TUME YA KUFELI KIDATO CHA NNE YATAKA USHIRIKIANO
Mwenyekiti
wa Tume ya Taifa ya kuchunguza kushuka kwa kiwango cha ufaulu kwa
wanafunzi wa kidato cha nne mwaka 2012 Prof. Sifuni Mchome
(katikati)akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam
kuhusu kuanza kwa zoezi la ukusanyaji wa maoni kutoka wadau mbalimbali.
Wengine ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) Assah Mwambene
(kushoto) na Bi.Tunu Temu mjumbe wa Sekretarieti ya Tume hiyo.
…………………………………………………………………
Na. Aron Msigwa -MAELEZO, Dar es salaam.
Tume ya Taifa iliyoundwa na Mh.
Waziri mkuu Mizengo Pinda kuchunguza kushuka kwa kiwango cha ufaulu kwa
wanafunzi wa kidato cha nne mwaka 2012 imewaomba watanzania kuipa
ushirikiano kwa kutoa maoni yao ili iweze kukamilisha majukumu iliyopewa
kwa muda na ufanisi mkubwa.
Akizungumza na waandishi wa habari
leo jijini Dar es salaam Mwenyekiti wa Tume hiyo Prof.Sifuni Mchome
ameeleza kuwa tume hiyo ilianza kazi mara baada ya kuzinduliwa na Waziri
mkuu tarehe 2 mwezi Machi mwaka huu na kufafanua kuwa jukumu lililopo
sasa ni kuanza kazi ya kukusanya maoni kutoka kwa watanzania ili kubaini
sababu za matokeo mabaya ya mtihani huo.
Amesema kuwa tume hiyo pamoja na
mambo mengine imepewa jukumu la kutoa mapendekezo ya hatua za kuchukua
ili kukabiliana na tatizo la mwenendo wa kushuka kwa kiwango cha elimu
nchini huku mapendekezo hayo yakizingatia kipindi cha muda mfupi , kati
na kipindi cha muda mrefu.
Prof. Sifuni ameeleza kuwa tume hiyo
inafanya kazi kwa kuzingatia hadidu mbalimbali za rejea zikiwemo
kubainisha sababu za matokeo mabaya ya kidato cha nne 2012, sababu za
kushuka kwa kiwango cha ufaulu, nafasi ya Halmashauri katika kusimamia
elimu ya sekondari katika halmashauri zake.
Rejea nyingine ni pamoja na pamoja
na kuanisha sababu nyingine zinazoweza kuwa zimechangia hali ya matokeo
hayo pamoja na kutoa mapendekezo ya hatua za kuchukua mara moja kwa
wanafunzi 240,903 waliofeli mitihani yao kwa kupata daraja sifuri.
Amefafanua kuwa tume katika
kutekeleza majukumu yake itapitia mitaala na mihutasari ya Elimu ya
Msingi na Sekondari, kutathimini kiwango na mazingira ya ufundishaji na
ufunzaji, kuangalia mfumo wa upimaji na tathmini ya mitihani pia
usimamizi na uendeshaji.
Pia pamoja na mambo mengine tume
itatathmini mchango wa jamii na wazazi/ walezi katika maendeleo ya
wanafunzi, hali ya upatikanaji wa chakula cha mchana, upungufu wa
majengo ya shule,madarasa, maabara na maktaba.
Vilelevile tume hiyo itafuatilia
mwamko wa wazazi katika kufuatilia mkazo wa eliimu kwa watoto na suala
la mmomonyoko wa maadili unaotokana na ukuaji wa utandawazi hususan
teknolojia ya Habari na Mawasiliano na kutathmini athari ya mfumo wa
ufundishaji wa mikondo miwili iliyopo katika shule za Zanzibar.
Aidha mwenyekiti wa Tume hiyo
amebainisha kuwa tume itaanza rasmi kukutana na wadau mbalimbali kwa
lengo la kupata maoni kuanzia tarehe 11 mwezi huu kwa kuanza na mkoa wa
Dar es salaam, Zanzbar na maeneo mengine nchini kwa kukutana na viongozi
wa ngazi mbalimbali za Wizara, Mikoa, Wilaya, Halmashauri, Kata, Shule,
Taasisi mbalimbali za kijamii na wananchi kwa ujumla na pia kuwasilisha
maoni kwenye tume kupitia Mwenyekiti wa Tume, Tume K4-2012, S.L.P 5909
Dar es salaam au kupitia simu 0737206038, Barua pepe:
maoni@tumek4.go.tz au kwa kutembelea Tovuti ya tume ya www.tumek4.go
No comments:
Post a Comment