CONGO YAWASILI KUIVAA SERENGETI BOYS
Congo 
Brazzaville imewasili leo alfajiri (Novemba 15 mwaka huu) kwa ajili ya mechi ya 
raundi ya mwisho ya mchujo kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Afrika kwa 
vijana wenye umri chini ya miaka 17 dhidi ya Tanzania (Serengeti Boys) 
itakayochezwa Jumapili.
Timu hiyo 
imewasili kwa ndege ya Ethiopian Airlines ikiwa na msafara wa watu 30 wakiwemo 
wachezaji 18 ambapo imefikia kwenye hoteli ya Sapphire. Mechi hiyo itafanyika 
Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10 kamili jioni. 
Serengeti Boys 
inaendelea na mazoezi kwenye Uwanja wa Taifa chini ya Kocha wake Jackob 
Michelsen wakati Congo inafanya mazoezi leo jioni Uwanja wa Karume, na kesho 
(Novemba 16 mwaka huu) asubuhi na jioni itafanya mazoezi kwenye uwanja huo huo. 
Timu hiyo 
ambayo katika raundi ya pili iliitoa Zimbabwe itafanya mazoezi yake ya mwisho 
Jumamosi jioni kwenye Uwanja wa Taifa. Viingilio kwenye mechi hiyo ni sh. 10,000 
kwa VIP A, sh. 5,000 kwa VIP B wakati VIP C ni sh. 2,000 tu. Kiingilio kwa viti 
vya rangi ya chungwa, kijani na bluu ni sh. 1,000 tu.
Makocha wa 
timu zote mbili na manahodha wao watakutana na waandishi wa habari Jumamosi saa 
5 asubuhi kwenye ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) 
kuzungumzia maandalizi yao kwa ajili ya mechi hiyo kabambe.
Boniface 
Wambura
Ofisa 
Habari
Shirikisho la 
Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

No comments:
Post a Comment