TIFFAN ENT

TIFFAN ENT

TUKO WANGAPI

TUKO WANGAPI

GLORY FREIGHT

GLORY FREIGHT

Tuesday, March 24, 2015

Zitto aingia na wanachama 12 ACT 

Aliyekuwa Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe jana alitaja sababu tano za kujiunga na chama cha ACT-Tanzania huku akijigamba kuwa yeye ni mchapakazi asiyeyumbishwa.
Akinukuu maneno ya Rais wa zamani wa Ghana, Hayati Kwame Nkrumah aliyewahi kusema, 'forward forever, backward never', Zitto alisema huu ni wakati wa kuangalia mbele badala ya kurudi nyuma.
"Mimi ni mchapakazi, siangalii nyuma tena, naangalia mbele. Mapambano yanaanza matokeo mtayaona baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba,"alisema Zitto.
Ikiwa ni siku moja tu baada ya kukabidhiwa kadi ya ACT, Zitto ambaye aling'atuka kutoka kwenye nafasi ya Ubunge Ijumaa iliyopita, aliweka wazi kuwa alijiunga na ACT Machi 20 na kukabidhiwa kadi katika Tawi la Tegeta, Dar es Salaam.
"Hii ilikuwa siku muhimu katika maisha yangu ya kisiasa," alisema Zitto na kuongeza kuwa amelipa ada ya uanachama hadi mwaka 2025.
Kauli hiyo ilithibitishwa na Mwenyekiti wa ACT, Lugano Mwaikenda ambaye alisema Zitto alijiunga na chama hicho na kupewa kadi namba 7184.
Zitto ambaye pia alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), alizisifu sera za chama hicho. "Nimejiunga na ACT kwa sababu huku ndiko kunaendana na kile ambacho mimi nimekipigania kwa miaka yote tangu nianze siasa ya kuweka masilahi ya Taifa mbele," alisema Zitto.
Alisema sababu nyingine ni kutokana na ACT kuwa chama pekee nchini kinachokubaliana na itikadi ya ujamaa na kinaamini katika falsafa ya Mwalimu Julius Nyerere.
Alisema misingi mikuu ya chama hicho ni pamoja na uwajibikaji na uwazi aliyosema ni muhimu kwa mustakabali wa nchi.
"Hakuna namna nchi yetu inaweza kupiga hatua ya kimaendeleo bila sisi sote kufanya kazi kwa bidii na kwa kuzingatia umakini na weledi," alisema Zitto.
Wanachama wengine 13 wapokewa
Ujio wa Zitto ndani ya ATC ni kama umefungua njia kwa watu wengine kujiunga na chama hicho. Jana wanachama wengine 13 walijiunga akiwamo mwanamuziki wa kizazi kipya, Selemani Msindi maarufu kama Afande Sele.Katibu Mkuu wa chama hicho, Samson Mwigamba alisema: "Tunaamini kutokana na nia thabiti ya chama hiki chenye misingi ya kutaka kuleta maendeleo kwa nchi, ndiyo umekuwa chachu ya wanachama kujiunga nasi," alisema Mwigamba.
Mmoja wa wanachama hao wapya, Dickson Ng'ili alisema mbali na kuvutiwa na itikadi za chama chake kipya, hakufurahishwa na hatua iliyochukuliwa na Chadema dhidi ya Zitto.
Msanii Msindi ambaye alikuwa mwanachama wa Chadema, aliunga mkono kauli ya Ng'ili akisema kuwa Chadema hawakufanya uamuzi wa busara wa kumfukuza Zitto.
Wanachama wengine wapya ni pamoja na Askofu Gerald Mpango, aliyekuwa, Jaji mstaafu Musa Kwikima na aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Tabora, Kansa Mbarouk.
Wengine ni Jorum Mbogo, Meck Mzirai, Charles Lubala na Albert Msando ambaye alikuwa wakili wa Zitto katika kesi yake dhidi ya Chadema.

No comments:

Post a Comment