Sheria mpya ya vibali vya ajira yaja
WIZARA ya
Kazi na Ajira iko katika mchakato wa kuandaa Sheria mpya ya utoaji wa
vibali vya ajira kwa wageni ili kudhibiti kuajiriwa kwa wageni ili
kufanya kazi ambazo Watanzania wenyewe wanaweza kuzifanya.
Waziri
katika wizara hiyo, Gaudentia Kabaka aliliambia Bunge kuwa sheria hiyo
itatoa mwongozo juu ya utoaji vibali, kwani sasa kumekuwa na sehemu
nyingi hivyo kuwa na sehemu moja pamoja na adhabu kwa wageni wanaofanya
kazi zinazoweza kufanywa na Watanzania.
Alisema
mchakato huo uko karibu kukamilika na utapelekwa bungeni kutokana na
ratiba na kueleza kuwa itasaidia kudhibiti wafanyakazi wageni wanaoingia
nchini bila utaratibu maalum na kusababisha kuajiliwa kwenye kazi
ambazo wenyeji wanaweza kufanya.
Waziri
alisema hivi karibuni walibaini wageni 300 walioingia nchini kufanya
kazi katika kiwanda cha saruji cha Dangote, Mtwara kwa kazi zinazoweza
kufanywa na watanzania.
Wakati
huo huo, wafanyakazi zaidi ya 350 wa Kampuni ya mgodi wa Bulyanhulu
waliodai kuachishwa kazi baada ya kupata madhara wakiwa kazini
wametakiwa kwenda kwenye Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA)
kupimwa ili kuthibitisha iwapo walipata madhara hayo kutokana na kazi
walizokuwa wakifanya ili kuweza kutibiwa.
Alisema
kuwa OSHA ndiyo wenye mamlaka ya kuthibitisha kuwa wafanyakazi hao
wameathirika na kwa utaratibu walitakiwa kupeleka OSHA barua kutoka kwa
mwajiri ili kuweza kupimwa na kujua athari walizopata wakiwa kazini
lakini tangu wafukuzwe kazi mwaka 2007 hawakupeleka barua hiyo.
“Tumegundua
kuwa wafanyakazi hao hawakuwa na uhusiano mzuri na chama cha
wafanyakazi hivyo kusababisha ufuatiliaji wa suala hilo kuwa mgumu hivyo
ninawaagiza kwenda OSHA Dar es Salaam wakapime kwani wako tayari wao
pamoja na wengine 50 waliofukuzwa “alisema Kabaka.
Pia
alitaka chama cha wafanyakazi migodini (TAMICO) kuwaunganisha
wafanyakazi hao ili kufuatilia kwa pamoja na kuepusha kuwa mmoja mmoja.
Mbunge wa
Kisarawe, Suleiman Jafo (CCM) alisema wafanyakazi hao wamekuwa
wakihangaika katika ofisi mbalimbali ikiwemo kwenye Wizara ya Kazi na
Ajira kufuatilia suala hilo.
No comments:
Post a Comment