ya kumsafirisha yeye,
mizigo na familia yake," ameeleza Profesa Assad katika taarifa hiyo.
Katika
Ubalozi wa Ottawa nchini Canada, Profesa Assad alibainisha wazi kuwa
ndiko angalau kulikokuwa na mstaafu ambaye alipewa mkataba wa miaka
miwili, ingawa hakukuwa na maelezo ya sababu ya kuongezewa mkataba.
Mstaafu
huyo wa Canada yeye alilipwa Sh milioni 137.5, huku katika Ubalozi wa
Washington Marekani, mtumishi aliyefanya kazi ya miezi mitatu tu zaidi
baada ya kustaafu, akiibuka na kitita cha Sh milioni 30.
Vyama vya
siasa Wakati wanasiasa wakiwa vinara wa kushutumu watumishi wa Serikali
na hata viongozi wengine kwa matumizi mabaya ya fedha za Serikali,
Profesa Assad amebainisha kuwa vyama vinavyoongoza kwa kupokea ruzuku
kubwa kutoka serikalini, baada ya ukaguzi vimepata hati yenye mashaka.
Vyama
hivyo ni CCM, Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi huku chama kimojawapo
kilichojiunga na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) cha NLD, kikiwa
miongoni mwa vyama sita vilivyopata hati mbaya.
Akielezea
sababu ya kutoa hati hizo kwa vyama hivyo, Profesa Assad alisema
alibaini kuwa taarifa ya hesabu za vyama hivyo, zinatofautiana na
misingi ya uhasibu na mfumo wa uandaaji wa taarifa za fedha.
Vyama
vingine maarufu ambavyo hata havikupeleka taarifa zao za fedha kwa ajili
ya kukaguliwa na CAG, ni pamoja na UDP na DP, huku chama cha ADC
kinachotarajia kusimamisha mgombea urais Zanzibar, kikipata hati mbaya.
"Nashauri
Msajili ya Vyama vya Siasa kwa kushirikiana na Mhasibu Mkuu wa
Serikali, kuandaa mwongozo mzuri wa namna ya kuandaa taarifa za hesabu.
Hii itawezesha kutoa taarifa za fedha kwa ubora unaotarajiwa," alieleza
Profesa Assad.
Watumishi
hewa Profesa Assad ameendelea kubainisha kuwa ndani ya Serikali
kumeendelea kutolewa mishahara hewa, inayolipwa kwa watumishi
waliostaafu, walioacha kazi na waliofukuzwa kazi.
"Nimebaini
kuwepo kwa malipo ya shilingi milioni 141 katika taasisi saba...ambao
hawakugundulika na kuondolewa katika orodha ya mishahara kwa wakati
baada ya muda wao wa utumishi kufikia ukomo kinyume cha Sheria ya Umma
kwa Wastaafu," amesema.
Malipo
hayo yalikutwa katika Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii Sh milioni 74,
Sekretarieti ya Mkoa wa Shinyanga Sh milioni 24, Ofisi ya Waziri Mkuu Sh
milioni 13 na Sekretarieti ya Mkoa wa Morogoro Sh milioni 10.
Mishahara
mingine hewa imekutwa katika Sekretarieti ya Mkoa wa Tanga Sh milioni
10, Idara ya Huduma za Uhamiaji Sh milioni 6 na Wizara ya Mambo ya Ndani
Sh milioni 1.9.CHANZO:HABARI LEO (Muro)
No comments:
Post a Comment