TIFFAN ENT

TIFFAN ENT

TUKO WANGAPI

TUKO WANGAPI

GLORY FREIGHT

GLORY FREIGHT

Monday, March 18, 2013

RIPOTI MAALUMU TOKA MAHAKAMA YA KISUTU ALIKOSHITAKIWA LWAKATARE WA CHADEMA


HATIMAYE Mkurugenzi wa Mashitaka nchini, Dk Eliezer Feleshi amemfikisha katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Usalama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Wilfred Lwakatare na mwenzake kwa makosa ya ugaidi.
Mbali na Lwakatare mshitakiwa mwingine ni Ludovick Rwezaula Joseph ambao wanatetewa na mawakili wa kujitetemea Profesa Abdallah Safari, Tundu Lissu na Nyaronyo Kicheere.
Washitakiwa hao wakifikishwa jana saa mbili asubuhi mahakamani hapo chini ya ulinzi mkali wa askari kanzu walikuwa wakiongozwa na Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Ilala, Duwani Nyanda na kuifadhiwa nyuma ya jengo la mahakama hiyo tayari kwaajili ya kufikishwa kizimbani kosomewa mashitaka yanayowakabili.
Washitakiwa hao waliingizwa ndani ya ukumbi namba moja wa mahakama hiyo saa 7:06 mchana chini ya ulinzi mkali wa wanausalama , huku Lwakatare akiwasalimu wafuasi wa Chadema, kwa kuwaonyesha ishara ya vidole viwili ambapo wafuasi hao walikuokuwa wamefurika mahakamani hapo tangia asubuhi jana wakimjibu kwa kumuonyeshea ishara ya
vidole viwili juu.
Baada ya kupanda kizimbani, jopo la mawaikili wakuu wa seriakali linaloongozwa na Mwanasheria Kiongozi wa Serikali Kanda ya Dar es Salaam, Ponsian Lukosi, Purdence Rweyongeza na Peter Mahugo  ambapo walidai hati ya mashitaka ina jumla ya makosa manne.
Wakili Rweyongeza alililata kosa la kwanza ambalo linawakabili washitakiwa wote kuwa ni la kula njama kutenda kosa la jinai kinyume na kifungu cha 284  cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu ya mwaka 2002 , na kwamba mnamo Desemba 28 mwaka jana, huko Kimara King’ong’o  Stopover, wote kwa pamoja walitenda kosa hilo kwa kutaka kutumia  sumu kwa lengo la kumdhuru  Denis Msaki  ambaye ni Mwanahabari wa Gazeti la Mwananchi ambalo ni kinyume na kifungu cha 227 cha sheria hiyo.
Wakili Rweyongeza alilitaja  kosa la pili kuwa ni la kula njama  ambalo pia ni kwaajili ya washitakiwa wote  ambalo ni kinyume na kifungu cha 24(2) cha Sheria ya Kuzuia Ugaidi Na.21 ya mwaka 2002, ambapo washitakiwa hao walitenda kosa la ugaidi la  kutaka kumteka Msaki  kinyume na kifungu  cha 4(2)(c) (iii) cha Sheria ya Kuzuia Ugaidi ya mwaka 2002.
Aidha alilitaja kosa la tatu  kuwa ni kutenda kufanya mkutano wa kupanga kufanya makosa ya ugaidi  kinyume na kifungu cha 59(a) cha Sheria ya Kuzuia ugaidi kwamba Desemba 28 mwaka jana,walishiriki katika mkutano wa kupanga kufanya vitendo vya kumteka nyaraka Msaki  kinyume na kifungu 4(2)(c) (iii) cha Sheria ya Kuzuia Ugaidi.
Wakili Rweyongeza alilitaja shitaka la nne ambalo linamkabili Lwakatare peke yake ni aliwezesha kutendeka kwa kosa la ugaidi kinyume na kifungu cha 23(a) cha sheria ya kuzuia ugaidi , kwamba Desemba 28 mwaka jana, Lwakatale akiwa ni mmiliki nyumba hiyo ilipo Kimaraka King’ong’o  kwa makusudi  aliliruhusu  kufanyika kwa kikao hicho baina yake na Ludovick  cha kutenda kosa la ugaidi la kutaka kumteka nyara Msaki hata hivyo walikanusha mashitaka hayo.
Wakili Rweyongeza  alidai kuwa makosa  hayo yameletwa chini ya sheria mbili tofauti yaani kosa la kwanza linaangukia katika sheria ya Kanuni ya Adhabu lakini kosa makosa yaliyosalia yanaangukia kwenye Sheria ya Kuzuia ugaidi na kwamba makosa yanaoangukia kwenye sheria ya ugaidi huwa  hayana dhamana na kwamba ni Mahakama Kuu peke ndiyo yenye mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.
Wakili Rweyongeza aliieleza mahakama kuwa jamhuri inawasilisha ombi la pili ambapo wanaiomba mahakama imruhusu mshitakiwa wa pili(Ludovick) aende kukaa chini ya ulinzi wa jeshi la polisi kwasababu Jeshi la polisi linamuiitaji kwaajili ya hatua za kiupelelezi zaidi.

Hata hivyo mawakili wa utetezi Peter Kibatara aliomba mahakama iwapatie wateja wake dhamana na kwamba suala la washitakiwa kupatiwa dhamana au kunyimwa ni la mahakama.
Kwa upande wake wakili Lissu alidai aliita hati ya mashitaka kuwa ni kipande cha karatasi kilichowasilishwa na DPP-Dk Feleshi ambacho akionyeshi nembo ya serikali, mhuri na wala hiyo hati ambayo aliipachika jina la kipande cha karatasi kuwa hakikuletwa mahakamani hapo kwa ridhaa ya DPP na kwamba anaiomba mahakama hiyo isiiamini hicho kipande cha karatasi kuwa ni nyaraka halali ya serikali.. Kwa upande wake wakili Profesa Abdallah Safari aliomba mahakama irejee kesi za kupambikiwa zilizowai kufunguliwa mahakamani hapo na ofisi ya DPP miaka ya nyuma ikiwemo kesi ya mauji ya fundi majeneza wa Manzese ya mwaka 2002, iliyofunguliwa na jamhuri dhidi ya Sheikh Issa Ponda na Sheikh Kundecha ambapo yeye alikuwa akiwatetea washitakiwa hao ambapo alilazimika kwenye kuonana na DPP wa wakati huo ambaye ni Jaji mstaafu kwa sasa Juxon Mlai na kumueleza kuwa kesi ile ya mauji ni ya kubambikwa ambapo Mlai alitumia mamlaka yake kuifuta kesi ile.

“Katika kesi hii ya Lwakatare ninachokiona ni matumizi mabaya ya sheria na wale waliombakizia kesi Lwakatare wanastarehe na kufurahi kuona Lwakatare anaenda kuishi gerezani”
alidai Profesa Safari.
Akipangua hoja za mawakili hao wa utetezi, wakili wa serikali Rweyongeza alidai kuwa hoja hizo tatu zilizowasilishwa na mawakili wa utetezi ni dhaifu na kwamba anaomba mahakama isiione kesi hii ni ya macho ya chama fulani ya kisiasa, tunaomba mahakama itambue kuwa kesi hii imefunguliwa na upande wa jamhuri na wala haijafunguliwa na chama cha siasa.
Kuhusu hoja ya kuwabambikizia kesi washitakiwa hao,Rweyongeza ambaye alikuwa akionyesha kujiamini alidai kesi hiyo siyo ya kubambikiziwa  na kwamba ofisi ya DPP inafanyakazi yake kwa mujibu wa sheria  na haipo kwaajili ya kubambikia watu kesi na kwamba kama Profesa Safari anaushahidi Lwakatare kabambikiwa kesi basi aende kuonana na DPP na ampatie huo ushahidi unaonyesha washitakiwa wamebambikiwa kesi.
Akiijibu hoja ya Lissu kuwa DPP amewasilisha kipande cha karatasi kisicho na kibali cha DPP, wakili Rweyongeza alimtaka Lissu aache kasumba ya kuongea mambo bila ya kufanya utafiti kwani DPP amefungua kesi hiyo na amewasilisha kibali chake mahakamani hapo ambapo wakili huyo aliklitoa kibali hicho kama kielelezo hali iliyofanya watu kuanza kuangua vicheko.
Aidha kuhusu hoja ya kutaka washitakiwa wapatiwe dhamana, wakili Rweyongeza alidai kuwa sheria ya ugaidi imetungwa na bunge na bunge  ambapo kifungu cha 49 cha Sheria ya Kuzuia Ugaidi kinakataza kabisa mshitakiwa anayeshtakiwa kwa makosa yanayoangukia kwenye sheria ya ugaidi kupewa dhamana na kwamba washitakiwa hao makosa yanayowakabili yanaangukia kwenye ya ugaidi hivyo mahakama haiwezi kuwapa dhamana.
“Sasa nawashangaa hawa mawakili wa washitakiwa leo hii wanajifanya hawajui matakwa ya kifungu cha 49 cha sheria ya ugaidi kinasema nini.Sheria ya ugaidi imetungwa na bunge hivyo ni sheria halali na kama mawakili wa utetezi wanaona sheria hiyo ni mbaya basi haraka sana nawashauri waende mahakama kuu wafungue kesi ya kikatiba ya kupinga kifungu hicho cha sheria ya ugaidi  lakini kwasasa sisi tunasema sheria ya ugaidi ipo kihalali na ndiyo imetumika kuwashitaki washitakiwa hawa”alidai wakili Rweyongeza.
Kwa upande wake hakimu mkazi Emilius Mchauru alisema amesikiliza hoja za pande zote mbili na kwamba atatolea uamuzi kesho na kuamuru washitakiwa wote wapelekwe gerezani

No comments:

Post a Comment