TIFFAN ENT

TIFFAN ENT

TUKO WANGAPI

TUKO WANGAPI

GLORY FREIGHT

GLORY FREIGHT

Sunday, March 24, 2013

WAKILI MAWALA NYANGA AJIUA KWA KUJITUPA TOKA JUU YA GHOROFA

Imenukuliwa kutoka kwenye gazeti la Mwananchi, ARUSHA-- Giza limeukumba Mkoa wa Arusha baada ya kutokea vifo vya ghafla vya watu maarufu. Jana Wakili Nyaga Mawalla alifariki baada ya kujirusha kutoka ghorofani akiwa jijini Nairobi, Kenya alikokwenda kwa matibabu.

Habari zilizopatikana zinaeleza kuwa Nyaga alikufa baada ya kujirusha kutoka katika jengo la ghorofa ya hospitali aliyokuwa akitibiwa jijini Nairobi usiku wa kuamkia jana.

Mfanyakazi wa Kampuni ya Mawalla Advocate, John Minja aliliambia gazeti hili kuwa mwili wa marehemu ulitarajiwa kurejeshwa nchini jana.

“Hali yake haikuwa mbaya, kwani juzi mchana tulizungumza naye tukitaka kwenda kumsalimia lakini, alitueleza kuwa angerejea jana nchini,”alisema Minja.

Hata hivyo, bado haijajulikana sababu za kujiua, lakini baadhi ya ndugu zake wanasema ni kutokana na msongo wa mawazo.

Taarifa za kifo cha Mawalla anayemiliki kampuni kadhaa ikiwamo Kampuni ya uwakili ya Mawalla Advocates, kimeshtua wengi akiwamo Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe aliyesema taifa limepoteza kijana mwenye maono, akili na mjasiriamali aliyetajirika bila kuiba.

“Nimepokea kwa mshtuko mkubwa taarifa za kifo cha Nyaga. Licha ya udogo wake kiumri, lakini alikuwa mshauri wangu kwenye mambo mengi kiuchumi, kibiashara na kijamii. Nyaga alikuwa kiongozi wa jamii asiye na mipaka katika huduma tofauti na wafanyabiashara wengi nchini walishirikiana naye,” alisema Mbowe.

Mawalla ambaye ni mtoto wa wakili wa kwanza wa kujitegemea nchini, Juma Mawalla alikuwa jijini Nairobi kwa matibabu ya kupungaza sumu mwilini kutokana na madhara ya matumizi ya dawa za shinikizo la damu kwa muda mrefu.

Wakati kifo hicho cha ghafla cha Mawalla kikitokea, Jiji la Arusha pia linaomboleza kifo kingine cha ghafla cha mfanyabiashara maarufu wa madini, Henry Nyiti kilichotokea mkoani Morogoro.

Nyiti ambaye ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Interstate yenye makao yake makuu eneo la Tengeru, wilayani Arumeru alifariki usiku wa kuamkia juzi akiwa Mahenge alikokwenda kwa ajili ya shughuli za uchimbaji madini na anatarajiwa kuzikwa nyumbani kwake eneo la Akheri, Arumeru keshokutwa Jumanne.

Akimzungumzia wakili Mawalla, Mbowe alisema mchango wake kwa maendeleo ya jamii hautasahaulika hasa kutokana na kujitolea kuendeleza taaluma ya uwakili kwa kudhamini tuzo ya wakili kijana kwa kutoa dola 5,000 kila mwaka kumsomesha mshindi wa tuzo hiyo.

Mbowe ambaye mwezi uliopita alipokea hati ya kiwanja chenye thamani ya Sh500 milioni iliyotolewa kwa Taasisi ya Maendeleo Arusha (ArDF) na wakili huyo kwa ajili ya ujenzi wa hospitali ya mama na mtoto, alipendekeza hospitali hiyo iitwe Nyaga Mawalla Memorial Hospital kama njia ya kumuenzi.

Mbunge wa Arusha mjini, Godbless Lema ambaye ndiye mwanzilishi wa taasisi ya ArDF, alimwelezea Mawalla kama kiongozi, tajiri na kijana aliyetumia akili, nguvu na rasilimali zake akishirikiana na viongozi wote bila kujali tofauti zao kiitikadi.

“ArDF tutauenzi na kuuthamini utu uliouonyesha Mawalla kwa kukamilisha ndoto ya kuwa na hospitali ya kisasa ya mama na watoto ili kuokoa maisha ya kundi hilo linapoteza maisha kwa kukosa huduma bora na sahihi,” alisema Lema.

Fred Lowassa, mtoto wa Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa alimwelezea wakili Mawalla kama kijana aliyeonyesha nidhamu tangu akiwa shule na aliendelea nayo hadi kwenye kazi na shughuli za kiuchumi kiasi cha kufanikiwa na kutumia utajiri wake kusaidia jamii. “Kifo hiki ni pigo siyo tu kwa Arusha bali taifa zima la Tanzania.”

Mchango wa Mawalla kwenye kuendeleza sekta ya elimu, hasa sheria umetukuka ndiyo maana alijitolea hata kufundisha bila malipo kwenye vyuo vikuu kadhaa nchini,” alisema Lowassa.

Pamoja na kujitolea kwenye shughuli mbalimbali za kimaendeleo, Mawalla pia alikuwa mfadhili wa watoto kadhaa wenye mahitaji maalumu ambapo hadi mauti yanamkuta, alikuwa akisomesha wanafunzi kadhaa katika ngazi mbalimbali kuanzia elimu ya msingi hadi chuo kikuu.

Nyumbani kwake anaishi na zaidi ya watoto saba ambao amewachukua kutoka sehemu na familia mbalimbali nchini anaowalea, kuwahudumia na kuwasomesha kama watoto wake wa kuwazaa.

Ingawa haikuweza kujulikana haraka kutokana watu walio karibu naye wote kudaiwa kuwa jijini Nairobi, mwili wa wakili huyo unatarajiwa kuletwa nchini kati ya leo na kesho na kupelekwa moja kwa moja katika chumba cha kuhifadhi maiti cha KCMC, mjini Moshi kusubiri maziko yanayotarajiwa kufanyika nyumbani kwao Marangu.


No comments:

Post a Comment