17 mahakamani kwa jaribio la kumpindua Nkurunziza
Jenerali
Niyungeko Juvenal (katikati) akipelekwa katika Mahakama Kuu mjini
Bujumbura kujibu shtaka la kujaribu kumpindua Rais Pierre Nkurunziza.
Picha na AFP.
Bujumbura,
Burundi. Maofisa 17 wa Jeshi la Burundi wametiwa mbaroni wakiwamo
majenerali watano na kufikishwa mahakamani kwa kosa la kuipindua
Serikali ya Rais Pierre Nkurunziza.
Wanajeshi
watatu wametajwa kuwa vinara wa kupanga njama za kuipindua Serikali ya
Burundi wakiwamo maofisa wawili wa ngazi za juu wa polisi.
Msemaji
wa Ikulu ya Burundi, Gervais Abayeho alisema jana kwamba washtakiwa
wengine wanne ni maofisa wenye vyeo vya chini na wanane ni wanajeshi wa
kawaida.
Mpaka sasa hakuna taarifa yoyote ya kukamatwa kwa Meja Jenerali Godefroid Niyombare ambaye aliongoza mapinduzi hayo.
Askaribi
hao wanatuhumiwa kufanya jaribio la kumpindua Rais Nkurunziza wakipinga
uamuzi wake wa kugombea urais kwa muhula wa tatu.
Abayeho
alisema wakati maandamano yakiendelea Bujumbura kupinga uamuzi wa Chama
cha CNDD-FDD kumteua Nkurunziza kugombea nafasi hiyo kwa mara nyingine,
Meja Jenerali Niyombare alitangaza kutomtambua Nkurunziza kama rais wa
nchi hiyo. Mawakili wanaowatetea watuhumiwa hao walisema kwamba baada ya
wateja wao kukamatwa waliteswa na kuumizwa.
"Wamepigwa
na ukiwatazama wamechoka na hawana mashati wala viatu," alisema mmoja
wa mawakili wanaowatetea watuhumiwa hao kutoka Kampuni ya Mawakili ya
Bar, Miburo Anatole.
Anatole
alisema anamwakilisha Meja Jenerali Cyrille Ndayirukiye ambaye alikuwa
waziri wa zamani wa ulinzi wa nchi hiyo na maofisa wawili wa polisi.
Wakili
mwingine, Cyriaque Nibitegeka alisema mteja wake ambaye ni ofisa wa
jeshi la nchi hiyo alilazimishwa kwa mtutu wa bunduki kukiri kwamba
alihusika kuipindua nchi hiyo. Alisema mteja huyo amegoma kula tangu
walipokamatwa wiki iliyopita.
Taarifa zilieleza kwamba endapo watuhumiwa hao watapatikana na hatia watahukumiwa kifungo cha miaka 15 gerezani.
Ijumaa iliyopita, Nkurunziza alirejea mjini Bujumbura akitokea Tanzania, huku maandamano ya kumpinga yakiendelea.
Licha ya
Serikali kuzuia kufanyika kwa maandamano, waandamanaji vikiwamo vyama
vya upinzani na wananchi wameapa kuendelea hadi Rais Nkurunziza
atakapotangaza kuacha mpango wake wa kugombea tena urais.CHANZO:
MWANANCHI (Muro)
No comments:
Post a Comment