Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta Amsimamisha Kazi Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA),Madeni Kipande
Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta amemsimamisha kazi Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Madeni Kipande kutokana na kile kilichoelezwa kuwa uendeshaji mbovu wa utoaji wa zabuni.
Aidha, amemteua Awadhi Massawe kushika wadhifa huo. Kabla ya uteuzi huo, Massawe alikuwa Meneja wa Bandari.
Akizungumza
na waandishi wa habari, Sitta alisema uamuzi huo umetokana na kuwapo
malalamiko ya kutofuatwa kwa taratibu za zabuni na ucheleweshaji wa
barua kwa wanaoshinda.
“Ni
muhimu sana taratibu zetu za ununuzi katika bandari ziwe wazi na
ziheshimike duniani kote, maana miradi hii ni mikubwa sana inayopitishwa
na bodi ya zabuni ya TPA,” alisema.
Sitta
alisema, aliyekuwa Waziri wa Wizara hiyo Dk Harrison Mwakyembe alianza
kushughulikia masuala hayo, lakini hayajakaa vizuri. Alisema hakuna
uwazi na kumekuwa na ubabaishaji mkubwa, ikiwemo kubadilika majina ya
kamati za kutathmini zabuni.
Wakati huo huo Sitta ameunda timu ya watu sita itakayochunguza tuhuma za Kipande. Imepewa wiki mbili iwe imefanya kazi hiyo.
Timu
hiyo itaongozwa na Jaji mstaafu, Augusta Bubeshi na Katibu wake,
Deogratius Kasinda ambaye ni mtumishi wa Wizara ya Uchukuzi.
Wajumbe
wengine wa timu hiyo ni Mkurugenzi Mkuu mstaafu wa Mamlaka ya Manunuzi (
PPRA) Dk Ramadhani Mlinga, Samson Lugigo , Happiness Senkoro na Flavian
Kinunda ambao walishawahi kushika nyadhifa za juu ndani ya TPA.
“Nimejitahidi
kuchukua hawa wastaafu kwa sasa hivi hawatafuti cheo chochote, naamini
watatenda haki, watachunguza tu bila kufanya uonevu,” alisema Sitta.
Waziri
Sitta alisema bandari ni eneo muhimu, kwani takwimu zinaonesha kwamba
asilimia 43 ya makusanyo ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), yanatokana
na kodi ya ushuru wa forodha. Kati ya makusanyo hayo, asilimia 87
yanakusanywa kupitia Bandari ya Dar es Salaam.
Kwa upande wa Kipande, alisema hawezi kupinga hatua iliyochukuliwa na waziri .
Hata hivyo, alisema anaamini kipindi chote cha uongozi wake, alifanya ambayo yalikuwa sahihi na hana wasiwasi na uamuzi huo.
"Mimi
sina wasiwasi na hilo sababu huo ni uamuzi wake; lakini nina imani kuwa
katika bandari hii, nimefanya kile ambacho nilikuwa natakiwa kufanya,
hivyo sina shaka na hilo," alisema Kipande.
Katika
hatua nyingine, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za
Serikali (PAC), Kabwe Zitto ametaka serikali kujenga matangi ya
kuhifadhia mafuta na kujenga bomba la mafuta kwenda mikoani.
Aidha,
kamati hiyo imetaka TPA kuangalia uwezekano wa kununua hisa 50 za
Kampuni ya Kuhifadhi Mafuta (Tiper) imilikiwe kwa asilimia 100 na
Serikali.
Kuhusu
ujenzi wa matangi, Zitto alisema hatua ya Serikali kujenga matangi yake
ya kuhifadhi mafuta, itasaidia kujua kiasi cha mafuta yanayoingia na
kuweza kukadiria kodi kwa uhakika.
Akitoa
mfano wa Kenya, alisema Serikali inamiliki matangi ya kuhifadhia
mafuta, wanayapima kujua kiasi cha mafuta kilichoingia na kukitoza
kodi kabla ya kupelekwa kwenye matangi ya waagizaji.
“
Walichofanya, wamemtaka kila muagizaji kuwa na flow meter yake na
yakitoka kwenye meli yanaingia kwenye matangi ya Serikali na baada ya
kujua kiasi na kutozwa kodi hupelekwa kwa walionunua,” alisema.
Zitto
alisema wakati umefika sasa kwa serikali kujenga mabomba ya
kusafirishia mafuta na kwa kuanzia yakawa matatu, ambayo yatasaidia
kuondoa mfumo wa sasa wa kusafirisha kwa magari.
“Linaweza
kujengwa bomba moja kwenda Mbeya, likawa na matoleo kwa ajili ya mikoa
ya Morogoro, Iringa na mikoa iliyo jirani, kwa kufanya hivyo tutaondoka
na hali ya sasa ya kusafirisha mafuta kwa magari,” alisema.
Alisema
katika kuimarisha reli, ni vyema ukaanzishwa mfumo wa kutoza kodi
asilimia 1.5 kwa kila bidhaa inayoingia nchini na fedha hizo ziimarishe
usafiri wa reli.
“Kwa
sasa asilimia 99 ya mizigo inasafirishwa kwa barabara, hili si jambo
jema kwa uchumi, najua nikisema hivyo wenye malori watalalamika, lakini
wanaweza kufanya biashara nyingine,” alisema.
Kwa
upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa TPA, Awadhi Massawe alisema asilimia
60 ya mafuta yanayoingia nchini hupitia kwenye boya la Single Buoy
Mooring (SBM).
Alisema
wamejipanga kujenga mita ya kisasa ya kupimia mafuta maeneo ya
Kigamboni huku ile ambayo haitumiki, wamepanga kuiboresha na kuwa ya
kisasa.
Kuhusu
maendeleo ya ujenzi wa gati namba 13 na 14 ambazo zabuni yake iliingia
utata, Massawe alisema ripoti ya maandishi wataipeleka kwa Kamati hiyo
ya Bunge ifikapo Machi Mosi mwaka huu.
Pia,
Massawe alisema hatua ya kitengo cha kupakua kontena kupewa mtu
binafsi, inawapunguzia mapato na kuwa hiyo ndio sekta ambayo inaingiza
fedha nyingi.
No comments:
Post a Comment