WAIMBAJI WA MUZIKI WA INJILI SOLOMONI MUKUBWA NA NTABOBA WATUA DAR
Mwimbaji wa nyimbo za injili, Solomon Mukubwa akizungumza na
waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo kuhusu maandalizi yake
katika tamasha la Pasaka 2013.
Mwimbaji wa nyimbo za injili, Faraja Ntaboba akiimba kwa
hisia moja ya nyimbo zake mbele ya waandishi wa habari jijini Dar es
Salaam .
Mwenyekiti wa Kamati Maalumu inayoratibu tamasha hilo la kimataifa, Alex Msama akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo kuhusu maandalizi ya tamasha hilo.
DAR ES SALAAM, Tanzania
WAKATI muimbaji Sipho Makhabane wa Afrika Kusini akitarajiwa
kutua Ijumaa, waimbaji wa nyimbo za injili kutoka Kenya na Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Congo (DRC), wamewasili jana jijini Dar es Salaa, tayari
kwa ajili ya kutumbuiza katika Tamasha la Pasaka, litakaloanza Machi 31
kwenye Uwanja wa Taifa jijini.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mwenyekiti wa Kamati
Maalumu inayoratibu tamasha hilo la kimataifa, Alex Msama aliwataja
waimbaji waliowasili jana kuwa ni Solomoni Mukubwa (Kenya) na Faraja
Ntaboba (DRC).
Msama aliwataka wapenzi, mashabiki na wadau wa muziki wa
injili kujitokeza kwa wingi katika tamasha hilo, ambalo mgeni rasmi
atakuwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda, ili kuunga mkono juhudi za kampuni
yake kuandaa tamasha hilo kwa malengo mbalimbali ikiwemo kueneza injili
ya Mungu na kusaidia makundi maalumu.
Kuhusu waimbaji, Msama alisema kuwa hadi kufikia Ijumaa,
wakali wote wa nyimbo za injili kutoka nje watakuwa wamewasili jijini
tayari kwa tukio hilo linalosubiriwa kwa hamu na mashabiki wa Dar es
Salaam na mikoa yote ambayo tamasha huilo litarindima.
Aidha, mkali wa aina hiyo ya muziki kutoka Kenya, Mukubwa,
alisema kuwa amejiandaa vya kutosha katika tamasha la mwaka huu ambalo
limebeba ujumbe wa Upendo na Amani.
“Wakati wa Uchaguzi wa Nchini Kenya tuliimba na kuhamasisha
Amani na Upendo na kwa kupitia tamasha hili tutaimba nyimbo za
kuhamasisha Amani na Upendo hapa Tanzania,” alisema Mukubwa.
Naye mwimbaji kutoka DRC, Ntaboba alisema kuwa, watu
wajitokeze kwa wingi katika tamasha hilo na kupata burudani
itakayokwenda sambamba na mafundisho ya dini.
Msama aliongeza kuwa idadi ya waimbaji imeongezeka baada ya
kujitokeza kwa nyota mwingine aliyemtaja kwa jina moja la Ntutuma kutoka
Kenya, ambapo baada ya tamasha hilo kutikisa kwenye jijini Dar es
Salaam, itakuwa zamu ya Dodoma, Iringa, Mbeya, Mwanza kabla ya
mashambulizi kuhimishwa mkoani Mara.
No comments:
Post a Comment