Wabunge wavurugana Mahakama ya Kadhi..
Waziri mkuu Mizengo Peter Pinda
BAADA ya
kutokea kutoelewana miongoni mwa wabunge juu ya marekebisho ya muswada
wa sheria inayoruhusu kuundwa kwa Mahakama ya Kadhi, Waziri Mkuu Mizengo
Pinda amesema kuna haja ya Serikali kutafakari upya kuhusu suala hilo
kabla ya kuliwasilisha bungeni.
Akifunga
semina ya Wabunge kuhusu muswada huo mjini hapo, Pinda alisema baada ya
majadiliano makali ya wabunge na mgawanyiko uliojitokeza miongoni mwa
wabunge, alisema wamebaini kuwa Waislamu wenyewe hawana msimamo mmoja
kuhusu jambo hilo.
Alisema
ni jukumu la Serikali kuhakikisha kuwa watakachokiandaa juu ya muswada
huo, kinakubalika na Waislamu wote juu ya uanzishwaji wa mahakama hiyo.
Pinda
alisema jambo hilo pamoja na nia yake kuwa njema, Waislamu hawajalielewa
na Wakristo nao wana wasiwasi mkubwa hali inayowafanya Serikali kwenda
kuliangalia upya.
“Zipo
fikra kwamba hata hiki tulichojaribu kufanya hapa wa kuleta muswada huu,
sio chenyewe na hatujawafikisha sehemu wanapotaka Waislamu wenyewe na
kwamba tulichofanya ni kama kilemba cha ukoka,” alisema Pinda.
Alisema
kile ambacho kilipelekwa na serikali bungeni kilitokana na ule mjadala
ulioibuka kwenye Bunge Maalumu la Katiba kuhusu kuanzishwa kwa Mahakama
ya Kadhi na hatimaye kwenye Kamati ya Maridhiano.
Eneo
lingine ambalo Waziri Mkuu alisema linafanya Serikali ikalitazame upya
suala hilo ni kwamba baadhi ya wabunge wameonesha wasiwasi kuwa kuna
ujanja ujanja mwingine nyuma yake kwenye sheria hiyo ambao unahusisha
watu kukatwa mikono, hivyo kuibua hofu kwa watu wa imani nyingine.
Nusura
warushiane makonde Awali wabunge wakati wanachangia kuhusu muswada huo,
walitofautiana kwa kiasi kikubwa hali ambayo ilisababisha almanusura
warushiane makonde huku wengine wakiishia kunyosheana vidole, kuzomeana
na kupeana mipasho.
Hali
hiyo, ilijitokeza baada ya Mbunge wa Kisarawe Seleman Jafo, kutoa maoni
yanayotofautiana na wabunge wote walioanza kuchangia ambapo kwa upande
wake, alitaka muswada huo uwasilishwe bungeni na maeneo yanayohitaji
marekebisho, yarekebishwe.
Wakati
akichangia maoni yake hayo, hali ya hewa ilibadilika katika kikao hicho,
ambapo wabunge walianza kumzomea na ndipo alipokatisha hoja yake na
kuwataka Waislamu wote wabunge wakutane nje baada ya kikao.
Kauli
hiyo ilizua mtafaruku na kikao hicho kilisimama kwa muda kurushiana
maneno na kuishia kunyosheana vidole hali iliyosababisha polisi wa
Usalama kuingia ukumbini humo kwa ajili ya kusimamia amani.
Vurugu
hizo zilizosababisha kikao hicho kusimama kwa muda, zilidumu kwa
takribani dakika 20 huku Mbunge wa Kasulu Mjini Moses Machali
(NCCR-Mageuzi) na Mbunge wa Nyamagana Hezekiah Wenje (Chadema),
wakisimama na kutaka kurusha ngumi kwa wapinzani wao ambao ni Jafo.
Sakata
hilo, lilitatuliwa na Spika wa Bunge, Anne Makinda, aliyewataka wabunge
waheshimiane na kujenga utamaduni wa kuvumiliana hata pale mbunge
mwingine akitoa hoja isiyopendwa na kusubiri muda wao na wao wajenge
hoja.
“Wabunge
nawaambieni utani wenu ni mauti yetu sisi, kuna wabunge hapa
wanafahamika kwa fujo, Machali na mwenzie Wenje, waacheni wenzenu
wazungumze kwanza hoja zao hata kama hamzipendi, kama mtu uvumilivu
umemshinda atoke nje,” alisema Makinda.
Awali
akizungumza katika semina hiyo, Waziri Mkuu Mizengo Pinda, alifanunua
kuhusu ukweli juu ya kuanzishwa kwa Mahakama hiyo ya Kadhi, ambapo
alibainisha kuwa mahakama hizo hazianzishwi na Serikali bali Waislamu
wenyewe na tayari zimeshaanzishwa nchini tangu mwaka 2012.
Alikanusha madai ya baadhi ya watu kuwa Serikali ina mpango wa kuingiza Mahakama hiyo kwenye Katiba.
“Hili
halina ukweli na niweke wazi tu kuwa uwezekano wa Mahakama hii kuingia
kwenye Katiba haupo, nimekutana na wadau mbalimbali wakiwemo maaskofu na
mashehe na nimewafafanulia vizuri tu,” Naye Mtoa Mada katika semina
hiyo Jaji wa Mahakama Kuu Dk Robert Makaramba, alisema Tanzania ni moja
ya nchi zinazojiendesha bila kufungamana na dini yoyote lakini imekuwa
ikisimamia na kulinda haki za waumini wa dini yoyote na kwamba kutungwa
kwa Sheria hiyo ni sehemu ya usimamizi wa Serikali kwa Waislamu.
Akifafanua
kuhusu muswada huo wa Sheria ya Kiislamu, Mwanasheria Mkuu wa Serikali,
George Masaju, alisema muswada huo una vifungu vinne na lengo lake ni
kutatua migogoro ya masuala yanayohusu ndoa, mirathi, talaka na wakfu.
Alisema
kwa mujibu wa Sheria hiyo, Mufti ndiye atakayechagua makadhi mbalimbali
na kutunga kanuni za sheria hiyo, zitakazotumika kusimamia na kuendeshea
mashauri mbalimbali katika Mahakama hiyo ya Kadhi. CHANZO: HABARI LEO
No comments:
Post a Comment