WAZIRI MKUU AONGOZA HARAMBEE
Waziri
Mkuu, Mizengo Pinda akiwa mkewe Tunu wakiwahamasisha waumini wa kanisa
katoliki la Magomeni jijini Dar es salaam kuchangia ukarabati wa kanisa
lao wakati alipohudhuria ibada kwenye kanisa hilo Machi 17, 2013. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri
Mkuu, Mizengo Pinda akizungumza na watoto baada ya kuhudhuria ibada ya
misa kwenye kanisa katoliki la Mgomeni jijini Dar es salaam Machi 17,
2013. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
…………………………………………………………………………..
WAZIRI MKUU Mizengo Pinda ameongoza harambee ya papo kwa papo
na kufanikiwa kukusanya sh. milioni 31.5 zikiwa ni ahadi na fedha
taslimu kwa ajili ya ukarabati wa Kanisa Katoliki la Mashahidi wa Uganda
la Magomeni, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waumini wa Kanisa hilo leo asubuhi (Jumapili,
Machi 17, 2013) kabla ya kuendesha harambee hiyo, Waziri Mkuu aliusifu
uongozi wa Kanisa Katoliki la Magomeni kwa kuamua kufanya upanuzi wa
kanisa hilo ili liweze kuhudumia waumini wengi zaidi.
“Nia yao ni nzuri sana na wameona mbali mapema.
Magomeni hii ya leo si ya wakati ule, na wala haitakuwa hivi katika
miaka mingine 50 ijayo. Zamani usingeweza kuona hata ghorofa moja hapa Magomeni lakini sasa hivi maghorofa hayahesabiki,” alisema.
Aliwasisitiza waumini hao kujitoa kwa ajili ya kazi ya Bwana
kwa sababu hakuna sadaka ambayo ni ndogo. “Hakuna sadaka iliyo ndogo
mbele ya Mungu, kikubwa ni dhamira tu. Kanisa ni letu na litajengwa na
sisi waumini ili mradi kila mmoja wetu aseme Kansa hili nitalijenga,”
alisisitiza.
Mapema akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na waumini hao,
Baba Paroko wa kanisa hilo, Padri Sixfrious Rwechungura alisema wameanza
kazi ya ukarabati tangu Agosti 15, 2011 na kwamba hadi sasa
wamekwishakusanya sh. milioni 350 iliyotokana na nguvu za waumini
wenyewe bila msaada wa kutoka nje.
Alisema wanahitaji kiasi cha sh. milioni 300 ili kukamilisha
kazi hiyo ambayo inapaswa kukamilika katika miaka miwili ijayo ili
iendane na maadhimisho ya miaka 50 ya kanisa hilo.
Katika harambee hiyo, Waziri Mkuu na mkewe Mama Tunu Pinda
waliahidi kuchangia sh. Milioni 10 na kutoa sh. Milioni mbili za
kianzio. Pia aliendesha mnada wa mbuzi aliyenunuliwa kwa sh. 600,000/-
na mkoba ulionunuliwa kwa sh. 150,000/-.
No comments:
Post a Comment