Mkasa uliompata Rais wa Misri nchini Ujerumani

Rais wa Misri Abdal-Fattah Al-Sisi
Kisa cha kushangaza na kufadhaisha kimetokea katikati ya wiki iliyopita katika mji mkuu wa Ujerumani, Berlin.
Rais wa 
Misri, Abd al-Fattah Al-Sisi, alikuwa katika ziara rasmi ya siku tatu 
ambayo ilizusha mabishano miongoni mwa wanasiasa wa Ujerumani kabla na 
zaidi wakati ilipokuwa inafanyika.
Wako wale
 waliosema kwamba licha ya utawala wa Al-Sisi tangu ulipompindua kutoka 
madarakani na kumtupa gerezani mtangulizi wake, Mohammed Mursi wa Chama 
cha Udugu wa Kiislamu, umefurutu ada katika kukandamiza haki za 
binadamu, hata hivyo, ni vizuri kufanya mazungumzo na kiongozi huyo.
Hawa 
walitoa sababu kuwa Misri ni taifa kubwa la Kiarabu ambalo liko katika 
eneo tete na lenye ufunguo wa kuyatatua matatizo ya eneo hilo.(P.T)
        
Lakini 
kuna wanasiasa wengine waliohoji kwamba madikteta kama huyo wa Misri- 
aliyewahi kuwa waziri wa ulinzi chini ya Mursi, ni mtu anayekanyaga haki
 za binadamu na kuwafumba midomo maelfu ya wapinzani wake kwa kuwatia 
magerezani, hivyo hastahiki kupokelewa Ujerumani.
Spika wa 
Bunge la Ujerumani, Nobert Lammert, alisema hana nafasi ya kukutana na 
mkuu huyo wa kutoka Mto Nile. Alimlaumu kwa kwenda kinyume na misingi ya
 demokrasia na kuthubutu hata kumtia gerezani Spika wa Bunge 
alilolivunja.
Hata 
hivyo, Rais wa Ujerumani, Joachim Gauk, alimpokea kwa mazungumzo punde 
alipowasili, japokuwa mazungumzo yao yanasemekana yalikuwa ya moto. Gauk
 alimpa mgeni huyo darasa juu ya haki za binadamu na kuheshimu roho za 
wanadamu.
Japokuwa 
Serikali ya Ujerumani hapo kabla ilitoa sharti kwamba Kansela Angela 
Merkel atakuwa tayari tu kukutana na Al-Sisi ikiwa uchaguzi wa Bunge 
utafanywa huko Misri, hata hivyo, hilo halijatimizwa.
Wakati 
ulipowadia, Merkel aliamua ni kwa masilahi ya Ujerumani kukutana na 
mgeni huyo. Misri ina umuhimu wa kijeshi katika eneo lililojaa mizozo, 
ubavuni mwake ikiwapo Libya ambako huko mifumo ya kidola imesambaratika,
 na Syria iliyovurugika kutokana na vita vya kienyeji.
Kansela 
anahisi Misri inaweza kutoa mchango mkubwa katika kupatikana suluhisho 
la Mashariki ya Kati baina ya Israel na Wapalastina.
Katika 
mkutano wao wa pamoja na waandishi wa habari, Merkel alitaja kwamba 
kumekuwako tofauti baina ya misimamo yao. Kwa mfano, Wajerumani 
hawakubaliani na adhabu ya kifo na inataka kuwapo kwa uhuru kwa dini 
zote nchini Misri.
Naye 
Al-Sisi alijinata na kujibu:“ Na sisi tunaishi katika demokrasia na 
uhuru, lakini tunaishi katika wakati mgumu.“ Alisema hatakubali kuiachia
 Misri itumbukie katika vita vya kiraia kama vile Syria, Iraq na Yemen, 
kwa hivyo ataendelea kupambana na wapinzani wake kwa nguvu zake zote.
No comments:
Post a Comment