Kamara achukua kijiji Yanga
Baadhi ya
mashabiki waliofika kwenye mazoezi ya Yanga Uwanja wa Karume jana
wakimshangilia kiungo mpya wa timu raia wa Sierra Leone, Lansana Kamara.
KOCHA wa
Yanga, Hans Pluijm, amevutiwa na ufiti wa mwili wa kiungo aliyeko kwenye
majaribio, Msierra Leone Lansana Kamara, ingawa amesisitiza kwamba
amebakiza hatua moja tu afuzu.
Lakini mchezaji huyo kwenye mazoezi ya jana Jumatano amefanya jambo ambalo mashabiki walilazimika kumzuia na kumjaza noti.
Kamara
ambaye alianza mazoezi juzi Jumanne kwenye Uwanja wa Karume, ameteka
akili za mashabiki wa Yanga kutokana na jitihada zake ambazo wamedai
zimewazidi wachezaji wote ambao wapo mazoezini kwa sasa.
Katika
mazoezi ya jana, mchezaji huyo alichukua kijiji baada ya kuwazidi kete
wenzake kwenye mazoezi mengi kuanzia ya mbio, kupiga mashuti, mazoezi ya
viungo mpaka pushapu. Pia alikusanya kijiji cha mashabiki mazoezini.(P.T)
Mwanaspoti
lilishuhudia baadhi ya wachezaji maarufu wa Yanga wakimwambia apunguze
mbio wakati wa mazoezi kwani alikuwa akiwaburuza jambo ambalo lingeweza
kuwagombanisha na kocha kwa kudhani kwamba wanatega.
Ndipo mchezaji huyo akawa anafanya mdogomdogo ingawa bado alikuwa akiwaburuza na kufanya wengi wao waonekane hawako fiti.
Pluijm
alivutiwa na jitihada za mchezaji huyo na kusisitiza kwamba mazoezini
ameridhika naye lakini hawezi kufanya uamuzi wa mwisho mpaka ampe mechi
moja kwani wachezaji walioko mazoezini Yanga kwa sasa ni wachache.
Mchezaji
huyo amefanya uamuzi mgumu kwa taifa lake kwa kugoma kujiunga na timu ya
taifa aliyoitwa kujiandaa na mechi dhidi ya Guinea ili amalizane kwanza
na Yanga.
“Nimezungumza
na kocha amenikubalia nimemwambia kama kutakuwa na mchezo mwingine
nitajiunga na timu, lakini kwa sasa sitaweza kujiunga nao,” alisema.
Wachezaji
ambao wameanza mazoezi Yanga ni mabeki Rajab Zahir, Pato Ngonyani,
Kelvin Yondani, kipa Benedicto Tinocco, viungo Geofrey Mwashiuya, Said
Makapu, Kamara na mshambuliaji Hussein Javu.
“Huwezi
kupata kipimo kizuri hapa katika mazoezi, nafikiri tunatakiwa kuwa na
subira kwanza nataka kumpa mechi moja ili nijue undani wa uwezo wake
ndani ya kiwanja,”alisema Pluijm.
AJAZWA NOTI
Wakati
Yanga wakimaliza mazoezi yao ya jana asubuhi kiliibuka kihoja kimoja kwa
mashabiki wa timu hiyo ambao walilazimika kumzunguka kiungo huyo na
kuanza kumchangishia fedha za kula bata baada ya kuridhishwa na kazi
yake.
Mashabiki hao ambao walimshtua kiungo huyo
walilazimika
kuchukua mfuko wa plastiki wa kuhifadhia maji ya kunywa na kuanza
kujichangisha fedha ambapo kila kiungo huyo alipotaka kuondoka walimzuia
wakitaka asubiri fedha hizo.
Baada ya
kumaliza zoezi hilo mashabiki hao waliendelea kumsindikiza Kamara mpaka
katika gari ndogo ya meneja wake Gibby Kalule alilolitumia kuondoka
katika eneo hilo.
“Sikuwa
nawaelewa kwanini wamenipa fedha huku pia wakinizuia kuondoka,
nimefurahi sana kuona hili walilofanya watu wa hapa wanapenda sana
mpira,”alisema Kamara.
SIMBA WASHTUKA
Katika
mazoezi hayo ya Yanga, mashabiki wa Simba waliohudhuria walionekana
kushtushwa na umbo la kipa Tinocco ambaye ni mrefu kuliko wachezaji wote
wa Yanga na Simba.
Mashabiki
hao wa Msimbazi walisikika wakidai kwamba kipa huyo huenda akaibua
changamoto kubwa kwa makipa nchini na akawa bora kuliko hata waliopo
sasa licha ya kwamba ni kijana.
Lakini
habari za ndani ya Yanga ni kwamba mchezaji huyo ngongoti bado
hajalivutia benchi la ufundi na linafikiria kumpa muda zaidi licha ya
kwamba umbo lake linawachengua mpaka mashabiki wao ambao wamekuwa
wakikejeli kwamba ni mrefu kuliko lango lenyewe.
Chanzo:Mwanspoti mtandaoni
No comments:
Post a Comment