MAHAKAMA YAAMURU MADIWANI WATANO KUILIPA CHADEMA SH. MILLION 15
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Arusha, imewaamuru madiwani watano waliotimuliwa Chadema kulipa gharama za kesi waliyokuwa wamefungua kupinga kufukuzwa uanachama, vinginevyo watapelekwa magereza.
Hakimu
Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Charles Magesa alitoa hukumu hiyo jana
baada ya Chadema kushinda kesi hiyo.Hakimu Magesa alisema madiwani hao
wanapaswa kulipa Sh15 milioni ndani ya miezi miwili, wakishindwa
watapelekwa gerezani.
Madiwani hao ni Estomih Mallah (aliyekuwa Naibu
Meya ya Manispaa ya Arusha kipindi hicho), John Bayo aliyekuwa Diwani wa
Elerai, Reuben Ngowi (Themi), Charles Mpanda (Kaloleni) na Rehema
Mohamed aliyekuwa Diwani wa Viti Maalumu.
Pia, katika kesi hiyo ya madai Chadema walikuwa
wakiwakilishwa na Wakili Method Kimomogoro, wakati wadaiwa hao walikuwa
wakijitetea wenyewe baada ya aliyekuwa wakili wao kujitoa.Akisoma uamuzi huo, Hakimu Magesa alisema baada ya
mahakama kupitia hoja za pande zote, imeona wadaiwa hao wanapaswa
kulipa zaidi ya Sh15.1 milioni, kila mmoja anatakiwa kulipa zaidi ya
Sh3.2 milioni katika kipindi kisichozidi miezi miwili.
Awali, kulikuwa na mvutano kati ya wadaiwa hao
jambo lililosababisha kesi hiyo kusikilizwa kwa kipindi kirefu ambapo
walitakiwa kueleza mahakama hiyo sababu ya kutokupelekwa gerezani, huku
kila mmoja akitamka kiwango cha fedha ambacho angeweza kulipa kwa mwezi.
Kwa upande wake, Ngowi alisema ana uwezo wa kulipa
Sh25,000 kwa mwezi, Mpanda Sh20,000, Mallah Sh20,000, Rehema Sh15,000
na Bayo Sh15,000 kwa mwezi bila kuonyesha mchanganuo wa kipato chao,
jambo lililopingwa vikali na Wakili Kimomogoro kwamba kiwango hicho ni
kidogo.
Hakimu Magesa alisema kisheria mtu akishinda kesi
ana uwezo wa kuchagua hukumu ya kulipwa kwa kuchukua mali za mdaiwa au
mlalamikiwa kupelekwa kifungoni.
“Kimsingi mtu anaposhinda kesi lazima alipwe
gharama aliyotumia na iwapo mahakama itaridhia alipwe kwa kiwango hicho,
itachukua muda mrefu kati ya miaka 10 na 16 kumaliza deni hilo, jambo
litakalosababisha aliyeshinda kushindwa kuona matunda ya ushindi wake,”
alisema Magesa.
Alisema fedha hizo wanapaswa kuzilipa mara mbili,
awamu ya kwanza inatakiwa kila mmoja kulipa zaidi ya Sh1.5 milioni na
wawe wamemaliza kwa miezi miwili na kwamba, iwapo watashindwa mdai
anaweza kupeleka mchanganuo wa gharama za kumtunza mfungwa na mahakama
kuupitia na baadaye kutoa amri wapelekwe
gerezani
No comments:
Post a Comment