TIFFAN ENT

TIFFAN ENT

TUKO WANGAPI

TUKO WANGAPI

GLORY FREIGHT

GLORY FREIGHT

Wednesday, June 3, 2015

Bilal, Magufuli waibukia Dodoma 

Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli.
Waziri wa ujenzi, DK John Magufuli
WANACHAMA watatu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) leo wanatarajiwa kuchukua fomu, kuomba ridhaa ya uteuzi wa kuwania urais wa Tanzania, wakati wakiwa hawajatangaza nia kama ilivyo kwa wengi wao.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Mohammed Gharib Bilal, Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli na Katibu Msaidizi wa Siasa na Ushirikiano wa Kimataifa katika Ofisi Ndogo ya CCM, Dar es Salaam, Amos Robert wanachukua fomu leo mjini hapa.
Watatu hao ambao hawajatangaza nia ya kuwania nafasi hiyo ya juu ya uongozi wa nchi wakipitia CCM, wataungana na mawaziri wakuu wa zamani, Frederick Sumaye, Edward Lowassa na Balozi Ali Karume kuchukua fomu leo.
Sumaye, Lowassa na Karume wote wamekwishatangaza nia ya kumrithi Rais Kikwete, tofauti na Dk Bilal, Magufuli na Robert ambao hawajatangaza popote nia yao.
Kwa mujibu wa Katibu wa Halmshauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC) wa Oganaizesheni, Dk Muhammed Seif Khatib, Robert atakuwa wa kwanza kuchukua fomu leo kuanzia saa nne asubuhi katika Makao Makuu ya CCM.
Dk Khatib alisema Katibu Msaidizi huyo atafuatiwa na Sumaye saa 5:30 asubuhi, Dk Bilal atafuata saa saba kamili, Balozi Karume saa 8:30 mchana, Lowassa ambaye aliahirisha jana atafuata saa 9:30 alasiri na Magufuli atafunga dimba kwa leo atakapochukua saa 10:30 jioni.
Lowassa aliahirisha kuchukua jana baada ya kuelezwa kuwa ilitokana na kushiriki kuaga mwili wa aliyekuwa Mbunge wa Ukonga, marehemu Eugen Mwaiposa, ambaye aliwahi kuwa Mjumbe wa Kamati yake ya Mambo ya Nje ya Bunge la Tanzania.
Aliagwa bungeni. Dk Bilal alikuwa mmoja wa wanaCCM waliowania urais wa Zanzibar mwaka 2010 na alishindwa na Rais Dk Ali Mohammed Shein katika uteuzi wa CCM.
Rais Kikwete baadaye alimpendekeza kuwa Mgombea Mwenza na aliposhinda awamu yake hiyo ya pili kuiongoza nchini, akawa Makamu wa Rais.
Dk Magufuli amekuwa akitajwa kuwa mmoja wa wanaCCM wanaofaa kwa urais wa Tanzania, na hajawahi kutangaza nia yake, ingawa vyombo vya habari vimekuwa vikimtaja kuwa miongoni mwa wanaofikiria nafasi hiyo.
Awali jana, wagombea wanne waliokwisha kutangaza nia, walifungua pazi la uchukuaji fomu za uteuzi wa CCM ambazo zitatolewa hadi Julai 2, mwaka huu.
Wa kwanza aliyekabidhiwa fomu na Dk Khatib alikuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalumu), Profesa Mark Mwandosya akifuatiwa na Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wassira, Balozi wa Umoja wa Afrika (AU) Marekani, Amina Salum Ali na Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki, Charles Makongoro Nyerere.
Profesa Mwandosya akifuatana na mkewe Lucy, aliwaambia waandishi wa habari kuwa baada ya kushika nafasi ya tatu nyuma ya Rais Kikwete na Dk Salim Ahmed Salim mwaka 2005, anaamini sasa zamu ni yake.
“Uamuzi wa kuchukua fomu ni uamuzi mzito sana, inabidi ujiandae kisaikolojia kwa maana ya kiakili, kiafya, kimaono, dhamira na dhima. Lakini kubwa zaidi huwezi kuwa na kiburi kama hutokani na wananchi wenyewe au huwawakilishi, kwa hiyo ni dhima kubwa,” alisema.
Profesa Mwandosya aliongeza, “Chimwaga nilikuwa wa tatu, huko sio kushindwa. Nikasema nimepata shaba si haba, sasa yule wa pili hayupo, kwa hiyo, naamini ni wakati wa kupata dhahabu.
Ofisi yangu sasa iko ghorofa ya chini, ninachoomba ni kupanda ngazi.” Kwa upande wake, Wassira naye akifuatana na mkewe, alisema uzoefu wa muda mrefu serikalini pamoja na uchapakazi na uadilifu wake, ni miongoni mwa sababu zinazomfanya aombe ridhaa ya uteuzi huo.
“Kwa hiyo, naomba nianze safari, siyo safari kama ile nyingine, hii ni safari ya uhakika ya kutafuta fursa, kwa nia, kwa uwezo, na sababu ninao uzoefu, hili sio jambo la bahati mbaya.
Nimeandaliwa na niko tayari,” alisema. Balozi Amina akifuatana na waliowahi kuwa viongozi wenzake wa Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT), Anna Abdallah na Halima Mamuya, alisema atajenga uchumi imara wa kuiwezesha Tanzania ijitegemee.
Alisema chini ya kaulimbiu yake ya ‘Matumaini Mapya kwa Kizazi Kipya,’ atazingatia mambo makuu matatu ambayo ni kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi kwa kupanga upya vipaumbele vya maendeleo kwa kutumia vizuri rasilimali za nchi ili ziwanufaishe wananchi.
Alisema anayo nia thabiti, uwezo na uzoefu wa kutosha kuizusha Tanzania kutoka ilipo sasa, huku akiahidi kuanzisha Mahakama Maalumu ya kushughulikia rushwa kwani alikiri ni rushwa na ufisadi ni tatizo kubwa sasa.
Kuhusu kama Tanzania iko tayari kwa Rais mwanamke, alisema, “takwimu zinaonesha kuwa nusu ya Watanzania ni wanawake, na kwa sababu hiyo, wanao uwezo wa kutoa rais.
Lakini kubwa wanawake ni waadilifu na waaminifu, wanao uwezo wa kupambana na rushwa na ufisadi, na hata katika matukio haya, ni nadra kuwakuta.”
Aliyefunga pazia jana alikuwa Charles Makongoro Nyerere, ambaye ni mtoto wa Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere na sasa Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki.
Makongoro alizungumzia kwa kirefu rushwa ilivyo tatizo sasa ndani ya CCM na kutaka zichukuliwe hatua kukabiliana na tatizo hilo haraka iwezekanavyo.
“Rushwa ikitawala katika chama ni hatari sana, kwani kwa kuwa kina uhusiano na serikali, basi hata huko hali itakuwa mbaya. Rushwa inaleta heshima mbaya.
“Mwenyekiti wetu wa CCM, Rais Kikwete amewaambia waache rushwa, lakini hawaachi. Rais wetu siyo dhaifu, ila mstaarabu na mwenye huruma, lakini wanamuangusha sana.
Nasema turudishieni chama chetu,” alisema. Makongoro aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa zamani wa Mkoa wa Mara, alifuatana na wazee tisa kutoka Zanzibar, na kueleza kuwa mdhamini wake wa kwanza Zanzibar atakuwa Rais wa Awamu ya Tano, Salmin Amour Juma maarufu kwa jina la Komandoo.
Baada ya kukabidhiwa fomu hizo, wagombea hao walianza kusaka saini za wadhamini 450 katika mikoa ya 15 ya Tanzania Bara na mikoa mitatu ya Tanzania Zanzibar, ikiwamo ya Unguja na Pemba.
Wakati huo huo, Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja atatangaza nia ya kugombea urais katika ukumbi wa Benki Kuu (BoT) mjini Mwanza leo.CHANZO: HABARI LEO

No comments:

Post a Comment