LOWASA AWAUNGA MKONO CHADEMA
Ni kuhusu elimu bure hadi sekondari, asema iwe moja ya ajenda za ccm 2015
WAZIRI Mkuu 
wa zamani, Edward Lowassa amesema wakati umefika kwa sasa hapa nchini 
elimu ya Sekondari iwe elimu bure na kumwondolea mwananchi wa kawaida 
mzigo wa kubeba gharama za elimu hiyo.
Lowassa 
akizungumza jana mjini Babati alisema, mjadala kuhusu elimu kutolewa 
bure hadi sekondari haukwepeki, hivyo kuwataka wadau wa elimu kuanza 
sasa kujadili suala hilo na kwamba Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinapaswa 
kulifanya hilo kuwa moja ya ajenda zake katika Uchaguzi Mkuu wa 2015.
Alisema 
elimu ya sekondari ikifanywa bure, itakuwa ni fursa kwa kila mtoto wa 
Kitanzania kuipata. Hatua ambayo itaongeza weledi na uelewa wa mambo 
mengi katika jamii.
“Ninasema 
sasa wakati umefika elimu ya sekondari kuwa kama elimu ya msingi kwa 
watoto kusoma bure kuanzia kidato cha kwanza hadi kidato cha nne,” 
alisisitiza Lowassa ambaye ni Mbunge wa Monduli (CCM).
Kwa kauli 
hiyo, Lowassa ni kama ameunga mkono Sera ya Chama cha Demokrasia na 
Maendeleo (Chadema) ambao waliingia katika mgogoro na CCM kuhusu elimu 
kutolewa bure wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa 2010.
Chadema 
wamekuwa wakisisitiza kwamba elimu bure inawezekana hadi ngazi ya 
sekondari, lakini wakati wote CCM wamekuwa wakisema kuwa suala hilo 
haliwezekani na kwamba kauli za aina hiyo ni kuwahadaa wananchi.
Katika 
Uchaguzi Mkuu wa 2010, aliyekuwa mgombea wa urais kupitia Chadema, Dk 
Willibrod Slaa alitumia sera ya elimu bure kuanzia chekechea hadi 
sekondari kama kete ya kusaka ushindi, huku akisema chama chake 
kingetenga asilimia 35 ya bajeti kwa ajili ya kuboresha elimu na kutoa 
elimu bure.
Hata hivyo, 
aliyekuwa mgombea wa CCM na baadaye kupata ushindi, Rais Rais Jakaya 
Kikwete alikuwa akiwatahadharisha wapigakura kuwa kwamba ahadi ya 
Chadema ni hewa na kwamba hilo lisingewezekana.
Mvutano huo 
uliwaingiza makada wengine ambao ni Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman 
Kinana ambaye wakati huo alikuwa Meneja Kampeni wa CCM na Waziri wa 
Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samwel Sitta na kwa upande wa Chadema, 
Dk Kitila Mkumbo naye alijitokeza kutetea sera ya chama chake.
Katika 
mkutano wa kampeni za CCM uliofanyika Novemba 10, 2010 katika Kata ya 
Mchangimbore katika Jimbo la Peramiho mkoani Ruvuma, Rais Kikwete 
alisema “Serikali haiwezi kutoa huduma za jamii bure” na kwamba lazima 
wananchi wachangie.
“Nimebahatika
 kukaa serikalini muda mrefu hiyo sera ya bure tulijaribu na ikatushinda
 na wakati huo Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, tulikaa naye 
tukaona hilo haliwezekani tukaamua tubadilishe sasa nawashangaa wenzetu 
wanawadanganya eti watatoa bure.”
Kwa upande 
wake Dk Slaa akiwa mjini Arusha katika moja ya mikutano yake alisema 
kwamba CCM walikuwa wakipinga sera ya elimu bure hadi sekondari kutokana
 na kulea ubadhirifu na kuthamini anasa kuliko maendeleo kwa wananchi.
Kauli ya Lowassa
Jana akizungumza muda mfupi kabla ya kuanza kuendesha harambee ya ujenzi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheli Tanzania (KKKT) Usharika wa Babati, Lowassa alisema wakati umefika kwa kila Mtanzania kuzungumzia suala hilo bila ya woga.
Kauli ya Lowassa
Jana akizungumza muda mfupi kabla ya kuanza kuendesha harambee ya ujenzi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheli Tanzania (KKKT) Usharika wa Babati, Lowassa alisema wakati umefika kwa kila Mtanzania kuzungumzia suala hilo bila ya woga.
Mwananchi

No comments:
Post a Comment