TIFFAN ENT

TIFFAN ENT

TUKO WANGAPI

TUKO WANGAPI

GLORY FREIGHT

GLORY FREIGHT

Tuesday, February 24, 2015

Taarifa Rasmi ya Jeshi la Polisi Kuhusiana na Sakata la Kutekwa kwa Wanajeshi wa JKT Waliotaka kuandamana Kudai Ajira


Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam linawashikilia vijana watano wa kundi la wahitimu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa tuhuma za kufanya uchochezi na kufanya mikusanyiko isiyo halali jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari, Kamishna wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alisema vijana hao wamekamatwa kwa nyakati tofauti kwa makosa ya kuunda kikundi kisicho halali kwa mujibu wa sheria za nchi na kuwahamasisha wenzao, kuandamana hadi Ikulu kwa Rais Jakaya Kikwete kudai ajira za kudumu.
 
“Tunawashikilia vijana watano ambao ndio viongozi wa kikundi kinachojiita umoja wa wahitimu wa Jeshi la Kujenga Taifa. Mwenyekiti ndio alikuwa wa kwanza kukamatwa na wengine tuliwakamata juzi mara baada ya kukusanyika eneo la Msimbazi Centre na Muhimbili,” alisema Kova.
 
Akieleza chanzo cha vijana hao kutaka kuandamana kuelekea Ikulu, alidai wahitimu hao wanadai kuahidiwa ajira za kudumu walipomaliza mafunzo yao na hivyo baada ya kukaa kwa muda mrefu bila kuajiriwa, ndipo wakaamua kuanzisha kikundi hicho ili kwenda kumwona Rais  Kikwete kumweleza tatizo la ajira linalowakabili.
 
“Vijana hawa wanadai kuwa waliahidiwa kupewa ajira za kudumu mara baada ya kumaliza mafunzo yao ya JKT.
 
" Jambo hili sio la kweli, kwani tumefanya uchunguzi na kubaini hakuna mkataba wowote unaosema wakimaliza mafunzo lazima waajiriwe, bali kila mtu anatakiwa kutumia ujuzi alioupata kujiajiri.  
 
"Lakini walipokaa kwa muda mrefu  bila kuona ahadi yao inatekelezwa, wakaamua kuanzisha kikundi chao ambacho sio halali kwa mujibu wa sheria za nchi.
 
"Hadi sasa tumeandaa jalada la mashitaka na tumelikabidhi kwa mwanasheria wa serikali kwa ajili ya kuwafikisha mahakamani watuhumiwa hawa kujibu mashitaka yanayowakabili,” aliongeza Kova katika taarifa yake.
 
Alitaja vijana wanaoshikiliwa na Polisi kuwa ni Mwenyekiti wa kikundi hicho George Mgoba (28) mkazi wa Mabibo Loyola, Katibu wao Linus Emmanuel (28) mkazi wa Tabata, Emmanuel Richard (28) mkazi wa Kawe, Jacob Joseph (36) mkazi wa Mabibo na Rizione Ngowi (27) mkazi wa Mtoni Mtongani.
 
Akizungumzia tuhuma za kutekwa na kuteswa kwa George Mgoba, Kova alisema Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi ili kubaini tukio hilo kama ni la kweli na kwanini watu hao walimteka.
 
 “Tunaendelea na uchunguzi kubaini kama ni kweli kijana huyo alitekwa kama anavyodai kuwa Februari 16 alitekwa na kupatikana tarehe 19 majira ya saa  nne usiku huko Tungi Kibaha kandokando ya barabara, pia tujue ni akina nani walimteka na kwasababu zipi kisha watu hao tutawapeleka mahakamani,” alisema Kova.
 
Kova alieleza kuwa “Februari 22 mwaka huu majira ya saa kumi na moja jioni, George Mgoba alijaribu kutoroka wadini katika Hospitali ya Muhimbili lakini polisi walibaini ujanja wake na kufanikiwa kumweka kizuizini. Lengo lake ilikuwa ni kukimbia matibabu na kuzua hofu kwa wananchi”.
 
Kwa sasa Mwenyekiti huyo wa vijana hao bado amelazwa katika  Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, akipatiwa matibabu. 
 
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Umma na Huduma kwa Wateja katika Hospitali  hiyo ya Muhimbili, Aminiel Aligaesha  alisema jana kuwa hali ya mtu huyo, inaendelea vizuri na afya yake imeimarika.
 
Wakati huo huo, katika taarifa yake kwa vyombo vya habari baadaye jana, Kova alimtaka Makamu Mwenyekiti wa Vijana hao, Parali Kiwango (25) mkazi wa Temeke Mikoroshini ajisalimishe mara moja Polisi kwa ajili ya mahojiano zaidi, kabla jeshi hilo halijaanza kumtafuta.
 
“Jeshi la Polisi linamtaka Makamu Mwenyekiti ajisalimishe mara moja kwani jana alipoona Katibu wake amekamatwa alikimbia na kutokomea kusikojulikana. 
 
"Yeye kama ni mhitimu wa JKT hatakiwi kukimbia, bali ajisalimishe mwenyewe katika ofisi ya Mkuu wa Upelelezi Polisi Kanda  Maalumu Dar es Salaam au kituo chochote cha Polisi kilicho karibu na alipo,” aliongeza Kova.

No comments:

Post a Comment