Tanzania na Msumbiji zafutiana malipo ya viza
Mkataba huo mpya ulisainiwa jana kati ya Waziri wa Mambo ya Ndani wa Msumbiji, Jaime Basilio Monteiro na Waziri wa Mambo ya Ndani wa Tanzania aliyewakilishwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe.
Ziara ya kwanza ya Rais wa Msumbiji, Filipe Nyussi nchini imefanikisha kusainiwa kwa mkataba wa kuondoa malipo ya viza kwa wanadiplomasia, wafanyabiashara na wananchi baina ya nchi hizo mbili.
Mkataba huo mpya ulisainiwa jana kati ya Waziri wa Mambo ya Ndani wa Msumbiji, Jaime Basilio Monteiro na Waziri wa Mambo ya Ndani wa Tanzania aliyewakilishwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe.
Makubaliano hayo yalifikiwa baada ya mazungumzo kati ya Rais Nyussi na mwenyeji wake, Jakaya Kikwete, Ikulu jijini hapa.
"Hakutakuwa tena na viza kwa Watanzania wanaokwenda Msumbiji. Awali, walilazimika kulipa Dola za Marekani 900 (zaidi ya Sh1.8 milioni) kwa muda wa siku 30 wakati wao walikuwa wanalipa Sh10,000 kwa siku 90. Baada ya mkataba huu, hakutokuwa tena na malipo hayo," alisema Membe.
Waziri Membe alifafanua kuwa mkataba huo umeondoa pia malipo ya viza kwa muda huo kwa wafanyabiashara, wanadiplomasia pamoja na wananchi wa kawaida lakini wanafunzi wamepewa kipaumbele cha pekee kwani hawatotakiwa kulipa kwa muda wote wa masomo yao.
Alisema uhusiano wa muda mrefu baina ya nchi mbili hizi, umechangia kwa kiasi kikubwa kufikia uamuzi huo na katika siku zijazo, wanatarajia kufanya mazingira ya kuvuka mipaka yasiwe kikwazo kwa maendeleo ya wananchi wake.
Rais Nyussi aliwasili nchini jana na atafanya ziara ya siku tatu itakayomfikisha pia Zanzibar ambako atazungumza na Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), Dk Ali Mohammed Shein kabla ya kuelekea Dodoma ambako atatembelea Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) kabla ya kulihutubia Bunge
No comments:
Post a Comment