Tamu, chungu ya kuhamia mfumo wa matangazo ya dijitali
Tanzania
juzi iliungana na jumuiya ya kimataifa kuadhimisha uzimaji rasmi wa
mfumo wa matangazo ya analojia, huku ikiwa ni miongoni mwa nchi za
kwanza katika nchi zilizo kusini ya Jangwa la Sahara.
Maadhimisho
hayo yamefanyika ikiwa ni mwaka mmoja na nusu wa mafanikio na
changamoto tangu kuanza safari ya kuingia katika matangazo ya dijitali,
ambayo ilianza rasmi Januari mosi, mwaka 2013 na kukamilika miezi mitatu
iliyopita.
Ujio wa
matangazo ya dijitali umefungua fursa mbalimbali za kiteknolojia,
kihuduma na kibiashara kwa watoa huduma za televisheni, wafanyabiashara
wadogo wadogo, mafundi na wananchi.
Kauli ya TCRA
Mkurugenzi
Mkuu wa TCRA, Profesa John Nkoma anasema kuwa Tanzania imepiga hatua
kwa kuwa mpaka sasa kuna visimbuzi milioni moja sokoni.
Anasema
kuwa mafanikio hayo yametokana na uamuzi wa Serikali kuweka sheria,
taratibu na kanuni ambazo wadau wamezitambua, tofauti na ilivyo katika
nchi nyingine za Afrika, ambazo bado hazijazima mfumo wa analojia.
Profesa
Nkoma anasema kwamba mamlaka hiyo iliwashawishi watu kununua visimbuzi,
lakini haikuwa na maana kuwa vyote vitakuwa na chaneli za ndani, ambazo
zinaonyeshwa bure.
Anaeleza
kwamba baadhi ya visimbuzi ni vya kibiashara, hivyo haiwezekani
kulazimishwa kuweka chaneli za bure za kitaifa. Anavitaja visimbuzi
hivyo vinavyopaswa kuonyesha chaneli tano za bure kuwa ni Digitek,
Continental, Startimes na Agape.
Faida za dijitali
Matokeo
ya ripoti iliyotolewa na jopo la wataalam kutoka Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam (UDSM) ya mwaka 2013, yanabainisha faida za kutumia mfumo wa
dijitali katika mawasiliano kuwa ni pamoja na kupata sauti na picha bora
na matumizi bora ya masafa, ambapo chaneli moja ya analojia hutumiwa na
kituo kimoja cha utangazaji wakati kwa mfumo wa dijitali chaneli hiyo
hutumiwa na vituo zaidi ya kumi.(VICTOR)
Faida
nyingine ni kuwa mitambo ya kurusha matangazo kutumia nguvu ndogo ya
nishati na kuwepo kwa luninga za mkononi (Mobile TV) kwenye mfumo wa
dijitali.
Wananchi wanasemaje?
Wakati
TCRA na baadhi ya wadau wakijivunia mafanikio ya mchakato huo yakiwemo
kuongeza nafasi kubwa ya masafa na urahisi wa kurusha matangazo, bado
kuna baadhi ya wananchi wanahaha kuendana na teknolojia hususan kumudu
gharama za huduma husika.
Fundi wa
kufunga madishi ya matangazo ya televisheni mkoani Mtwara, Ali Mnunduma
anasema kuwa idadi ya wanaotumia visimbuzi imeongezeka kwa kiasi kikubwa
kutokana na kupata wateja wengi wanaotafuta huduma za kufungiwa madishi
hayo kwenye makazi yao.
“Ukilinganisha
na mwaka jana, kwa sasa watu wameamka hasa baada ya Serikali kutangaza
kuwa wanazima matangazo ya analogia Songea na Mtwara, lakini wengi bado
wanalalamika kuwa hawawezi kulipia Ankara za kila mwezi, hivyo
tuwashauri au tuwatafautie visimbuzi vyenye chaneli zote za ndani na vya
bei nafuu,” anasema Mnunduma.
Maumivu
na mkanganyiko wa uelewa juu ya kupata visimbuzi vyenye chaneli tano za
taifa za bure na vyenye ahueni ya malipo, vinazidi kutesa idadi kuwa ya
Watanzania na kuwafanya baadhi kununua kisimbuzi zaidi ya kimoja au
kushindwa kabisa na kubaki kuangalia mikanda ya video pekee.
“Ni kweli
lazima tuendane teknolojia kama Serikali inavyotaka lakini ‘bill’
(Ankara) za kila mwezi zinatuumiza sana hasa pale unapotaka chaneli
nzuri, kuna baadhi ya ving’amuzi ikiisha fedha yako hupati hata TBC,”
anaeleza Abdallah Khamis mkazi wa Vingunguti, jijini Dar es Salaam.
Khamis
anasema kuwa amenunua visimbuzi vya aina tatu tofauti, vingine vikiwa
vya madishi bila kuridhika na huduma zinazotolewa na kuamua kuvitumia
wakati anapopata pesa pekee.
“Unapokuwa
na biashara lazima uangalie soko likoje, biashara inaendaje na ubora wa
huduma, sio kama karanga ukienda sokoni utakuta hazina thamani kwa kuwa
kila mtu anazo,” anaeleza Profesa Nkoma, alipoulizwa iwapo kuna
uwezekano wa kuongeza watoa huduma wengine wa visimbuzi ili kuongeza
ushindani na kushusha bei ya bidhaa hizo.
Ukweli wa
idadi ya Watanzania wasiopata huduma ya televisheni kutokana na
kutomudu gharama za kununua visimbuzi na zile za mwisho wa mwezi, bado
ni giza nene kutokana na kutokuwepo utafiti mpya zaidi zile za mwaka
2013.
Utafiti wa UDSM
Matokeo
ya utafiti wa Chuko Kikuu cha Dar es Salaam(UDSM), yanaonyesha kuwa
asilimia 89 ya kaya zilikuwa zikitumia huduma ya matangazo kwa mfumo wa
kidijiti bila matatizo baada ya uzimaji wa mitambo ya analojia kwenye
miji saba ilikofanyika tathmini, huku asilimia 11 ya kaya zikishindwa
kupokea matangazo hayo kwa sababu mbalimbali.
Ripoti
hiyo ilibainisha kwamba kati asilimia hizo 11, asilimia 5.5 hawakununua
visimbizi, asilimia 0.1 walisema vilikuwa havipatikani, asilimia 3.2,
walisema bei ipo juu na asilimia 0.2 walisema visimbuzi vyao vilikuwa
vibovu.
“Zoezi
hili halijawanyima Watanzania haki ya kupata habari kwani wengi tayari
wameshajiunga na mfumo huu mpya. Jopo liliona kuwa sababu ya malalamiko
mengi ni tabia halisi ya wanadamu kuogopa mabadiliko,” inasema ripoti ya
UDSM.Utafiti Twaweza
Hata
hivyo, ripoti hiyo inakizanzana na ile iliyotolewa na Taasisi ya
Twaweza, Novemba 2013, iliyoonyesha kuwa zaidi ya asilimia 50 ya wakazi
wa Jiji la Dar es Salaam hawakukubaliana na uamuzi wa Serikali kufunga
mfumo wa analojia.
Kwa
mujibu wa ripoti hiyo namba 21, inaonyesha kuwa gharama za kununua
king’amuzi, kukilipia kila mwezi na mwonekano hafifu zilichangia
uharakishaji wa watumiaji wa televisheni kuhama kutoka mfumo wa analojia
kwenda dijitali.
Pamoja na
gharama kununua visimbuzi na gharama za kila mwezi, kuna kila dalili
kuwa Watanzania watahitajika tena kutoboa mifuko yao zaidi ili kuangalia
televisheni kutokana na kuongezeka kwa bei ya vifaa hivyo na huduma,
baada ya kasi ya kushuka kwa thamani ya Shilingi.
Kaui ya Tido
Naibu
Mtendaji Mkuu wa Azam Televisheni, Tido Mhando anasema kuwa Tanzania
imefanikiwa kutokana na utayari wa wadau na ari ya Serikali katika
kusimamia mchakato wa kuhamia dijitali tofauti na ilivyokuwa katika nchi
nyingine ikiwemo Kenya.
Tido
aliyeliongoza Shirika la Utangazaji Tanzania(TBC) katika hatua za
kuingia mfumo wa dijitali anasema changamoto kubwa zilizosalia ni uwezo
mdogo wa baadhi ya wananchi kushindwa kulipia huduma za kila mwezi za
visimbuzi na mkanganyiko miongoni mwao katika kupata king’amuzi
kinachokidhi mahitaji yote ya huduma ambazo zinaweza kutatuliwa na baina
ya Serikali na wadau.
Hata
hivyo, matumaini ya kushuka zaidi bei ya huduma za visimbuzi kwa sasa ni
hafifu huku Tido akibainisha kuwa gharama za uendeshaji (hasa uingizaji
visimbuzi na ununuzi wa maudhui ya nje) zimeongezeka kutokana na
kushuka kwa thamani ya shilingi hali itakayozisukuma kampuni
zinazohusika kuongeza bei.
“Watoa
huduma (subscribers) wananunua maudhui ya nje kwa fedha za kigeni kuuza
Tanzania. Kwa sababu na sarafu yetu imeshuka...kuna uwezekano mkubwa
kupandisha bei ya ving’amuzi kwa sababu havina faida tena.”
“Wananchi
nao lazima waelewe hivyo na suala zima la hali ya uchumi wa nchi
linaathiri mambo mengi...huenda hao watu wa ving’amuzi wangetaka
kushusha bei, lakini hawawezi kwa sababu hawana njia nyingine labda
shilingi iimarike siku za karibuni,” anasema Tido.
Njia mbadala
Vilio vya
Watanzania wasio na uwezo wa kumudu gharama hizo vinaweza vikatatuliwa
iwapo Serikali itatoa ruzuku au unafuu wa kikodi kwa wasioweza kununua
visimbuzi, kudhibiti bei ya malipo ya mwezi na kutumia njia mbadala
zisizo za kulipia, kama anavyoeleza Mtaalamu wa Teknolojia ya Habari na
Mawasiliaono, Dk Geoffrey Karokola.“Kwa wale ambao hawawezi kulipia kila
mwezi wanaweza kununua televisheni yenye king’amuzi ndani na kupata
chaneli za bure zaidi ya 90 na mimi natumia hivyo,” anaeleza Dk Karokola
wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
“Pia, kwa
wenye televisheni zisizo za dijtali wanaweza kununua visimbuzi visivyo
na gharama za kila mwezi kwa kufunga madishi ya mfumo wa C-Band au Ku na
watapata chaneli za ndani na nje bure.”CHANZO:MWANANCHI
No comments:
Post a Comment