WATANZANIA WAHIMIZWA KUPIMWA FIGO ZAO
Mwenyekiti wa Taasisi ya Figo Tanzania
Mh. Frederick Werema akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar
es salaam kuhusu umuhimu wa kunywa maji safi na salama kama moja ya njia
za kukinga figo kuathiriwa na magonjwa mbalimbali na kutoa wito kwa
watanzania kuepuka tabia hatarishi kwa afya ya figo zikiwemo za utumiaji
wa pombe kupita kiasi, madawa ya kulevya, utumiaji wa dawa za binadamu
kupita kiasi na uvutaji wa sigara. Picha na Aron - MAELEZO.
--------------------------------------------------------------------------------------------------
Na. Aron Msigwa - Dar es salaam.
Watanzania wametakiwa kujenga tabia
ya kuvitumia vituo vya afya kupima afya ya figo mara kwa mara na kupata
ushauri na tiba mapema pindi wanapogundulika kuwa na matatatizo ya
figo ili kuepuka kusababisha usugu wa ugonjwa huo.
Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dkt. Hussein Mwinyi ametoa kauli hiyo leo jijini wakati akitoa tamko kuhusu maadhimisho ya Siku ya Afya duniani yatakayofanyika tarehe 14 mwezi huu duniani kote.
Amesema wananchi wengi wamekuwa wakichelewa kwenda kwenye vituo vya afya kuchunguza afya ya figo zao kwa wakati ili kujua kama ni wazima au wameathirika ili waweze kupata tiba sahihi ya ugonjwa huo.
Dkt. Mwinyi amesema ugonjwa wa figo unazuilika na kutibika na kuongeza kuwa kinga ya maradhi ya figo huanzia kwenye kaya na vituo vya awali vya utoaji wa huduma za tiba na kuongeza kuwa maradhi haya yanawapata watu wengi hasa baadhi ya vijana na watu ambao wamekua wakipata magonjwa ya kuambukiza kama vile kuhara, Malaria, homa ya Ini, Pepopunda na Ukimwi.
Amesema mwaka huu 2013 Tanzania inaungana na mataifa mengine duniani kuadhimisha siku ya afya ya figo duniani kitaifa katika viwanja vya hospitali ya AICC Arusha kwa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa kushirikiana na Chama cha Taifa cha Afya ya Figo ikitoa elimu kuhusu umuhimu wa katika kudumisha afya ya figo kwa kuongozwa na kauli mbiu isemayo " Afya ya Figo kwa Maisha Bora: Epuka kuharibu Figo"
Amefafanua kuwa lengo kuu la kauli mbiu hiyo ni kuwahimiza wananchi kufahamu umuhimu mkubwa wa kiungo hicho katika mwili wa binadamu.
" Napenda kuwaeleza kuwa kauli mbiu ya mwaka huu inatuhimiza watu wote tufahamu kuwa figo ni kiungo muhimu sana katika maumbile yetu hivyo hatuna budi kutunza viungo hivi katika miili yetu visije kupata madhara yoyote yanayoweza kujitokeza kuviharibu" Amesema Dkt. Mwinyi.
Ameongeza kuwa serikali ya Tanzania inafanya kila linalowezekana kuhakikisha kuwa fedha, vifaa tiba na dawa za kukabiliana na ugonjwa huo zinapatikana ili kuinua na kulinda afya ya jamii.
Katika hatua nyingine Dkt. Mwinyi amesema maadhimisho ya mwaka huu yataambatana na upimaji wa afya ya figo bure na kuongeza kuwa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Taasisi ya Figo Tanzania na Kampuni ya Simu za mkononi ya Tigo Tanzania na Uhuru One kwa pamoja watazindua programu ya kutuma ujumbe mfupi wa simu (sms) wa IJUE AFYA YA FIGO YAKO"
Amesema huduma hiyo itatoa fursa kwa wananchi kupata na kutuma taarifa zinazohusu hali zao za afya ambapo wataweza kupewa maelezo na namna ya kupata huduma katika vituo mbalimbali vya afya kwa kuanza na mkoa wa Dar es salaam, Zanzbar na baadaye kusambaa nchi nzima ili kuwawezesha wananchi kuzifahamu afya zao kupitia simu zao za mkononi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Taasisi ya Taifa ya Figo Tanzania ambaye pia ni Mwanansheria mkuu wa Serikali Frederick Werema amesema kuwa tatizo la ugonjwa wa figo nchini tanzania limekua likiongezeka kutokana na wananchi walio wengi kushindwa kufuata kanuni za afya na kuzingatia lishe bora.
Amesema kuwa ugonjwa wa figo unazuilika endapo watu watajenga tabia ya kuepuka matumizi ya baadhi ya dawa zenye athari kwa mwili wa binadamu, ulevi kupita kiasi, uvutaji wa sigara, kula vyakula visivyofaa ama vyenye sumu na kuzingatia unywaji wa maji safi na salama mara kwa mara.
Naye Katibu wa Taasisi ya Figo Tanzania Dkt. Linda Ezekiel amefafanua kuwa idadi ya wagonjwa wa figo nchini imekua ikiongezeka mwaka hadi mwaka na kufafanua kuwa kati ya wagonjwa 1000 wanaohudhuria kwenye vituo vya afya kwa ajili ya matibabu asilimia 3-9 wanasumbuliwa na matatizo ya figo huku akitoa wito kwa wananchi kupima afya zao mara kwa mara.
No comments:
Post a Comment