TIFFAN ENT

TIFFAN ENT

TUKO WANGAPI

TUKO WANGAPI

GLORY FREIGHT

GLORY FREIGHT

Tuesday, November 20, 2012

RIPOTI YA TUME YA UCHUNGUZI WA AJALI YA MELI YA MV SKAGIT IPO HADHARANI

Na Mauwa Mohammed, Zanzibar (Tanzania Daima)

TUME ya Rais wa Zanzibar ya kuchunguza chanzo cha ajali ya kuzama kwa meli ya Skagit, imetoa ripoti yake ikisema kuwa meli hiyo ilisajiliwa kinyume cha sheria na hivyo kupendekeza msajili wa meli hiyo, Seif Juma, achukuliwe hatua kali za kinidhamu.
Akitoa taarifa ya tume kwa waandishi wa habari mjini Zanzibar jana, Katibu Mkuu Kiongozi wa SMZ, Abdullahamid Yahaya Mzee, alisema tume imebaini kuwa taarifa za idadi ya abiria waliopanda meli siku ya tukio pia ilikuwa ni potofu.
Alisema kuwa tume hiyo ilibaini pamoja na mambo mengine, kuwa meli hiyo ilikuwa na idadi ya abiria 447 wakiwemo Watanzania 429 na raia wa kigeni 18 tofauti na idadi iliyotolewa awali na uongozi wa meli hiyo kuwa ilikuwa na abiria 295 wakiwemo wafanyakazi kumi wa meli hiyo.
Hata hivyo, taarifa ya tume hiyo ilitofautiana na taarifa zilizokuwa zikitolewa na Jeshi la Polisi kuhusiana na idadi ya maiti zilizokuwa zikipatikana siku hadi siku.
Katika ripoti hiyo, watu 81 walipoteza maisha tofauti na taarifa zilizokuwa zikitolewa na polisi kuwa hadi kufikia Agosti 11, mwaka huu, idadi ya watu waliopoteza maisha ilikuwa ni 143.
Maiti za watu 222 zilipatikana katika maeneo mbalimbali ya mwambao mwa bahari kwa upande wa Zanzibar na nyingine 21 zikapatikana mkoani Tanga.
Hata hivyo baada ya kuonekana kwa kasoro hiyo, baadhi ya waandishi walikuwa na wasiwasi kuwa huenda tume hiyo haikupata taarifa kutoka polisi na madaktari waliofanya uchunguzi wa miili ya watu iliyokuwa ikipatikana siku hadi siku tangu kutokea kwa tukio hilo.
Tume hiyo iliyokuwa ikiongozwa na Jaji wa Mahakama Kuu, Aabdruhakim Ameir Issa, pia imetoa mapendekezo kuwa watu watano akiwemo mmiliki wa meli hiyo, Saidi Abdallahmani Juma na nahodha Mussa Makame Mussa pamoja na meneja mkuu wa kampuni ya Sea Gall inayomiliki meli ya Skagit, Omari Mnkonje, washtakiwe mahakamani.
Wengine wanaotakiwa kushtakiwa ni nahodha wa meli hiyo na mhandisi wa zamu wa meli hiyo.
Mv ilizama Julai 17 mwaka huu baharini karibu na kisiwa kidogo cha Chumbe na kusababisha vifo kadhaa.
http://www.freemedia.co.tz/daima/habari.php?id=42655

No comments:

Post a Comment