NIMR yatengeneza dawa ya Ukimwi
Dk Mwele Malecela
TAASISI
ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), imetengeneza dawa za
asili zilizoboreshwa kwa ajili ya tiba kwa magonjwa mbalimbali, ikiwemo
Ukimwi baada ya kuzifanyia utafiti kubaini uwezo na usalama wake.
Mkurugenzi
Mkuu wa Taasisi hiyo, Dk Mwele Malecela amesema iko katika hatua za
mwisho za kukamilisha usajili wa dawa asilia 11 ziingizwe sokoni.
Magonjwa
mengine ambayo dawa hizo zilizoboreshwa zitatumika kwa ajili ya tiba ni
kisukari na kupunguza mafuta (lehemu) mwilini, uvimbe wa tezi dume kwa
wanaume na dawa inayoongeza nguvu za kijinsia kwa wanaume.
Dk Mwele
alisema hayo jijini Dar es Salaam jana, wakati akizungumza na waandishi
wa habari kuhusu miaka 35 ya utafiti na maendeleo ya afya na kusema
tafiti katika tiba asilia zilifanyika kubaini uwezo na usalama wa dawa
hizo zinazotumiwa na jamii mbalimbali hapa nchini.
“Aidha
taasisi imefanya utafiti kwa kuzingatia uwezo na usalama kwa watumiaji
na kufanikiwa kutengeneza dawa asili zilizoboreshwa kwa ajili ya tiba
kwa magonjwa ya malaria, Ukimwi na magonjwa nyemelezi, ugonjwa wa ini,
shinikizo la damu…,” alisema.
Alisisitiza, “taasisi iko katika hatua za mwisho za kukamilisha usajili wa dawa asilia 11 ili ziweze kuingizwa sokoni.”
Akizungumzia
tatizo la kupungua kwa nguvu za kiume, alisema linaonekana ni kubwa na
hata katika maonesho wanayofanya, dawa inayoimarisha nguvu hizo
hununuliwa zaidi.
Aidha
alisema iko haja kwa wadau na serikali kuwekeza nguvu zaidi katika
taasisi hiyo kufanya tafiti zitakazosaidia kugundua chanzo na tiba ya
tatizo la uvimbe kwa matumbo ya uzazi ya wanawake wengi wenye asili ya
kiafrika.
Kuhusu
ugonjwa wa malaria, Dk Mwele alisema matokeo ya tafiti yanaonesha
kupungua maeneo ya Kaskazini, Kaskazini-Mashariki, Kanda ya Kati na
Kanda ya Ziwa Victoria kutokana na kuongezeka kwa matumizi ya vyandarua
na uelewa wa wananchi juu ya utunzaji wa mazingira.
Alisema utafiti wa chanjo ya malaria uliofanywa katika wilaya za Bagamoyo na Korogwe umeonesha uwezo mkubwa wa kinga kwa watoto.
Alisema
taasisi inaendelea kushirikiana na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii,
Kupitia Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Malaria kufuatilia na kutathmini
usugu wa mbu dhidi ya viuatilifu vinavyotumika katika vyandarua na
katika kunyunyizia ukoko kwenye nyumba.
Alisema
taasisi imeendelea kuishauri Serikali katika kuainisha mbinu sahihi za
kupambana na usugu huo ambapo pia matokeo ya tathmini za ubora wa dawa
za tiba ya malaria yameonesha kuwa dawa mseto ya ALU bado inao uwezo
mkubwa wa kutibu ugonjwa wa malaria.CHANZO:HABARI LEO
No comments:
Post a Comment