UFISADI WA MABILLION USWISI WATIKISA NCHI
Na Julius Magodi na Habel Chidawali, Dodoma
MJADALA
mkali uliibuka bungeni jana baada ya Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto
Kabwe (Chadema) kuwalipua baadhi ya viongozi waandamizi wa Serikali
akitaka wachunguzwe kwa makosa ya kuficha mabilioni ya fedha nje ya
nchi.
Zitto alitoa kauli hiyo jana bungeni wakati akiwasilisha hoja yake
binafsi kuhusu kulitaka Bunge kuchunguza na kuielekeza Serikali
kuchukua hatua dhidi ya raia wa Tanzania walioficha fedha na mali
haramu nje ya nchi.
Bila
ya kuwataja kwa majina, mbunge huyo aliwataja watu hao kwa nyadhifa
kuwa ni watu wote walioshika nyadhifa za uwaziri mkuu katika kipindi cha
2003 hadi 2010, walioshika nyadhifa za uwaziri wa nishati na madini
katika kipindi hicho na waliokuwa makatibu wakuu Wizara ya Nishati na
Madini.
Wengine
ni mawaziri na makatibu wakuu wa Wizara ya Ulinzi, wakuu wa majeshi,
wanasheria wa Serikali, makamishna wa nishati, walioshika wadhifa wa
Ukurugenzi Mkuu wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC),
Uenyekiti na Ujumbe wa Bodi wa TPDC katika kipindi cha mwaka 2003 hadi
2010. Kutokana na hilo, Zitto aliitaka Serikali kupeleka bungeni muswada
wa sheria bungeni wakati wa Mkutano wa 11 wa Bunge wa Aprili mwakani.
“Mbali
na hilo napendekeza kuwa iwe ni marufuku kwa kiongozi yeyote wa umma
au mume au mke wake au mtoto wake kuwa na akaunti nje ya nchi isipokuwa
kwa sababu maalumu na kwa kibali rasmi kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya
Muungano,” alisema Zitto.
Pia
Zitto alitaka Serikali kuwasiliana na Benki ya Dunia kupitia kitengo
cha ‘Assets Recovery Unit’ ili mabilioni ya fedha na mali ambazo
zimetoroshwa nje ya nchi kwenda Uswisi, Dubai, Mauritus na maeneo
mengine ziweze kurejeshwa.
Aliwataka
Watanzania wote wenye akaunti za fedha nje ya nchi waeleze wamezipata
wapi na Takukuru wachukue hatua za kisheria dhidi ya watu wote
wanaomiliki fedha hizo kinyume cha sheria.
Zitto
alisema katika mkutano wa Bunge la 11 na baada ya taarifa ya Kamati
Teule ya Bunge kuhusu raia wa Tanzania wenye kumiliki fedha za kigeni
kwenye benki na mali nje ya Tanzania ilete taarifa ya hatua ilizochukua
ili kuziba mianya ya utoroshaji wa fedha nje ya nchi.
Alipendekeza
kwamba Serikali katika bajeti ya mwaka 2013/14 ianzishe kodi maalumu
ya asilimia 0.5 ya thamani ya fedha zilizotoroshwa ili kuweka rekodi za
uhakiki fedha za ndani na zinazotoka nje.
Mbunge
huyo alisema mazungumzo yake na wachunguzi wake binafsi kiwango cha
fedha kinachomilikiwa na Watanzania Uswisi peke yake ni takriban mara 20
ya kiwango kilichotangazwa na benki ya taifa ya nchi hiyo. Alisema
fedha hizo ni sehemu tu ya fedha ambazo Watanzania wamezificha katika
benki mbalimbali za nje.
Alitoa
mfano wa Benki ya UBS peke yake iliyopo katika nchi hiyo ina maofisa
240 ambao wanashughulikia wateja wa Tanzania na kila ofisa mmoja
husimamia mteja mmoja mwenye kiwango kisichopungua dola za Marekani 10
milioni.
Zitto
alisema Benki Kuu ya Uswisi ilitangaza kuwa jumla ya dola za Marekani
196 milioni zilikuwa zimehifadhiwa kwenye akaunti za benki za nchi
hiyo. Alisema kuwa pamoja na Mkurugenzi wa Takukuru kukaririwa akisema
kuwa ataiandikia Serikali ya Uswisi barua kuomba kurejeshwa kwa fedha
hizo, lakini mpaka sasa hakuna hatua zilizochukuliwa.
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment