Tibaijuka abishana dakika 415, Chenge aenda Mahakama Kuu
Dar es
Salaam. Wakati Mbunge wa Muleba Kusini, Profesa Anna Tibaijuka jana
alitumia dakika 415 (takribani saa 7) akibishana katika mpambano mkali
wa kisheria kuhusika kwake katika sakata la Akaunti ya Tegeta Escrow,
mwenzake wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge aliamua kutimkia Mahakama
Kuu kukwepa kuhojiwa na Baraza la Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa
Umma.
Jana,
mwenyekiti wa baraza hilo, Jaji Hamisi Msumi alitoa uamuzi kuhusu
pingamizi la Chenge aliyetaka baraza hilo lisisikilize shtaka lake la
kukiuka maadili ya uongozi wa umma.
Hata
hivyo, Chenge alikwamisha kwa mara ya pili baada ya kuomba kwenda
Mahakama Kuu kutafuta tafsiri iwapo baraza hilo linaweza kusikiliza
shauri lake kinyume na amri ya mahakama iliyoagiza lisijadilie na
taasisi kwa kuwa kuna kesi kadhaa mahakamani zinazohusiana nalo.
Profesa
Tibaijuka na Chenge kila mmoja aliingiziwa Sh1.6 bilioni kwenye akaunti
zao binafsi kutoka kwa mkurugenzi wa VIP Engineering iliyokuwa ikimiliki
asilimia 30 ya hisa za kampuni ya Independent Power Solution Limited
(IPTL).
Baraza
hilo, linasikiliza mashauri hayo kuhusu ukiukwaji wa Sheria ya Maadili
ya Viongozi wa Umma namba 13 ya mwaka 1995 katika vipengele vya matumizi
mabaya ya madaraka na sakata la escrow.
Chenge,
juzi katika baraza hilo alipoitwa kuhojiwa aliibua hoja ya zuio la
Mahakama Kuu na baada ya mabishano ya kisheria, Jaji Msumi alisema
angekwenda kuisoma amri huyo kisha kutoa uamuzi wake jana.
Akisoma
uamuzi huo, Jaji Msumi alisema: "Mlalamikiwa ametoa hoja ya amri ya
Mahakama Kuu kuwa ndiyo hiki kinachojadiliwa, chimbuko lake ni miamala
ya Akaunti ya Tegeta Escrow ambalo chimbuko lake ni bungeni na mahakama
ilizuia lakini amri hiyo haizuii mamlaka hii."
"Orodha
ya taasisi zilizotajwa hailihusu baraza hili, wadaiwa wote pamoja na
mawakala, watumishi, wasaidizi wao au watu wengine wanaofanya hili. Amri
iliyoandikwa, Baraza si mlengwa wa hili. Kinachozuiwa kufanywa ni
kupelekwa bungeni au kujadiliwa taarifa ya (Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa
Hesabu za Serikali pamoja na umiliki wa IPTL," alisema.
Akihitimisha
kusoma uamuzi wa baraza hilo, Jaji Msumi alisema: "Hoja iliyotolewa na
mlalamikiwa haina msingi na tunaomba kuendelea kulisikiliza."
Mara
baada ya kumaliza, Chenge aliyekuwa amevalia shati la kitenge na suruali
nyeusi akiwa haonyeshi kuwa na wasiwasi alisema: "Nashukuru kwa uamuzi
huo lakini sina nia ya kubishana, natoa hoja ya kukata rufaa ya kwenda
Mahakama Kuu ili mahakama itafasiri kama Baraza lina mamlaka ya kujadili
suala hili."
Chenge
ambaye pia aliwahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali alisema: "Kama
wanasheria wa sekretarieti wangejituma kidogo kwenda masijala ya
Mahakama Kuu kupitia wangeliona hili. Amri hii ya zuio ni pana kuliko
uamuzi wa Baraza lako uliofikia, naomba nitumie nafasi hii kwenda
Mahakama Kuu."
Akihitimisha
hoja hiyo, Jaji Msumi alisema: "Nakuruhusu, niongeze tu sina hakika
kama kanuni zimetengenezwa kuruhusu rufaa na kama hazipo kutakuwa na
utaratibu. Ukipeleka itasaidia kujenga Baraza lakini Mahakama Kuu ina
haki, kila mtu ana haki kwa suala lolote, mimi siwezi kukuzuia."Mara
baada ya uamuzi huo, Chenge akiwa anatoka ukumbini waandishi wa habari
walianza kumpiga picha huku wengine wakimtaka kuzungumzia uamuzi wake wa
kupeleka suala hilo Mahakama Kuu, lakini yeye alisema: "Nani anataka
nimpeleke tuisheni," kauli iliyowafanya waandishi hao kucheka.
Profesa Tibaijuka
Shauri la
Profesa Tibaijuka lililoanza kusikilizwa saa 3:16 asubuhi hadi saa 5:18
asubuhi kabla ya kuahirishwa na kurejea tena saa 6.30 mchana hadi
lilipohitimishwa saa 11.23 jioni, lilivuta hisia za wananchi na
watumishi mbalimbali wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Barbro
Johansso wakiongozwa na Mkuu wa Shule hiyo, Halima Kamote.
Mashtaka
Akisoma
hati ya malalamiko dhidi ya mbunge huyo wa Muleba Kusini, mwanasheria wa
Sekretarieti ya Maadili, Wemaeli Wilfred alisema: "Mheshimiwa Profesa
Anna Tibaijuka kwa kutumia wadhifa wake (waziri wa ardhi, nyumba na
maendeleo ya makazi) alishawishi na kuomba na kupokea fedha Sh1.617
bilioni kutoka kwa James Rugemalira.
Mara baada ya kumaliza kusoma hati hiyo, Wakili wa Profesa Tibaijuka, Rugemeleza Nshala alisimama na kusema: "Tunayakataa yote."
Kutokana
na kauli hiyo, Jaji Msumi aliingilia kati na kusema: "Hii siyo mahakama
ya kisheria, taratibu zetu siyo za kimahakama, hivyo ni vizuri
kuyafikiria hayo."
Ushahidi
Baada ya
kauli hiyo shahidi wa Sekretarieti, Waziri Kipacha ambaye pia ni Katibu
Msaidizi, Idara ya Siasa ya Sekretarieti alisimama na kuanza kutoa
ushahidi wake akiongozwa na Wilfred.
Shahidi
huyo alisema alichokifanya Profesa Tibaijuka (kuomba na kupokea fedha
hizo) wakati huo akiwa waziri, ni kinyume na sheria za maadili ya
vingozi wa umma.
"Kuna
tatizo, kwa mujibu wa masharti ya maadili ya viongozi wa umma
hawaruhusiwi kuomba maslahi ya kiuchumi kutoka kwa mtu yeyote,
mheshimiwa Tibaijuka Februari 12 mwaka 2014 alipokea fedha kutoka VIP
Sh1.617 bilioni...hapa kuna tatizo la kimaadili."
Kipacha
aliendelea kulieleza baraza hilo kuwa: "Kiongozi wa umma haruhusiwi
kupokea maslahi ya kiuchumi lakini mheshimiwa Tibaijuka alifanya hivyo
akijua kuwa ni makosa kutokana na sheria ya maadili ya viongozi wa
umma."Profesa Tibaijuka kupokea kiasi kikubwa cha fedha kama hicho na
wadhifa aliokuwa nao wa uwaziri ni ukiukwaji wa sheria za viongozi wa
umma mheshimiwa mwenyekiti. Viongozi wa umma wanapaswa kuzingatia
maadili wanapokuwa na uhusiano na kampuni au taasisi binafsi."
Baada ya
maelezo hayo, Wakili Nshala alimuuliza Kipacha kuwa ni kosa gani
alilolifanya kupokea mchango wa shule kama alivyokwishaeleza?
Kipacha
alijibu: "Hapa ni ukiukwaji wa sheria ya maadili, Profesa Tibaijuka
alipokea mchango ambao ni kiasi kikubwa cha fedha tena kwa kupitia
akaunti yake binafsi, jambo ambalo ni kinyume kabisa cha sheria hii."
Nshala
aliuliza tena: "Je, kama kiongozi wa nchi yetu ana jukumu la kuhamasisha
na kusaidia watoto wetu kupata elimu, sasa hapa Profesa Tibaijuka kosa
lake ni lipi?
Kipacha
alijibu: "Kama kusaidia kwa kutoa fedha zake mfukoni siyo kosa na kama
unachangisha au kuhamasisha watu kuchangia elimu na fedha hizo
zinakwenda moja kwa moja kwa walengwa siyo kosa, lakini fedha hizo
zikiingia moja kwa moja kwako hapo ni makosa kwa mujibu wa sheria hii ya
maadili ya viongozi wa umma."
Nshala
aliendelea kumuuliza, "Baada ya kufuatilia ninyi kwa uchunguzi wenu
baada ya yeye (Profesa Tibaijuka) kuingiziwa fedha mlibaini nini?"
Kipacha
kwa upole na kujiamini wakati wote alijibu: "Tulibaini fedha hizo
zilianza kutoka kwa mafungu. Februari 18, 2014 zilitoka Sh1 bilioni
kwenda Bank M na Machi 12, 2014 zilitoka Sh500 milioni kwenda Bank M na
kubakiwa na Sh117 milioni katika akaunti yake ambayo hatujui alizifanyia
nini. Lakini mwenyekiti hapa lalamiko ni ukiukwaji wa maadili tu."
Nshala
aliuliza tena: "Kwa nini katika uchunguzi wenu hamkwenda kuwahoji Bank M
au bodi ya wadhamini wa shule kwa kuwa ndiko fedha zilikwenda na iwapo
wao walitoa uamuzi huo?
Kipacha alisema: "Kwa mujibu wa sheria hii sisi hatukuona sababu ya kwenda kuwahoji wao."
Baada ya
kauli hiyo, Jaji Msumi aliingilia kati na kusema: "Katika uchunguzi wenu
kwa nini hamkwenda kuhoji zaidi wakati mnasema kuna taasisi imenufaika
kwa nini hamkwenda huko?
Akijibu hoja hiyo, Kipacha alisisitiza kuwa hawakuona sababu ya kufanya hivyo.
Sh10
milioni za mbogaHoja iliyoibua vicheko barazani ni kauli ya Profesa
Tibaijuka kuwa kati ya fedha hizo alichota kwanza Sh10 milioni za
kununua mboga.
Akitoa
utetezi wake ambao mara zote ulikuwa ukiwafanya watu waliojaa ukumbini
humo kuangua vicheko, Profesa Tibaijuka akihojiwa na mwanasheria wa
sekretarieti hiyo, Getiruda Cyriacus aliyetaka kujua kama fedha hizo
ziliingia Februari 12, 2014 kwa nini zilitoka Februari 18, mwaka huo na
wakati huo huo kuna kiasi cha Sh10 milioni kilitoka mapema?
Profesa Tibaijuka alisema: "Nilitoa kiasi hicho kwenda kununua mboga, kwani kuna kosa gani."
Akiendelea,
Profesa Tibaijuka alisema: "Uongozi mzima wa shule ya Babro wanafanya
kazi kwa uadilifu, uwazi na ukweli wa hali ya juu na mimi kuomba mchango
wa kuwasaidia watoto wa kike waliokuwa hawana fursa ya kupata elimu
bora sioni kosa lake.
"Harakati
hizi zitaendelea kwani nimekuwa nikizifanya nje na ndani ya nchi na
ndiyo maana Rais mstaafu, Benjamini Mkapa alitupa kiwanja cha shule hiyo
inayopigiwa kelele na yeye alishachangia fedha na watu wengine wakiwamo
wafadhili wakubwa, mfano Serikali ya Sweden iliyochangia zaidi ya Sh8
bilioni lakini leo hii Sh1.6 inanidhalilisha hapa."
Aliongeza:
"Mimi ni mstaafu wa Umoja wa Mataifa nina mafao yangu napata na nina
akaunti za benki kama 10 ndani na nje ya nchi, sasa hii ya Rugemalira
kama ningetaka angeiingizia katika akaunti nyingine, lakini yeye alisema
ili asaidie shule nifungue akaunti Benki ya Mkombozi, sasa
ningefanyaje?
Profesa
Tibaijuka aliongeza, "Leo hii nadhalilishwa na kusimamishwa hapa kwa
harakati zangu za kumkomboa mtoto wa kike, niwahakikishie kuwa
nitaendeleza harakati hizi na malengo yangu ni kuhakikisha kila kanda
kunakuwa na shule hizi za mfano, tulianza na Dar es Salaam, Bukoba sasa
tunatafuta kiwanja Mwanza na Mbeya."
Mbunge
huyo aliambatana na mashahidi wake wawili, Balozi Paul Rupia ambaye ni
mlezi wa Bodi ya Wadhamini wa shule hiyo na mwenyekiti wa bodi hiyo,
Simon Odunga ambao wote kwa pamoja walisema fedha walizopokea kutoka kwa
Rugemalira kupitia akaunti ya Profesa Tibaijuka zilitumika kulipa deni
la Sh2 bilioni walilokuwa wakidaiwa na Bank M, ambalo hata hivyo
halikumalizika.
Baada ya
utetezi huo, Jaji Msumi alizitaka pande zote ziandae majumuisho ambayo
yatawasilishwa kabla ya Machi 13 mwaka huu, ili Baraza liandae
mapendekezo ya siri yatakayopelekwa kwenye mamlaka za juu.CHANZO:MWANANCHI
No comments:
Post a Comment