Lowassa akubali yaishe Urais CCM
Aliyekuwa waziri mkuu Edwad Lowasa
SIKU moja
baada ya Chama cha Mapinduzi (CCM), kumuonya aliyekuwa Waziri Mkuu
Edward Lowassa, kwa tuhuma za kukiuka Katiba na kuanza kampeni za Urais
kabla ya muda, kiongozi huyo ameibuka na kudai kuwa hana njia ya
kuwazuia watu wasimuombe agombee Urais.
Pia
Lowassa ametumia nafasi hiyo na kuwaomba wale wote ambao bado wana nia
ya kumshawishi agombee nafasi hiyo ya urais, wasubiri kwanza hadi pale
chama chake hicho kitakapotoa maelekezo.
Akizungumza
na vijana 60 wa bodaboda kutoka wilaya ya Mbarali, Mbeya waliokwenda
pia kumshawishi agombee nafasi hiyo, mjini Dodoma jana, alisema si vyema
kwa maofisa wa chama kuzungumzia masuala ya wanachama wao kwenye vyombo
vya habari wakati kuna vikao vya chama.
Alisema
watu waliojitokeza na kumshawishi kuchukua fomu za kuwania nafasi hiyo
ya Urais, hajawaita wala kuwalipa chochote kama inavyodaiwa na kwamba
walikuwa wakifuata maneno ya Rais Jakaya Kikwete aliyoyatoa mkoani
Ruvuma katika sherehe za maadhimisho ya miaka 38 ya Uhuru.
Alisema
katika siku hiyo, Rais Kikwete aliwataka watanzania wawashawishi
viongozi wanaoona wanafaa ili wajitokeze kugombea nafasi hiyo ya Urais.
“Mimi ni
vigumu kuzuia mafuriko kwa mikono. Nazuia mafuriko kwa mikono, yanakuja
mimi nayazuia kwa mikono, nitaweza kweli? Hawa watu sina hoja nao, sina
cha kuwaambia,” alisema Lowasa.
Alisema
tangu makundi hayo yaanze kujitokeza kumshawishi kuchukua fomu mambo
mengi ya ajabu yamesemwa jambo ambalo linamsikitisha na kumshangaza kwa
kuwa endapo kuna mtu wa chama mwenye hoja, ni vyema kuwasilisha kwenye
vikao vya chama badala ya kuzungumza hadharani na kwenye vyombo vya
habari.
Alisema
mambo ya chama humalizwa kwenye vikao vya chama, ambapo majadiliano
hufanyika na mwisho wa siku watu huelewana na kamwe mambo yanayohusu
chama yahawezi kuzungumziwa kwenye vyombo vya habari., televisheni na
redio jambo ambalo ni hatari sana.
“Niseme
mawili tu yanayonisikitisha, wanasema mnakuja nimewaiteni ninawapa
fedha, hela za kuwapa ninazitoa wapi? Mkija hapa nikiwawekea maturubai
ni kosa, mkiwa na viti ni makosa na wanasema nawapikieni chakula, mambo
ya ajabu sana,” alisema.
Alisema
juzi vijana takribani 300 walimtembelea nyumbani kwake, na kushangaa ni
namna ipi angeweza kuwapikia chakula vijana wote hao.
“Ni
vibaya sana kumdhalilisha mwenzako kwamba maisha yake yote akili yake ni
kufikiria tumbo, huyu hana cha kufikiria isipokuwa tumbo, kwa hiyo
mnakuja hapa kwa sababu mnataka Lowasa awape chakula, ni kudhalilisha
watu,” Alisema watu waliomtembelea walikwenda kwa utashi wao wenyewe,
kwa gharama zao.
“Sijawaona,
sijawatuma, ama mmeniona huko? Nimekuja kuwashawishi? Nimewahi kuja
huko Mbarali kuwashawishi mje kwangu? Au nimewapeni hela leo mlipokuja
hapa, hata soda zenyewe hamjanywa.”
Aliwataka
wale ambao wanapanga kumshawishi waache kwanza hadi wapate maelekezo ya
chama ili kuepusha migogoro kwenye chama hicho.
“Nina
uhakika tutapata nafasi, jambo moja ninataka kuwapa matumaini ipo siku
watanzania watapata uhuru wa kusema juu ya mtu mimi, iko siku watapiga
kura zao kusema kwa hiyo tungojee hiyo siku. Nina uhakika wapo
watanzania wengi wanaonipenda kama walivyosema kwa kazi zangu, watapata
nafasi ya kusema naam ama hapana, kwa hiyo huyo anayepiga kelele nyingi
sijui nitoke chama sijui nifanye kitu gani angoje wanaCCM na watanzania
waamue,” alisisitiza.
Alisema
kitendo cha kufuatwa na makundi mbalimbali ya watanzania kumshawishi
kuwania nafasi ya Urais, kinatokana na ukweli kuwa anaaminika na
kupendwa kutokana na mambo mengi aliyoyafanya.
Kwa
takribani wiki nzima sasa, Lowasa amekua akipokea makundi mbalimbali ya
watu wakiwemo wazee wa CCM, mashehe kutoka Bagamoyo, wanafunzi wa Chuo
Kikuu cha Dodoma (UDOM) na jana waendesha bodaboda kutoka Mbarali
wakimtaka achukue fomu kuwania urais.
Hata
hivyo kutokana hayo, juzi Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, Itikadi na
Uenezi Nape Nnauye, alisema vitendo hivyo vya kupokea makundi hayo ni
ukiukwaji wa Katiba na chama hicho kwa kuwa kinachofanyika ni kampeni za
wazi kabla ya muda kufika.
Wakati
huo huo, Sifa Lubasi anaripoti kutoka Dodoma kuwa Chuo Kikuu cha Dodoma
(UDOM) kimesema baadhi ya wahadhiri na wanachuo wa chuo hicho walikwenda
nyumbani kwa Waziri Mkuu Mstaafu Edward Lowassa kumuomba kwamba wakati
ukifika atangaze nia na kugombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania hawakwenda kama wawakilishi wa chuo bali kwa matakwa yao
binafsi.
Kwa
mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana na Mhadhiri
mwandamizi wa Chuo hicho Profesa Peter Kopoka ilisema baadhi ya
wahadhiri na wanachuo waliokwenda nyumbani kwa Lowasa , Machi 22, mwaka
huu walikwenda kwa matakwa yao binafsi bna si kwa kutumwa na chuo.
“Ukweli
wa tukio hilo ni kwamba, Wahadhiri na Wanachuo waliokwenda nyumbani kwa
Lowasa, walikwenda wao kama watu binafsi na kwa mahusiano yao binafsi na
Lowasa, na wala hawakwenda kama wawakilishi wa chuo” alisema .
“Ni vema umma wa Watanzania ukaelewa kwamba Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) hakikushiriki kwa namna yoyote ile.” Alisema.CHANZO:HABARI LEO
No comments:
Post a Comment