TIFFAN ENT

TIFFAN ENT

TUKO WANGAPI

TUKO WANGAPI

GLORY FREIGHT

GLORY FREIGHT

Tuesday, March 24, 2015

TAARIFA KUHUSU MVUA ZINAZOENDELEA KUNYESHA JIJINI DAR ES SALAAM

unnamed
Kamishina wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es salaam Suleiman Kova akitoa taarifa ya hali ya ulinzi na usalama katika jiji la Dar es salaam na vifo vya watu 7 waliopoteza maisha kutokana na mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha katika jiji la Dar es salaam.
Aidha, kuhusu mvua zinzoendelea kunyesha katika jiji la Dar es salaam na kusababisha madhara, Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Saidi Meck Sadiki amewataka wananchi kuzingatia agizo la kuhama mabondeni na maeneo mengine hatarishi ili waepuka maafa kufuatia watu 7 kupoteza maisha kutokana na kutokana na athari za mvua zinazoendelea kunyesha.
Akifafanua kuhusu matukio hayo Mhe. Sadiki amesema maeneo yaliyokumbwa na mafuriko hayo na kupata maafa hayo ni bonde la Mto Msimbazi na eneo la Buguruni kwa Myamani.
Amesema kuwa maeneo yaliyokumbwa na mafuriko hayo yameonekana kuwa na wingi wa takataka ngumu na wingi wa mifuko ya plastiki iliyotupwa na wakazi hao hali iliyochangia kuziba mifereji inayopeleka maji katika bonde la mto Msimbazi na maji hayo kuhamia kwenye makazi ya watu.
Ameeleza kuwa kazi ya uokoaji , kumwaga dawa kwenye maji yaliyotuama ili kuzuia athari ya magonjwa ya milipuko, kuzibua mifereji na kukusanya taka katika maeneo hayo inaendelea ili kuruhusu maji kupita kwa urahisi na kuwataka wakazi hao kuepuka kutupa taka ngumu zinazoziba mifereji ya maji.
Amesema Serikali inasubiri taarifa kutoka kwa viongozi wa Serikali za Mitaa kwa maeneo ambayo wakazi wake wanaishi kihalali ili waweze kupatiwa misaada ya kibinadamu.
Kwa upande wake Kamishina wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es salaam Suleiman Kova amethibitisha vifo vya watu hao 7 waliopoteza maisha kutokana na maeneo yao kukumbwa na mafuriko pamoja na athari ya Umeme.
Akitoa ufafanuzi wa vifo hivyo amesema kuwa watu 5 wamepoteza maisha kwa kusombwa na maji na wengine 2 wamepoteza maisha kutokana na ajali iliyosababishwa na Lori moja kugonga Transfoma ya umeme eneo la Buguruni Mnyamani.
Kamishna Kova amesema tayari Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji na Shirika la Ugavi wa Umeme (TANESCO) wameunda kikosi kazi cha uokoaji.
Ametoa wito kwa madereva wa magari ya mizigo, mgari binafsi na yale ya abiria kuepuka kupita katika maeneo yaliyojaa maji ili kuepuka ajali na vifo vinavyoweza kuzuilika.

No comments:

Post a Comment