LEO SIKU YA UKIMWI DUNIANI  WAKAZI WA DAR WAHIMIZWA KUPIMA AFYA ZAO NA  JK KUHUTUBIA TAIFA
Na: Aron Msigwa – 
MAELEZO. Dar 
es salaam. 
 Wakazi wa mkoa wa Dar es salaam wameshauriwa 
kujitokeza kupima afya zao mara kwa mara na kujiepusha na vitendo vinavyochangia 
maambukizi ya Virusi vya Ukimwi. 
Akizungumza na 
waandishi wa habari kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Dar es salaam leo jijini Dar es 
salaam Afisa habari wa mkoa huo Bi. Adrofina Ndyeikiza amesema kuwa kuna umuhimu 
wa jamii kujitambua na kushiriki kikamilifu katika kufanya tathmini ya mapambano 
dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi na namna bora ya kujikinga. 
Amesema kila mwaka 
ifikapo tarehe 1 Desemba Tanzania huungana na mataifa mengine kuadhimisha siku 
ya Ukimwi Duniani kwa kuwahusisha wadau mbalimbali ambao wote kwa pamoja hupata 
nafasi ya kutathmini mikakati ya kudhibiti Ukimwi iliyofanyika kwa muda wa mwaka 
mzima na kutafuta mbinu za kuboresha harakati hizo. 
Amesema 
maadhimisho hayo yatakayofanyika katika viwanja vya Biafra jijini Dar es salaam 
umeichagua na kuipa heshima manispaa ya Kinondoni kuandaa maadhimisho hayo 
“Maadhimisho ya 
Siku ya Ukimwi duniani mwaka huu yanabeba ujumbe ule ule uliotolewa  
mwaka jana ambapo kauli mbiu hii inaendelea mpaka mwaka 2015 na kwa mwaka 
huu  jijini Dar es salaam yanafanyika katika uwanja wa Biafra 
yakiongozwa na kauli mbiu ya Tanzania Bila Maambukizi Mapya, Unyanyapaa na vifo 
vitokanavyo na Ukimwi Inawezekana” 
Amesema lengo la 
kauli mbiu hiyo ni kuhamasisha na kuelimisha zaidi jamii kuhusu VVU na Ukimwi na 
kubadilisha tabia ili kujikinga na maambukizi ya mapya ya VVU, kuhamasisha jamii 
kuacha kabisa unyanyapaa, unyanyasaji na ubaguzi kwa watu wanaoishi na VVU na 
ubaguzi kwa watu wanaoishi na VVU na UKIMWI na kuboresha huduma za afya na tiba 
ya magonjwa nyemelezi na dawa za kufubaza makali ya VVU 
(ARVs). 
Bi. Ndyeikiza 
amesema kuwa mbali na maadhimisho hayo katika mkoa wa Dar es salaam serikali kwa 
kushirikiana na Asasi zisizo za kiserikali zilizo katika mapambano dhidi ya 
ugonjwa huo zinaendelea kuwapatia wananchi huduma za elimu, ushauri na upimaji 
wa hiari wa VVU  katika maeneo 
mbalimbali. 
Kwa upande wake 
mratibu wa Ukimwi wa mkoa wa Dar es salaam kutoka  Tume ya 
Kudhibiti Ukimwi nchini (TACAIDS) Bw. Omary Chambo amesema kuwa jamii bado 
inahitaji elimu juu ya namna na mikakati ya kukabiliana na virusi vya Ukimwi na 
hatimaye kupunguza maambukizi mapya ya Virusi vya 
Ukimwi. 
Amesema takwimu za 
mwaka 2012 kwa mkoa wa Dar es salaam zinaonyesha kuwa katika Manispaa ya Ilala 
hali ya maambukizi ni 8.3%, Temeke 6% na Manispaa ya Kinondoni ni 6.7 na 
kuongeza kuwa vitendo vya unyanyapaa miongoni mwa jamii kwa waathirika wa 
ugonjwa huo vinachangia watu wengi wasijitokeze kupima kwa hiari ili kujua kama 
wanaishi na VVU. 
“Vitendo vya 
unyanyapaa vimekua sababu ya kuwafanya wengi wasijitokeze kupima kuhofia 
kutengwa na jamii pindi watakapogundulika kuwa wameathirika , hivyo tunaendelea 
na juhudi ya kuwaelimisha wananchi kuepuka vitendo hivyo na wajitokeze kupima 
afya zao kwa hiari” ameeleza Bw. Omary. 

No comments:
Post a Comment