Mwendesha mashitaka auawa Uganda
Askari akikagua gari ambalo lilikuwa likiendeshwa na Joan Kagezi
Watu wenye silaha wamemuua mwendesha
mashitaka mkuu katika kesi ya watuhumiwa wa Kiislam wanaotuhumiwa kuua
watu kadha katika mashambulio ya bomu mwaka 2010.Mwendesha mashitaka huyo Joan Kagezi ambaye alikuwa kaimu mkurugenzi mwendesha mashitaka msaidizi nchini Uganda ameuawa kwa kupigwa risasi na watu waliokuwa katika pikipiki wakati akiendesha gari kurudi nyumbani mjini Kampala.
Kesi inayoendelea inawahusu watu kumi na watatu wanaotuhumiwa kuwa wapiganaji wa kikundi cha al-Shabaab.
Wanatuhumiwa kuua watu zaidi ya sabini wakati wakiangalia Fainali za Kombe la Dunia za mwaka 2010 katika mgahawa mmoja na katika uwanja wa klabu ya rugby.
Wiki iliyopita Marekani ilisema ilipata "habari za kuwepo uwezekano wa shambulio" katika maeneo ya mji ambayo raia wa mataifa ya magharibi wanakutana.
Serikali ya Uganda imesema Marekani ilionya juu ya uwezekano wa kuwepo kwa mtu anayejitoa mhanga akijaribu kuingia nchini humo.
Msemaji wa serikali amesema Uganda ilikuwa katika kitisho kwa sababu imechangia askari wengi katika jeshi la Umoja wa Afrika linalolinda amani nchini Somalia wakipambana na kundi la al-Shabab ndani ya Somalia.(BBC)
No comments:
Post a Comment